Makala

SANDRA TENAI: Alenga kuwa mwigizaji na mwanahabari mtajika

August 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA JOHN KIMWERE

KILA mja hujipa matumaini ambapo huwa ni hali ya kutarajia. Ni katika hali ya kutumainia na kuvumilia ambapo anaaminia nyota yake itang’aa na kutinga upeo wa mwigizaji wa kimataifa miaka ijayo.

Ingawa ndio anaanza kupiga ngoma anasema anapania kutwaa tuzo ya kimataifa katika masuala ya maigizo ndani ya miaka mitano ijayo.

Sandra Jepchumba Tenai maarufu Mama Taby anadokeza kuwa ingawa hajapata mashiko katika tasnia ya maigizo anaamini ipo siku kazi yake itakubalika kote duniani.

”Bila kujisifia ninaamini nitafanya vizuri katika maigizo wala sina shaka kabisa ingawa kwa sasa nimezamia zaidi masuala ya shule,” anasema na kuongeza analenga kufikia kiwango cha mwigizaji wa kimataifa, Mercy Johnson ambaye huigiza filamu za Kinigeria (Nollywood).

MWANA HABARI

Dada huyu anasema anaamini hivi karibuni atafanya filamu na kupata mpenyo kupeperushwa kwenye runinga. Binti huyu aliyetamani kuhitimu kuwa mwana habari tangia akiwa mdogo kwa sasa ni mwanafuni wa mwaka wa nne anakosomea kuhitimu kwa shahada ya diploma kama mwana habari wa runinga. Anasomea katika Chuo Kikuu cha East Africa Institute of Certified Studies.

BITTER SMILE

”Ninajivunia kufanya kazi na Peacepalm Production na Jicho Four Production ambapo nimeshiriki filamu kadhaa,” alisema na kuongeza kwamba analenga kutumia maigizo kufunza vijana madhara ya ndoa za mapema pia matumizi ya dawa za kulevya. Anajivunia kushiriki filamu kama ‘Bitter Smile,’ na ‘Antonina,’ kati ya zingine.

Ingawa alivutiwa zaidi na uigizaji mwaka 2014 anasema alianza kujituma katika masuala ya maigizo akiwa na umri wa miaka saba kipindi hicho akisoma shule ya Msingi.

”Mwaka 2014 nilipata motisha zaidi kushiriki uigizaji baada ya kutazama kipindi cha Real Househelps of Kawangware nilipokuwa kinapepeushwa kupitia runinga ya KTN,” akasema.

Kwa kuzingatia kila mmoja hupenda kujifunza na wenzie kwa wasanii wa humu nchini kisura huyu anasema angependaa kufanya kazi na Celestine Gichuki ‘Selina,’ pia Sandra Datcha ‘Real Househelps of Kawangware.’

Kwa wanamaigizo wanaotamba kimataifa anatamani sana kushirikiana nao Lupita Nyong’o anayevunia kushiriki filamu kama ’12 Years a slave,’ pia ‘Black Panther.’ Pia Mercy Johnson wa Nigeria aliyeshiriki ‘Heart of a fighter’ na ‘Dumebi the dirty girl.’

MAHUSIANO

Kipusa huyu anashauri wenzie wajipe moyo wala wasivunjike moyo bali wasiweke katika kaburi la sahau kujituma bila kulegeza kamba na waamini ipo siku matamanio yao yatatimia. Anasema ingawa mwanzoni wazazi wake walikuwa wanapiga hatua yake kujiunga na uigizaji hatimaye wamekubali.

Katika mpango mzima anadokeza kuwa nyakati zingine maprodusa humnyima nafasi kwa kuwapendelea marafiki zao. ”Sio mara moja baadhi ya maprodusa wameniomba tuwe na mahusiano ya kimapenzi ili wanipe nafasi ya kuigiza,” akasema na kutoa mwito kwa viongozi sampuli hiyo waache kushusha wanawake.