Makala

SANAA YA KUPODOA: Alitanga na njia akitafuta ajira, wateja wanamtafuta wenyewe

September 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

“YEYOTE anayejua bingwa wa kupodoa mjini Nakuru?” lilisoma chapisho kwenye mtandao ya kijamii wa Facebook na baada ya dakika chache jina ‘Angie Boke’ likawa linatolewa kama jibu kwa aliyetafuta huduma.

Alipohitimu na akatuzwa shahada yake katika somo la Rasilimaliwatu kutoka Chuo Kikuu cha Moi, Agnes Nyaboke, 28, ambaye anajiita ‘Angie Boke’, hakujua hatima gani ilimsubiri.

Aliomba kazi kwa kila kampuni inayojulikana bila bahati. Ni wakati alitamani sana ajira ya aina yoyote kumtafutia mwanawe riziki na hela za kukidhi mahitaji yake.

“Nilikwenda katika kila ofisi kutafuta kazi lakini hakuna mtu aliyeniajiri. Nilitamani kuwa na pesa za kunisaidia kumlinda mtoto wangu,” anasema.

Ilitokea siku moja ameenda studio kupiga picha ya mtoto alipotambua kuwa mpigapicha hakuwa na msaidizi na akamwomba kazi kama karani wa mapokezi.

“Nilifurahi aliponiajiri ingawa alikuwa akinilipa Sh6,000,” anasema akifafanua alikubali kiasi hicho kuliko kukaa bure.

Alipokuwa akifanya kazi huko, aligundua kuwa watu wengi waliokwenda pale kupiga picha walikuwa wakiulizia msanii wa upodozi lakini kwa sababu hakukuwa na yeyote wakati huo, walielekezwa kwingineko.

Agnes anasema aliona fursa ya kazi na alianza kujifunza sanaa ya kuwapodoa na kuwapamba wateja. Alifuatilia YouTube na kufanya majaribio kwa marafiki zake.

“Hiyo ilikuwa fursa kwangu kufanya sanaa ya upodozi ambayo inahitaji ubunifu. Mitandao ya YouTube na Google ikawa mwalimu wangu,” anasema.

Alitumia Sh3,000 kununua vipodozi vya kuanzia biashara yake.

“Sikuogopa kujaribu. Nilipopata ujasiri wa kutosha, nilimpeleka mteja wangu wa kwanza kwenye studio na matokeo yalikuwa ya kuridhisha na ndivyo nilivyokuza idadi ya wateja wangu,” anaongeza.

Baadaye, alianza kupata wateja wengi hasa baada ya huyu kesho kumwelekeza yule kwa Angie na kadhalika. Walioleta wateja wapya akawa anawafanyia nafuu.

Mpodoaji Agnes Nyaboke ‘Angie Boke’ akiwa na mteja wake. Picha/ Margaret Maina

Kulingana na Agnes, unaweza kuanza biashara yako bila kutarajia.

Anaamini ikiwa hakwenda studioni kupiga picha, huenda pengine angekuwa anajitahidi kutafuta ajira.

Amekuwa akijiuza kupitia majukwaa ya mitandao ya kijamii; kwenye Instagram @ taiboke254 na Facebook angiezmakeup.

Agnes pia hufanya sanaa ya athari maalum za upodoaji kuonyesha hali au hisia fulani kwa mteja.

“Hakuna kinachokuja kwa urahisi na wakati mwingine lazima upanue mawazo na mtazamo,” anasema.

Sasa analipisha kati ya Sh1000-Sh3000 kwa mteja kulingana na hafla kutoka Sh300 za awali, ingawa amekuwa na changamoto kama za kujaribu kuwashawishi wateja wake kulipa kiasi hicho kwani watu wengi hawaelewi kwa nini viwango vya juu wakisema anatumia tu bidhaa asili.

“Wakati mwingine nina wateja zaidi ya watano na wakati narembesha biarusi au kukiwa na karamu za siku ya kuzaliwa, nina wateja wengi; kama 15 kwa siku, ” anaongeza.

Mwanzoni mwa 2018 aliingizwa kwenye programu iitwayo ‘Ongoza Youth’ ambapo alijifunza jinsi ya kupangia pesa zake matumizi mazuri na aliweka akiba ya kuanzisha biashara yake mwenyewe.

Aliweka faida yake na mnamo Agosti 2018, akiwa na Sh150,000 alifungua Taiboke Beauty Parlor katika mji wa Nakuru ambapo wateja hufika kurembeshwa na kupodolewa uso, kutengenezwa kucha za mikono na miguu. Agnes amawaajiri wafanyikazi wanne wanaomsaidia kazi.

Agnes ana mpango wa kupanua biashara kwa sababu wateja wake wameongezeka sana.