Sababu za Raila kukosa udhibiti wa kisiasa Luo Nyanza
Na CHARLES WASONGA
KUSHINDWA kwa mgombeaji wa ODM katika uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Ugenya kumeibua maswali mengi mno kuhusu iwapo hiyo ni dalili ya kiongozi wa chama hicho Raila Odinga kuanza kupoteza udhibiti wa eneo la Luo Nyanza kisiasa.
Lakini kulingana na wadadisi, mipango mibaya kutozingatia haki katika kura ya mchujo, matumizi ya lugha chafu nyakati za kampeni, kiburi na vitisho ni miongoni wa sababu zinazodidimiza nyota ya Bw Raila Odinga kisiasa katika eneo hili ambalo ni ngome yake.
Hii ndio maana, wanasema, David Ochieng’ aliyewania kwa tiketi ya chama ndogo cha Movement for Democracy and Growth (MDG) alimbwaga, kwa urahisi Chris Karan aliyefanyiwa kampeni na vigogo wa chama hicho cha chungwa wakiongowa na Seneta wa Siaya James Orengo.
Bw Ochieng’, ambaye alihudumu kama mbunge wa eneo hilo tangu 2013 hadi 2017, alipata kura 18,730 dhidi ya kura 14,507 alizopata Bw Karani.
Na hali ilikuwa mbaya zaidi kwa ODM katika eneobunge la Embakasi Kusini, Bw Julius Mawathe wa Chama cha Wiper alipoimzima kwa kuzoa kura 21,628 dhidi ya 7,988 zake mgombeaji wake, Irshad Sumra.
Matokeo ya Ugenya yalisawiriwa kama ya kuaibisha ODM kwa sababu eneobunge hilo liko katika kaunti ya Siaya nyumbani kwa Bw Odinga na seneta Orengo, ambaye ni mshirika wake mkuu.
Na Waziri Mkuu huyo wa zamani alionekana kung’amua uwezekano wa kupata kichapo hicho mapema mwezi Machi alipowasihi wakazi wa Ugenya wasimwaibishe kwa kumwangusha Bw Karan.
Akiongea katika halfa ya mazishi ya chifu wa zamani, Daudi Owino, katika kijiji cha Sifuyo Bw Odinga alisisitiza kuwa itakuwa jambo la aibu kwa ODM kushindwa na wagombeaji wa vyama ambavyo “vinadhaminiwa na wapinzani wetu”.
“Kwa sababu ya umoja na moyo wa kufanya kazi pamoja, Rais Kenyatta hakudhamini mgombeaji katika chaguzi ndogo za Ugenya na Embakasi Kusini. Rais pia alidhihirisha kuwa ananiunga mkono pale alipokosa kudhamini mgombeaji katika uchaguzi mdogo wa useneta wa Migori mwaka jana. Sasa je, itakuwa aibu iliyoje ikiwa mtu mwingine atatwaa kiti hiki cha ugenya ambacho ameniachia? Nawasihi mpigie kura mgombeaji wangu,” Bw Odinga akaomba.
Kiongozi huyo wa ODM alidai kuwa macho ya Wakenya yameelekezwa kwa eneo bunge la Ugenya, “ikizingatiwa kuwa ni muhimu kwa ODM kudumisha kiti hiki,”
Usemi huu wa Bw Odinga uliashiria kuwa ushindi kwa Bw Karan ungekuwa sawa na ushindi kwake. Hii ndio maana wadadisi, na Wakenya kwa ujumla, walichukulia kushindwa kwa mgombeaji huyo wa ODM kama kushindwa kwa Bw Odinga “nyumbani kwake.”
Kulingana na Bw Martin Andati, usemi huu wa Bw Odinga ndio chimbuko la propaganda ambazo zilienezwa na Orengo na wenzake kwamba “kura kwa Ochieng’ ni sawa na kura kwa Naibu Rais William Ruto.”
Hata hivyo, akiongea na Jamvi la Siasa kwa njia ya simu, Bw Ochieng’ alikana kuwa alikuwa “mradi” wa Dkt Ruto akisema iliibuka wapiga kura wa Ugenya walimchagua kwa misingi ya rekodi yake ya maendeleo.
Lakini alikubali kuwa alipata usaidizi kutoka kwa “marafiki kadha ambao walichangia hela chache kufadhili kampeni zangu.”
