Makala

Sababu ya vijana Afrika kumpenda Traore

Na John Kamau May 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KATIKA miji, mitaa, masoko na mitandao ya kidijitali kote Afrika, jina la Rais wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, linatajwa kwa shauku isiyo ya kawaida kwa kiongozi wa nchi.

Picha yake inachorwa kwenye kuta za miji, inachapishwa kwenye fulana na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii kama vile masihi.

Kwa kizazi kilichotamaushwa na ahadi zilizovunjika na kutegemea ukoloni mamboleo, kapteni huyu mwenye umri wa miaka 36 kutoka Burkina Faso amekuwa zaidi ya kiongozi — ni ishara ya uasi, heshima na ujasiri. Uso wa kizazi kipya cha Pan-Afrika.

Kapteni Traoré aliponyakua madaraka Septemba 2022, kwa kumpindua Rais wa mpito Paul-Henri Sandaogo Damiba, wachache nje ya Ouagadougou walielewa uzito wa kilichokuwa kimefanyika. Haya hayakuwa tu mapinduzi mengine katika ukanda wenye misukosuko ya kisiasa, bali ni mpasuko wa kizazi.

Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Ouagadougou na kamanda wa zamani wa kikosi cha mizinga, Kapteni Traoré alijiwasilisha si kwa kiburi cha dikteta, bali kwa utulivu wa mtu aliye na dhamira: kuikomboa nchi yake kutoka kwa ufyonzwaji wa kigeni na kuirudisha kwa watu wake. Hakusita kutangaza nia ya kurudisha rasilmali za Afrika mikononi mwa wenyewe. Wakati Traoré aliponyakua mamlaka, mataifa ya Magharibi yalitilia shaka kimya kimya, lakini umaarufu wake miongoni mwa vijana ulilipuka kama cheche kwenye majani makavu.

Ujumbe wake unaeleweka. Katika kuapishwa kwa Rais John Mahama nchini Ghana Januari 7, Traoré alipokelewa kwa shangwe kubwa kuliko marais wengine 21 wa Afrika waliokuwepo. Haikuwa tu makofi — ilikuwa ni tamko kutoka kwa vijana waliokatishwa tamaa kisiasa. Ndani ya Traoré, wanamwona kama mwiba dhidi ya ubeberu wa kiuchumi wa Magharibi, urejesho wa heshima ya Afrika, na labda, mfano wa uongozi mpya — si kwa cheo, bali kwa misingi.

Kwa vyombo vya habari vya Magharibi, yeye ni “mwenye mamlaka kupita kiasi.” Jenerali Michael Langley, mkuu wa majeshi ya Amerika barani Afrika, alimwita Traoré “mtu hatari” katika ukanda wa Sahel, hali iliyochochea maandamano katika miji mbalimbali kuonyesha wazi uungwaji mkono kwa Traoré. Katika hotuba yake mbele ya Bunge la Seneti la Amerika, Langley alimlaumu Traoré kwa kutumia akiba ya dhahabu ya nchi kwa faida ya utawala wa kijeshi badala ya wananchi kwa ujumla. Lakini kwa Waburkinabe wengi, tuhuma hizo zinaonekana kuwa za kinafiki. Kama alivyosema Ocibi Johann, msanii wa muziki, akizungumza na Associated Press: “Kwa sababu Colin Powell (waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Amerika) alidanganya, Iraq iliharibiwa. Barack Obama (rais wa zamani wa Amerika) alidanganya, Muammar Gaddafi (rais wa Libya) aliuawa. Lakini safari hii, uongo wao hautatuathiri. Ndiyo maana tunawaambia – hatuwapingi – lakini tunapinga ufyonzaji na utumwa wa kiuchumi.”

Kwa mamilioni barani Afrika na katika nje ya bara, Traoré ni mkombozi — Sankara mpya aliyevaa sare, sauti jasiri dhidi ya tamaa ya kibeberu, na kielelezo cha ndoto ya muda mrefu: Afrika huru inayojitawala.

