Makala

Sababu za korti kuzima dili ya Adani ya Sh96 bilioni

Na SAM KIPLAGAT October 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA Kuu imezuia serikali kutia saini au kutekeleza mkataba wa Sh95.68 bilioni wa kujenga laini za kusambaza umeme kwa kampuni tanzu ya shirika la Adani Group kutoka India, Adani Energy Solutions Limited.

Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kilipata agizo hilo katika kesi kinachoshutumu serikali kwa kupanga mkataba wa mradi ulioanzishwa kibinafsi na Adani Energy Solutions wa kujenga na kuendesha laini kuu za usambazaji umeme na vituo vidogo kwa gharama ya Sh95.68 bilioni kwa muda wa miaka 30.

LSK ilisema mradi huo ulianzishwa kwa njia isiyo wazi, bila ushirikishaji wa maana wa umma na serikali imeficha kwa makusudi habari muhimu kuhusu mradi huo.

“Kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi iliyowasilishwa Oktoba 23 2024 amri ya muda inatolewa kusimamisha utekelezaji wa makubaliano yoyote ya mradi kati ya washtakiwa kwa pamoja na au kampuni na mashirika yoyote yanayohusiana na ujenzi wa laini za kusambaza umeme, vituo vidogo au miundombinu yoyote ya umeme,” Jaji Bahati Mwamuye alisema.

Kesi hiyo itatajwa Novemba 11 kwa maagizo zaidi.

Jaji huyo alisema kuwa LSK ilidai kwamba makubaliano hayo yalikuwa ‘udanganyifu wa kikatiba’ na ‘yana usiri na hayana kanuni za uadilifu, uwazi na uwajibikaji.’

“Baada ya kuzingatia masuala na nyenzo zilizowekwa mbele ya Mahakama hii na kwa kuzingatia masharti ya katiba na sheria, nimeridhika kwamba mlalamishi amekidhi vigezo vya kisheria vya kupatiwa maagizo ya muda,” alisema Jaji.

LSK imetaja Kampuni ya Usambazaji Umeme ya Kenya (Ketraco), Adani Energy Solutions Ltd, Mawaziri wa Fedha na Kawi na Petroli, John Mbadi na Opiyo Wandayi, mtawalia, Idara ya Ushirikiano wa Sekta ya Umma na ya Kibinafsi na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor, kama washtakiwa katika kesi hiyo.

‘Laini na vituo vidogo ni mali muhimu ya kitaifa ambayo isipokuwa mahakama hii ikikosa kuingilia kati, itakodishwa kwa mashirika ya kigeni kwa kukiuka kabisa kanuni za uwazi, uwajibikaji, usawa na matumizi ya busara ya pesa na rasilimali za umma,’ LSK ilisema.

LSK iliongeza kuwa kutokana na athari za utekelezaji wa pendekezo la kusimamia miundombinu ya umeme na gharama ya kawi, ni muhimu mahakama iamue uhalali wake wa kikatiba wa dili ya serikali na Adani ili kulinda maslahi ya umma.

Stakabadhi za mahakama zilisema kuwa makubaliano na kampuni ya Adani yanapendekeza kujenga laini mpya ya kilomita 206 ya Thika-Malaa- Konza, ya kilomita 95 inayounganisha Rongai-Keringet-Chemosit na takriban kilomita 98 kutoka Menengai-Ol-Kalou-Rumuruti.

Alipokuwa akitangaza mpango huo mapema mwezi huu, Bw Wandayi alisema makubaliano hayo yaliashiria mwanzo wa mpango wa mageuzi wa kuendeleza, kufadhili, kujenga na kuendesha na kusimamia laini kuu za usambazaji na vituo vidogo vya stima kote nchini.

Hapo jana, Mahakama Kuu ilituma kesi nyingine ya kupinga mpango wa kukodisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kampuni ya Adani Group kwa Jaji Mkuu Martha Koome, ili ateue jopo la majaji watatu.

Jaji John Chigiti alisema kesi ya Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK) na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC), inaibua masuala mazito ya kikatiba na akatuma faili hiyo kwa Jaji Mkuu

KHRC na LSK zilipinga mpango huo zikisema kuwa JKIA ni mali ya kimkakati ya kitaifa na kwa hivyo mpango huo, hauna mashiko na unakiuka kanuni za utawala bora, uwajibikaji, uwazi, na matumizi ya busara ya pesa za umma.

‘Kesi itapelekwa kwa Jaji Mkuu ili kuteua jopo la majaji kuisikiliza’ alisema jaji.

Mashirika hayo mawili yamepinga mpango huo yakisema kuwa utanyima umma, na kuhamishia Adani, mapato yote ya sasa yanayotoka JKIA,

LSK ilisema kwamba ingawa mradi huo unaitwa wa Ushirikiano wa Kujenga na Kusimamia, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege

vya Kenya (KAA) itakabidhi uwanja wa ndege uliopo na unaofanya kazi kwa Adani na baada ya miaka 30, Adani, itabaki na asilimia 18 ya biashara JKIA.

Imetafsiriwa na Benson Matheka