Sababu ya NEMA kufunga viwanda 12
Na BERNARDINE MUTANU
Serikali inajitahidi kuhifadhi Mto Nairobi ambao kwa kiwango kikubwa umechafuka, na ambao ni moja ya matawi ya Mto Athi.
Viwanda 12 vimefungwa kwa kuchafua Mto Nairobi na vingine 48 kuonywa kuhusu uchafuzi wa mito na viini vya maji Nairobi na Mombasa.
Mamlaka ya Kusimamia Mazingira (NEMA) ilionya kuwa ikiwa viwanda hivyo havitatekeleza sheria kwa kuhakikisha kuwa havichafui maji mitoni, hata navyo vitafungwa.
Viwanda hivyo vilipewa makataa ya siku saba hadi siku 14 kutekeleza sheria hizo, “Ikiwa hatukuvifunga, inamaanisha kuwa hali sio mbaya sana na vinaweza kurekebisha hali katika muda mfupi. Ikiwa havitafanya hivyo, tutavifunga,” alisema Prof Geoffrey Wahungu, Mkurugenzi Mkuu wa NEMA wakati wa ziara sehemu tofauti Nairobi.
Viwanda hivyo vilipewa maagizo ya kurekebisha hali baada ya kupatikana kukiuka sheria kuhusu usimamizi wa maji taka.
Vilipatikana kutoa kuachilia kemikali na uchafu mwingine katika bomba la maji taka na kuchafua Mto Nairobi, na hivyo Mto Athi.
“Viwanda hivyo vitasalia kufungwa mpaka vitekeleze sheria zote kuhusu usimamizi wa maji taka,” alisema Prof Wahungu wakati wa mkutano na wanahabari baada ya kufunga Giloil, Viwandani.
Uchunguzi uliofanyiwa maji taka kutoka kiwandani humo ulionyesha kuwa maji hayo hayakuwa safi kiwango cha kuachiliwa kuingia katika mfumo wa maji taka.
Baadhi ya viwanda vilivyoathiriwa ni pamoja na Supra Textile Limited na Sunflag Company, eneo la Viwandani. Kampuni hizo zilisimamishwa kutengezeza bidhaa mpaka wakati zikapokuwa na kiwanda cha kusafisha maji taka.
NEMA pia ilifunga kampuni ya Herbatula mpaka itimize masharti kutoka kwake kuhusu maji take, “Kampuni hiyo haina mfumo wa kusafisha maji taka na pia leseni ya kuachilia maji chafu kutoka kwa NEMA licha ya kutumia asidi katika utengenezaji wa bidhaa zake,” ilisema NEMA.
Kampuni zingine zilizoathirika ni pamoja na EPZ, Kariobangi na vituo vya kuuza mafuta eneo la Karen, ambazo zilipewa maagizo ya kuboresha hatua zake za kusafisha maji taka, Basco Paints na kampuni ya kutengeneza vyuma ya APA.
Prof Wahingu alisema operesheni hiyo itaendelea mpaka viwanda vyote victimize masharti na kutekeleza sheria.
Hata hivyo, mamlaka hiyo iliidhinisha kufunguliwa kwa kampuni ya Africa Apparel, eneo la Viwandani, ambayo ilifungwa zaidi ya wiki moja iliyopita baada ya kutimiza matakwa.
Wakati huo, NEMA ilionya kampuni ya maji na usafi ya Nairobi kwa kuachilia maji taka kuingia Mto Nairobi.
“Kiwanda cha kampuni hiyo cha kusafisha maji chafu kiliharibika, kinafaa kurekebishwa haraka iwezekanavyo,” alisema mwenyekiti wa Bodi ya NEMA Bw John Konchella alipozuru eneo la Korogocho, Nairobi.
NEMA ilizindua mpango wa siku 100 kuchunguza viwanda, kampuni na taasisi kuhakikisha kuwa zimetimiza sheria kuhusu mazingira. Hivyo, kampeni ya kufunga na kufungua kampuni na viwanda katika muda wa wiki kadhaa zijazo.
“Serikali imechukua hatua makusudi kusafisha Mto Nairobi, kuanzia kiini chake mpaka unakoungana na Mto Athi kuhakikisha kuwa maji yanatiririka yakiwa safi kabisa,” alisema.
Uchafuaji wa Mto Nairobi na Mto Athi umezua malalamishi miongoni mwa wananchi ambao hutumia maji yake.
Ni hali hiyo ambayo ilipelekea serikali kuchukua hatua. Afisa Msimamizi wa Mazingira katika Kaunti ya Nairobi Vesca Kangogo kwa kusisitiza umuhimu wa kusafisha Mto Nairobi alisema maji chafu yataathiri bwawa la Thwake, ambalo linajengwa kaunti za Machakos, Makueni na Kitui.
“Hatuwezi kubali Bwawa la Thwake, litakalopokea maji kutoka Nairobi kuchafuka kutokana na shughuli zinazoendelea Nairobi,” alisema Jumatano eneo la Korogocho, wakati wa shughuli za kusafisha mto huo.
Wakati wa shughuli ya kusafisha mto huo eneo la Korogocho, malori 200 ya taka yalizolewa kando ya mto huo, licha ya taka zaidi kuendelea kurundikwa humo.
Kulingana na afisa huyo, Serikali ya Kaunti ya Nairobi imetenga Sh400 milioni za kusafisha mto huo katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020.
Serikali kupitia kwa Nairobi Regeneration campaign na Serikali ya Kaunti ya Nairobi imekuwa na kampeni kubwa ya kusafisha mto huo na matawi yake, Ngong na Mbagathi.