Kupaa kwake kunafufua kumbukumbu ya Thomas Sankara, “Che wa Afrika,” ambaye kwa miaka minne tu, alifafanua kwa vitendo jinsi uongozi wa mageuzi unaweza kuonekana Afrika. Mgogoro wake na mataifa ya kibeberu, sera zake za kujitegemea, usawa wa kijinsia na vita dhidi ya ufisadi vilimfanya apendwe na watu wa Burkina Faso na kuwa tishio kwa maslahi ya nje. Kama Traoré, Sankara alithubutu kutetea ardhi na raslimali, kukataa misaada ya kigeni na kupinga ushawishi wa Magharibi. Lakini mageuzi ya Sankara yalikatizwa na risasi katika mapinduzi yanayoaminika kuungwa na mataifa ya kigeni.

Traoré, kwa sasa, anaandika hadithi yake mwenyewe. Na hadi sasa, inagusa mioyo ya kizazi kinachotamani mabadiliko.

Tofauti na watangulizi wake, alichukua hatua za haraka kufanikisha sera kwa misingi ya kanuni. Alifuta nyongeza ya mishahara kwa maafisa wa serikali iliyotangazwa na mtangulizi wake, huku yeye akibaki na mshahara wake wa kawaida wa kijeshi. Aliwafukuza majeshi maalum ya Ufaransa kutoka Burkina Faso, akidai kuwa walikuwa wakimlinda rais aliyepinduliwa — madai ambayo Ufaransa imeyakana vikali. Lakini kwa kufanya hivyo, Traoré aliweka msimamo wazi: Burkina Faso haitakuwa tena chombo cha kuchezewa na wengine.

“Kwa vijana, utawala wa Traoré ni nafasi ya kuonyesha kile vijana wanaweza kufanya. Lakini kwa Waburkinabe wa kawaida, kipaumbele ni kuboresha maisha yao ya kila siku,” inasema Taasisi ya Masuala ya Usalama (ISS).

Inaonekana Traoré anakuwa uso wa Afrika mpya na thabiti — Afrika inayojinasua kutoka kutegemea wengine kiuchumi na kurejesha udhibiti wa rasilimali zake. Alipoanzisha ujenzi wa kiwanda cha kwanza cha kusafisha dhahabu nchini humo Novemba 23, 2023, haikuwa tu mradi wa miundombinu. Ilikuwa ishara ya kuvunja historia ya kuchimba bila kusindika, ya utajiri kutoka barani huku umaskini ukibaki.

Serikali yake inataifisha migodi miwili mikubwa ya dhahabu na kusitisha usafirishaji wa dhahabu ghafi kwenda Ulaya. Sasa, Burkina Faso ina kiwanda kipya cha kusafisha dhahabu chenye uwezo wa kuchakata tani 150 kwa mwaka — ishara ya mabadiliko kutoka uchimbaji wa malighafi hadi uzalishaji wa thamani ya juu.

“Hatutasafisha tena dhahabu yetu nje ya nchi, na sasa tutajua thamani halisi ya dhahabu ghafi kutoka migodi yetu,” alitangaza Traoré.

. Kwa miaka mingi, mataifa ya Afrika yamezalisha dhahabu lakini yamekuwa yakiisafisha nje — hasa Uswisi, China, au Afrika Kusini — hivyo kupoteza faida na udhibiti wa mfumo mzima wa thamani.

“Kapteni Traoré ni tumaini kwa Afrika,” alisema mfuasi mmoja jijini Ouagadougou. “Tumaini kwa watu Weusi, tumaini kwa wapiganiaji wa uhuru duniani kote.”

Sasa macho yote ya Afrika yanamwangalia. Je, Kapteni Traoré atakuwa kiongozi atakayetekeleza ahadi za mapinduzi ambazo wengi kabla yake walisahau? Au naye atamezwa na vishawishi vya madaraka?

Traoré pia amekataa mikopo na masharti kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, akisisitiza kuwa Burkina Faso haitaiweka rehani mustakabali wake. Kwa wafuasi wake, msimamo huu ni dalili ya bara linalojifunza kujisimamia lenyewe.

“Afrika inapaswa kushughulikia mambo ya Afrika,” wanasema.