Makala

Safiri salama 'Papa', tutaonana baadaye

July 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

NA THOMAS MATIKO

JUMAMOSI iliyopita majira ya alasiri tasnia ya burudani ilipatwa na simanzi kufuatia kifo chake mchekeshaji Charles Bukeko al-maarufu Papa Shirandula.

Papa Shirandula alifariki dunia akiwa anasubiri kuhudumiwa katika hospitali ya Karen Hospital kwa mujibu wa mke wake anayeilaumu hospitali hiyo kwa kutomshughulikia kwa dharura.

Alikimbizwa huko baada ya kuugua ghafla. Jumatatu wiki hii, alizikwa nyumbani kwake Funyula, Kaunti ya Busia.

Lakini bado wadau wengi hasa mastaa wa kiwanda cha uigizaji na vichekesho wanaendelea kumuenzi mwenda zake. Lakini je, safari ya Papa ilianzia wapi?

AZALIWA KAKAMEGA

Papa alizaliwa miaka 58 iliyopita umri aliokuwa nao hadi anapumua mara yake ya mwisho, katika kijiji cha Buhalarire, Kaunti ya Kakamega.

Alikuwa ndiye kifungua mimba katika familia ya watoto wanne kwa mzee Cosmas Wafula na mkewe valeria Makokha.?Baada ya kumaliza masomo ya kidato, alihamia mjini Nairobi kuja kusaka maisha.

SAFARI YA UIGIZAJI

Mjini Nairobi, aliishi katika mtaa wa Uhuru maeneo ya Eastlands na mara kwa mara alikuwa akitembea kilomita za kutosha hadi mjini kujaribu bahati yake kwenye usahili mbalimbali uliokuwa ukiendelea kwenye kumbi la kitaifa la maigizo, Kenya National Theatre.

Baada ya kushiriki sahili kibao, aliishia kupewa kazi yake ya kwanza na mwelekezi Dkt JPR Ochieng Odera 1998.

Baada ya hapo aliishia kujiunga na kampuni ya uigizaji ya Phoenix Theatre ambako alikutana na mwigizaji mkongwe na mchanganuzi wa talanta na uigizaji ‘jaji’ Ian Mbugua.

Ian akamtambulisha Papa kwa mwalimu wa uigizaji James Forkland aliyempa mafunzo kwa kipindi cha miaka mitatu na toka hapo, mwendazake akawa ameiva maigizo.

DILI ZA MATANGAZO

Ukiachia mbali kipindi chake cha Papa Shirandula alichoigiza kwa miaka zaidi ya 10 akiwa mhusika mkuu, mwendazake pia alifanikiwa kuangukia dili kubwa kubwa na tamu tamu za kibiashara.

Miongoni mwa kampuni kubwa alizoshiriki kwenye biashara matangazo ya bidhaa zao ni kama GoTV ambako alikuwa ni balozi.

Lakini pia Safaricom walimtumia sana kwenye biashara za matangazo yao huku dili yake ya mwisho ikiwa wiki chache zilizopita.

Hata hivyo dili ya kwanza iliyomfungulia michongo hii ni alipohusishwa kwenye matangazo biashara ya kampuni ya Coca Cola 2001, tangazo lililoishia kuwa maarufu sana kote nchini.

Papa aliigiza kama dikteta Idi Amin Dada aliyekuwa anapinga utandawazi. Ni kweli tangazo hilo ambapo kauli aliotumia ‘Brrrrrr’ lilipata umaarufu mkubwa sana nchini kiasi cha kutumika kama neno la Sheng.

Shoo ya PAPA SHIRANDULA

Licha ya kuigiza sana, ni shoo ya ‘Papa Shirandula’ iliyomfungulia milango ya neema na kumpa michongo ya kutosha.

Kwenye shoo hiyo, Papa aliigiza kama bawabu wa tajiri fulani baada ya kutoka kijijini na kuja mjini kusaka kazi.

Shoo hiyo ilipeperushwa katika runinga ya Citizen na ilipigwa jeki na sapoti ya Meneja Mkurugenzi wa runinga hiyo Waruru Wachira.

Wachira alikuwa amepata fursa ya kutizama mojawapo ya maigizo ya ‘Papa Maloon’ 2006 ambapo aliigiza kama bawabu.

Hapo ndipo akamshauri kuja na wazo la shoo yake kuhusiana na maisha ya bawabu na ndio ikawa chimbuko la ‘Papa Shirandula’.?Lakini kando na shoo hiyo, pia Papa aliigiza kwa miaka miwili katika kipindi cha ‘Makutano Junction’ kilichopeperushwa runingani vile vile.

UTAJIRI

Limekuwa jambo la kawaida kushuhudia wasanii na wabunifu wakifariki dunia wakiwa wanapitia maisha ya umaskini licha ya kuwa maarufu, hata hivyo kwa Papa ilikuwa tofauti kidogo.

Hadi anakata pumzi, alikuwa ni mtu anayejiweza. Alitumia maarifa na akili yake kuwekeza kupitia shughuli zake. Papa anakadiriwa kuwa kaacha nyuma utajiri unaofikia Sh50 milioni.

AACHA MJANE NA WANA

Kutokana na uigizaji wake katika kipindi cha ‘Papa Shirandula’, wapo walioishia kuamini kuwa mwigizaji Wilbroda (Jackie Nyaminde) alikuwa ni mke wake haswa.

Hata hivyo katika uhalisia wa maisha yake, alikuwa kwenye ndoa na Beatrice Andega ambaye ni mjane kwa sasa.

Katika maisha yao ya ndoa, walijaliwa watoto watatu. Miaka miwili iliyopita, aliwahi kutania kuwa unene wake ulitokana na mapishi ya mke wake.

SHABIKI WA INGWE

Papa alikuwa ni shabiki mkubwa wa klabu ya AFC Leopards. Alikuwa akihudhuria mechi za timu yake na hasa Mashemeji Derby.

Kwenye mojawapo ya mahojiano yake ya awali, aliwahi kusema kuwa ushabiki wake kwa klabu hiyo ulianza alipokuwa na umri wa miaka minne tu.

Mwendazake alinukuliwa akisema kuwa babake alikuwa ni shabiki sugu wa Ingwe na mara nyingi angeenda naye uwanjani kucheki mechi zao na hapo naye akaishia kuipenda timu hiyo.

AZUSHIWA KIFO

Japo kwa sasa kauma pamba, Papa Shirandula aliwahi kauawa wakati akiwa hai. Hii ilikuwa ni mwaka jana ambapo kulizuka tetesi kwamba alikuwa kalazwa Nairobi Hospital baada ya kulalamika kuwa na maumivu ya mgongo, pamoja na kuumwa na kichwa.

Tetesi hizo zilidai kuwa alifariki akipokea matibabu na mwili wake ukahamishiwa katika mochari ya Lee Funeral Home.

Baada ya uvumi kusambaa, Papa alijitokeza na kusema kwamba alikuwa mzima wa afya. Ila safari hii kalala kabisa.

Kifo chake kimeifufua kibwagizo cha ‘hit’ yao Amos & Josh, ‘Baadaye’. “Safiri salama, msalimu Maulana, tutaonana baadaye…”