Makala

Sakaja: Ni muhimu kukubali Jubilee haiko kama zamani

September 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

SEPTEMBA  7, 2016, vyama zaidi ya 10 vilivunjiliwa mbali kuunda mrengo tawala kwa sasa wa Jubilee, JP.

Vinajumuisha The National Alliance (TNA) kilichoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, United Republic Party (URP) cha Naibu Rais Dkt William Ruto, Alliance Party of Kenya kilichoanzishwa na gavana wa sasa wa Kaunti ya Meru Kiraitu Murungi na New Ford Kenya cha Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa, miongoni mwa vingine.

Mbali na ajenda za maendeleo nchini, viongozi wake wakuu Rais Kenyatta na Naibu wake Ruto walisema kilipania kuleta umoja, utangamano na uwiano wa kitaifa.

Wakihutubu wakati wa kukizindua rasmi Jumatano, Septemba 7, 2016, walisema JP ni chama cha kitaifa, kilicholeta pamoja makabila yote nchini.

Aidha, walieleza kwamba chini ya utawala wa JP, kila jamii itashirikishwa serikalini.

Ni mrengo huohuo kiongozi wa taifa aliutumia kutetea wadhifa wake kwa awamu ya pili na ya mwisho, na ushawishi wao kwa wapiga ulizaa matunda.

Makubaliano yalikuwa Rais Kenyatta aongoze kiti cha hadhi ya juu zaidi nchini kwa muda wa miaka 10, unaotarajiwa kukamilika 2022, kisha naibu wake Dkt Ruto amrithi chini ya JP.

Katika harakati za kampeni, wawili hao walitambuana kama “ndugu yangu”.

Hata hivyo, kitumbua kinaonekana kuingia mchangani hususan baada ya salamu za maridhiano kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga, almaarufu Handshake Machi 9, 2018.

JP imegawanyika na kuunda mirengo miwili, Tangatanga kinachoegemea upande wa Rais na Kielewek cha Naibu wake.

Kufuatia mkondo wa siasa unaoshuhudiwa, aliyekuwa mwenyekiti wa TNA na ambaye kwa sasa ni seneta wa Nairobi, Johnson Sakaja, anasema umoja wa Jubilee uliokuwepo awali umefifia.

“Hakuna haja tudanganyane, umoja uliokuwepo awali haupo. Ingawa Jubilee haijasambaratika, lakini utangamano tulioshuhudia kabla ya 2017 hauonekani,” anasema Bw Sakaja.

Katika kisa cha hivi majuzi ambapo mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro alikamatwa na kuachiliwa huru kwa kile alidai ni idara ya polisi kutumiwa vibaya na baadhi ya viongozi serikalini.

Kuna mrengo ambao umekuja kutambulika  kama Tangatanga na ambao viongozi wake wanamuumga mkono Ruto.

Pia kuna kundi lingine la Kieleweke linalojiegemeza zaidi kwa Rais.

Nyoro anasema anapigwa vita kisiasa kwa sababu ya kuegemea upande wa Naibu wa Rais Ruto.

“Iwapo ningekuwa na hatia, korti haingeniachilia huru. Mimi si mhalifu, na kamwe sijawahi kushiriki kisa chochote cha uhalifu. Hii ni vita ya kisiasa kwa sababu ninaunga azma ya Dkt William Ruto kuingia Ikulu 2022,” akasema mbunge huyo mapema wiki hii baada ya kuachiliwa huru na mahakama ya Murang’a.

Bw Ndindi alitiwa nguvuni na maafisa wa polisi kwa kudaiwa kusambaratisha mchango wa kanisa moja la Kikatoliki Murang’a uliohudhuriwa na mbunge maalum Maina Kamanda na ambaye ni mfuasi wa Kieleweke.

Seneta Sakaja anasema kujiri kwa Tangatanga na Kieleweke ni suala ambalo hakutarajia lingeibuka ndani ya Jubilee. Anasema changamoto zilizoko ndani ya JP zitatatuliwa na Rais Kenyatta na Naibu wake Dkt Ruto, ambao ndio viongozi wakuu.