MakalaSiasa

JAMVI: Sababu fiche za vita vya Raila na Ruto

February 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES WASONGA

MITAZAMO kinzani katika ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto kuhusu wazo la kubuni kwa wadhifa wa Waziri Mkuu imeibua maswali si haba.

Hii ni licha ya hali kwamba wawili hao wanakubaliana kuwa katiba inapaswa kufanyiwa marekebisho. Lakini wanatofautiana kuhusu aina ya marekebisho hayo na lini yanapopaswa kutekelezwa.

Juzi Bw Odinga alisema kuwa mabadiliko ya Katiba kupitia kura ya maamuzi yatafanyika mwaka huu.

Alitoa kauli hiyo alipokutana na ujumbe wa muungano wa wanafunzi wa vyuo vikuu vya humu nchini afisini mwake katika jumba la Capitol Hill, Nairobi akiwaonya wale ambao watajaribu kupinga shughuli hiyo akisema watawekwa kando. Hapa bila shaka alikuwa akirejelea Dkt Ruto na wandani wake.

Kulingana na kiongozi huyo wa chama cha ODM, mfumo wa uongozi unapaswa kugatuliwa kupitia kubuniwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka na manaibu wake wawili. Mashikilizi wa afisi hii mpya atafanya kazi kwa ushirikiano na Rais na naibu wake kuendesha serikali.

Wazo hili lilipata uungwaji mkono kutoka kwa Baraza la Kitaifa la Makanisa Nchini (NCCK), baadhi ya makundi ya mashiriki ya kijamii na baadhi ya wanasiasa kama vile Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

Naye Rais Uhuru Kenyatta ameonekana kuchangamkia wazo la kugatuliwa kwa mamlaka makuu “kama njia ya “kusambaza mamlaka kiusawa na kuzuia mtindo wa mshindi kutwaa kila kitu”. Hata hivyo, Rais hajabainisha wazi ikiwa anataka mabadiliko ya katiba kufanikisha pendekezo hilo yafanyike mwaka huu anavyotaka Bw Odinga.

Lakini kwa upande wake Dkt Ruto anapinga wazo la Bw Odinga kwamba kura ya maamuzi ifanyike mwaka huu akisema serikali haina pesa za kufadhili mpango huo.

Isitoshe, akiongea mujuzi katika kituo cha Chatham House jijini London Dkt Ruto alipendekeza kwamba Katiba ifanyiwe mabadiliko ili kubuniwe Afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani.

Kulingana naye, cheo hicho kinapaswa kutengewa mgombeaji urais ambaye ataibuka nambari mbili katika uchaguzi.

“Kubuniwa kwa cheo cha Waziri Mkuu sio suluhu ya shida inayotukabili sasa ambapo watu walioshindwa katika uchaguzi mkuu wanahisi kwamba wao na wafuasi wao wametengwa kiuongozi. Hii ni kwamba sababu kuna uwezekano mkubwa wa chama kilichoshinda urais pia kupata wadhifa wa Waziri Mkuu kwani mshikilizi wa wadhifa huo sharti atoke chama au muungano wenye wabunge wengi katika mabunge yote mawili,” akasema.

Lakini wachanganuzi wa masuala ya kisiasa, kisheria na uongozi wanasema kuwa sababu kuu ya Dkt Ruto kupinga kuanzishwa kwa wadhifa wa waziri mkuu ni kwamba anataka kufurahia mamlaka makuu ambayo Rais Kenyatta anafurahia wakati huu.

Mbunge wa Mugirango Magharibi Vincent Mogaka anasema kuwa haja kuu ya Dkt Ruto ni kurithi mamlaka makuu kutoka kwa bosi wake na ndiyo maana anapinga kuanzishwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu.

“Baada ya kuhudumu kama Naibu Rais tangu 2013 na hata kuhudumu kama “kaimu rais” wakati mmoja Bw Kenyatta alipoenda katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC) Dkt Ruto anafahamu utamu wa wadhifa huo. Hii ndio maana hataki kubuniwe wadhifa wa Waziri Mkuu ambao bila shaka utanyofoa sehemu ya mamlaka ya urais,” anasema mbunge huyo ambaye pia ni wakili.

Naye wakili James Mwamu anasema msimamo wa Dkt Ruto unatokana na makubalino kati yake na Rais Kenyatta mnamo mwaka wa 2012 walipobuni muungano wa kisiasa ulioshirikisha vyama wa United Republican Party (URP) na The National Alliance (TNA).

“Japo makubaliano hayo yalikuwa ya kisiri, Rais Kenyatta aliwaambia wafuasi wao waziwazi, haswa kutoka Rift Valley, kwamba waliafikiana kwamba baada yake kukamilisha kipindi chake cha miaka 10 ikuluni atamuunga mkono Dkt Ruto naye ashikilie urais kwa miaka mingine 10,” anasema.

Wafuasi wa Dkt Ruto, kulingana na Bw Mwamu, wangali wanaamini kwamba “urais” ambao Rais Kenyatta alikuwa akirejelea ni ule mwenye mamlaka kama ulivyo sasa.

“Hii ndio maana Bw Ruto na wafuasi wake wanaamini kuwa kuanzishwa kwa cheo cha waziri mkuu kutavuru ndoto yake ya kurithi mamlaka ya urais ambayo Rais Kenyatta anafurahia sasa,” akasema wakili huyo.

Naye Bw Barasa Nyukuri, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uongozi, anasema wadhifa Waziri Mkuu unafaa kuanzishwa nchini lakini katika hali ambapo haileti migongano katika kitovu cha utawala wa nchi.

“Naibu Rais William Ruto hafai kupinga wazo la kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu kwa sababu huenda jambo hilo likamfaidi yeye mwenyewe na chama chake cha Jubilee. Ni wazi kuwa mshikilizi wa cheo hicho sharti atoke chama au muungano wenye idadi kubwa ya wabunge…. na hali hii inaweza kufaidi chama cha Jubilee ikiwa kitadumisha umaarufu wake hadi 2022,” anasema Bw Nyukuri.

Wakati huu chama cha Jubilee na vyama vingine vilivyomuunga mkono Rais Kenyatta katika uchaguzi wa 2017 kina uungwaji mkono wa jumla ya wabunge 216 katika bunge la kitaifa na maseneti 38 katika seneti.

Hii ina maana kuwa ikiwa kura ya maamuzi itafanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 na kubuniwe wadhifa wa waziri mkuu ni wazi kuwa cheo hicho kitatwalikwa na mrengo wa Jubilee. Na baadhi ya wadadisi wanasema kuwa huenda hata Rais Kenyatta akapewa wadhifa wa Waziri Mkuu ikiwa cheo hicho kitabuniwa na aendelee kushikilia wadhifa wa kiongozi wake.

Hali kama hii ambapo chama kimoja kinatoa Rais na Waziri Mkuu kwa wakati mmoja umewahi kushuhudiwa nchini Urusi mwaka wa 2008 pale Rais Vladimir Putin alimteua mwandani wake Dimitry Medvedev kuwa waziri mkuu

Hii ndio maana mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati anaonya kwamba mjadala kuhusu kubuniwa kwa wadhifa kwa Waziri Mkuu unapasa kuendeshwa kwa uangalifu ili kuzuia hali ilivyo nchini Urusi.