Makala

Sababu ya kamati kudinda kuunda nafasi ya kiongozi wa upinzani bungeni

Na SAMWEL OWINO October 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto na kinara wa upinzani Raila Odinga wamepata pigo baada ya Kamati ya bunge kukataa mapendekezo kadhaa yaliyomo kwenye ripoti ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO).

Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Haki na Sheria inasema katika ripoti yake iliyowasilishwa bungeni kwamba, imekataa kuundwa kwa wadhifa wa kiongozi rasmi wa upinzani kupitia mswada wa sheria ikisema pendekezo kama hilo linahitaji kura ya maamuzi na haliwezi kufanywa kupitia bunge.

Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba, 2024 unahusu masuala matatu makuu kama vile uchaguzi, kukitwa kwa Ofisi za Serikali na fedha katika katiba, kufuta kazi mbunge na kutangazwa kwa uchaguzi wa urais miongoni mwa mambo mengine.

Ripoti ya NADCO ilitokana na muafaka wa pande mbili kati ya Rais Ruto na Bw Odinga kufuatia maandamano ya kupinga serikali na ilitoa mapendekezo mengi yanayohusu marekebisho ya sheria na sera na masuala waliyolalamikia Wakenya.

Miongoni mwa Miswada iliyotokana na ripoti hiyo ni pamoja na Mswada wa (Kubadilisha) Katiba ya Kenya 2023, ambao ukiidhinishwa na Bunge utabadilisha muundo wa serikali ukilenga kuanzishwa kwa afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani na kukita afisi ya Mkuu wa Mawaziri, Hazina ya Uangalizi ya Seneti na Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneobunge (NG-CDF) miongoni mwa zingine.

Kamati hiyo katika ripoti yake inasema kwamba kukita Ofisi ya Kiongozi wa Upinzani katika katiba kunagusia ukuu wa katiba, mamlaka ya watu, maadili ya taifa na misingi ya utawala, na hivyo kunahitaji kura ya maamuzi.Kamati hiyo inakosoa mapendekezo hayo ikisema hakuna mfumo wa kitaasisi wa kuanzishwa kwa ofisi hiyo na pia haijabainika iwapo ofisi hiyo itakuwa ya umma au ya Serikali.

‘Kuanzishwa kwa afisi kama hiyo katika mfumo wa sasa wa serikali ya Kenya lazima kufafanuliwe kwa uwazi kulingana na mfumo wa kitaasisi na jukumu lake,’ inasema ripoti hiyo.

Kamati hiyo ilibaini kuwa pendekezo hilo linahujumu mfumo wa sasa wa utawala wa rais nchini.

Kamati hiyo ilieleza kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 108 ya Katiba, kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa kimsingi ndiye kiongozi wa upinzani bungeni na hivyo kuanzishwa kwa Ofisi ya Kiongozi rasmi wa Upinzani kunabadilisha majukumu ya Bunge na ni lazima kufanywe kupitia kura ya maamuzi.

Kamati hiyo hata hivyo ilipitisha pendekezo la kutaka mwenyekiti wa IEBC asitangaze matokeo ya urais bila kuthibitishwa na makamishna.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022 makamishna wanne wa IEBC wakiongozwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Juliana Cherera, Justus Nyang’aya, Francis Wanderi na Irene Masit walisusia matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na aliyekuwa mwenyekiti wa wakati huo Wafula Chebukati wakisema hawakuyathibitisha.

Pia ilipitishwa pendekezo la kuongeza muda wa kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi za uchaguzi wa urais kutoka siku 14 za sasa hadi siku 21.

Kamati hiyo pia ilipitisha pendekezo katika ripoti ya NADCO inayotaka kuongeza kiwango cha chini cha usawa cha mapato ya kitaifa kinachotengewa serikali za kaunti kutoka asilimia 15 za sasa hadi asilimia 20.