“Ningependa kubainisha wazi kwamba sikuchaguliwa kwa sababu ya uungwaji mkono kutoka kwa Naibu Rais. Kampeni zangu zilipigwa jeki na marafiki zangu wengine wao wakiwa mawakili wenzangu. Na muhimu zaidi ni kwamba watu wa Ugenya waliniunga kutokana na rekodi yangu ya maendeleo,” Bw Ochieng’ akasema.
Kulingana na Bw Andati, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, ODM haikuwasoma ipasavyo wapigakura wa Ugenya ili kubaini kile ambacho walikuwa wanataka katika uchaguzi huo.
“ODM walidhani kuwa watu hao wangeshawishika na siasa za kuwarushia matusi wale wanaodhaniwa kuwa mahasidi wa Bw Odinga. Chama hicho kilidhani kwa wananchi watachangamkia lugha ya matusi, siasa za kumwondoa Dkt Ruto mamlakani kwa tuhuma za ufisadi na vitisho dhidi ya wapigakura,” anasema.
Kulingana na Bw Andati, mtindo kama huu wa kuendesha siasa za uchaguzi zimepitwa na wakati akisema kuwa wananchi wamezinduka na wanataka siasa zilizosheheni sera za maendeleo.
Kwa upande wake, Dkt Tom Mboya anamshauri Bw Odinga kwamba anapaswa kubadili mtindo wa siasa zake ikiwa anataka kuendelea kudhibiti sio tu siasa za ndani bali hata zile za nje ya ngome yake ya Luo Nyanza.
“Kwanza kabisa, Bw Odinga anapaswa kuzingatia matakwa ya raia kwa kuhakikisha kuwa yanaheshimiwa wakati wa kura za mchujo za chama hicho. Huu mwenendo wa kuwapokonya vyeti vya uteuzi watu wenye umaarufu mkubwa miongoni mwa wananchi ndio umeikosesha ODM viti vingi vya ubunge tangu 2013,” anasema.
“Pili, Bw Odinga anapaswa kuzika katika kaburi la sahau siasa za kiburi, matusi na uenezaji wa propaganda zisizo na msingi endapo chama hicho kinalenga kudumisha ushawishi wake katika Luo Nyanza,” anaongeza Dkt Mboya ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Maseno.
Msomi huyu anabashiri kwamba vyama vingine vya kisiasa vitaendelea kupenyeza katika eneo hilo na ngome zingine za Bw Odinga ikiwa chama hicho hakitajisaili kwa lengo la kubadili mitindo yake ya kuendesha shughuli zake.
“Hilo lisipofanyika basi Bw Odinga ajiandae kwa aibu zaidi, kuliko ile aliyopata Ugenya, katika uchaguzi mkuu wa 2022,” anasema Dkt Mboya.
Hata hivyo, Ugenya sio eneobunge la kwanza katika Luo Nyanza ambalo ODM imepoteza.
Itakumbukwa kwamba katika uchaguzi mkuu uliopita, ODM ilipoteza viti kadha vya ubunge katika Luo Nyanza kutokana na kile kilichotajwa kama usimamizi mbaya wa kura za mchujo.
Katika eneobunge la Suna Magharibi mbunge wa sasa Bw Peter Masara aliyewania kama mgombeaji huru, alimshinda Bw Joseph Obiero Ndiege wa ODM huku Bw Shakeel Shabir akitamba dhidi ya Nicholas Odongo kule Kisumu Mjini Mashariki.
Na katika eneobunge la Kisumu Mjini Magharibi Bw Olago Aluoch aliyewania kwa tiketi ya Ford Kenya alimbwaga John Awiti wa ODM.
Lakini Bw Odoyo Owidi anapinga dhana kwamba kushindi wa wawaniaji wa vyama vingi katika Luo Nyanza ni ishara ya kudhoofika kwa ushawishi wa Odinga katika eneo hilo.
Kulingana mdadisi huyu, hali hiyo ni kielelezo cha wananchi kuamua kutumia uwezo walio nao kuwachagua viongozi wanaoamini kuwa watawaletea maendeleo.
“Hali hii haionyeshi kuwa makali ya Odinga kisiasa yanapungua katika ngome yake. Wananchi bado wanampenda na kumheshimu wangali wanamtegemea kuwapa mwelekeo wa kisiasa na masuala mengine ya kitaifa. Kwa wao kuwachagua wabunge wanaowataka haonyeshi ukaidi kwa Bw Odinga,” anasema.
Wachanganuzi, wafuasi wa ODM na Wakenya kwa jumla wanasubiri kuona namna ambavyo ODM itashughulikia makosa yaliyosababisha kushindwa kwake katika ngome zake huku ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022.