Makala

Ruto: Nilijumuisha Azimio kwenye serikali ili sote tuitwe Zakayo

Na SAMMY WAWERU August 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto ametetea vikali hatua yake ya kujumuisha upinzani kwenye serikali ya Kenya Kwanza kupitia uteuzi wa baadhi ya wanasiasa wa Azimio, kujiungva na Baraza lake la Mawaziri.

Akizungumza katika Kaunti ya Embu Jumatano, Agosti 7, 2024, Rais Ruto alisema hatua hiyo itamsaidia kuletea nchi maendeleo.

Akifafanua, kiongozi wa nchi alisema kupitia serikali ya umoja wa kitaifa watasaidiana kuangazia changamoto zinazozingira nchi.

“Niliapa kuunganisha Wakenya wote, na juzi nimetengeza serikali inayojumuisha kila mtu. Hata wale walikuwa wanapiga kelele nje, nimewaambia kujeni tuketi pamoja ndio hii pesa tutafute pamoja, madeni tulipe pamoja, na ushuru tutafute pamoja,” Rais alisema.

Julai 2024, siku chache baada ya kuvunja Baraza lake la Mawaziri, Rais Ruto aliteua Mabw John Mbadi kuwa Waziri wa Fedha na Hazina ya Kitaifa, Opiyo Wandayi (Kawi), Gavana wa zamani Mombasa Hassan Joho (Madini na Uchumi Samawati na aliyekuwa Gavana wa Kakemega, Wycliffe Oparanya kusimamia Wizara ya Vyama vya Ushirika na Maendeleo ya Biashara Ndogo Ndogo na zile za Kadri, wote wakiwa ni wanasiasa wa upinzani – Azimio.

Kufuatia kuendelea kupanda kwa gharama ya maisha na uchumi ambapo Dkt Ruto amekuwa akikosolewa kwa kuongeza ushuru wa ziada (VAT) hasa kwa bidhaa muhimu za kimsingi, wakosoaji wake wamempa jina la utani la Zakayo.

Zakayo ni mhusika kwenye Biblia ambaye alikuwa mtoza ushuru tajiri na mkuu wa watoza ushuru Jericho, ambapo Yesu alipokuwa akipita eneo hilo alitaka kumwona.

Hata hivyo, hakuweza kumwona kwa sababu ya kimo chake cha ufupi akiwa kwenye umati mkubwa wa watu waliojitokeza, hivyo basi akalazimika kupanda mti aina ya mkuyu.

Yesu alipomwona, alimtaka ashuke haraka akisema yeye – Yesu atakuwa mgeni nyumbani kwake na watu waliposkia hayo wakaanza kunung’unika, wakilalamika ameenda kwa mtu mwenye dhambi.

Rais Ruto amenukuliwa mara kadha akihoji hashtuliwi na watu kumuita Zakayo.

Akitetea uteuzi wa wanasiasa kadha kutoka Azimio kujiunga na Baraza la Mawaziri wa serikali ya Kenya Kwanza, alidai yeye hataki kuitwa Zakayo pekee yake.

“Mimi sitaki kuwa Zakayo pekee yangu, kila mtu akuje akuwe Zakayo hapa ndani,” Dkt Ruto aliambia umma eneo la Kanyuambora, Mbeere Kaskazini kufuatia ziara yake Kaunti ya Embu.

Katika kile kilionekana kama kuainisha uwazi wa utendakazi wake hasa katika ukusanyaji ushuru, Rais alisema fedha hizo zinapokusanywa huelekezwa kwenye akaunti ya Hazina ya Kitaifa.

“Kwani ile ushuru inakusanywa inapelekwa kwa akaunti yangu (Ruto)? Inapelekwa kwa akaunti ya Hazina ya Kenya. Kila mtu akuje hapa tuongee hiyo maneno, vile tutalipa madeni, vile tutatafuta ushuru, vile tutapanga maendeleo ili Kenya iende mbele,” alifafanua.