• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 5:45 AM
SEKTA YA ELIMU: Kanuni na sheria za usalama shuleni zipo, shida ni mapuuza

SEKTA YA ELIMU: Kanuni na sheria za usalama shuleni zipo, shida ni mapuuza

Na CHARLES WASONGA

NI wazi kuwa watoto hukabiliwa na aina mbalimbali ya hatari katika taasisi za elimu, hususan, shule za msingi na za upili nchini ilhali hakuna hatua za maana huchukuliwa kudhibiti hali hiyo.

Kisa cha Jumatatu cha kuporomoka kwa darasa katika Shule ya Msingi ya Precious Talents Top School iliyoko Dagoretti, Kaunti ya Nairobi ni moja kati ya visa vingi ambavyo hushuhudiwa kila leo maeneo kadhaa; mijini na mashambani.

Watoto pia hukabiliwa na hatari ya kuathiriwa na maradhi kama kipindupindu, haswa katika shule za mabweni, kujeruhiwa katika ajali za mabasi ya shule, kudhulumiwa kimapenzi na walimu na wafanyakazi wa shule, paa za madarasa yao kung’olewa kwa upepo kati ya aina nyingine za hatari.

Swali ni je, wahusika wamechukua hatua zipi kuzuia hatari kama hizi?

Itakumbukwa kuwa baada ya mkasa wa moto uliotokea katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi, Nairobi, ambapo wasichana wanane walifariki mwaka 2018, aliyekuwa Waziri wa Elimu Amina Mohamed aliahidi kuwa serikali ingechukua hatua zifaazo kuhakikisha kuna usalama katika taasisi za masomo.

Huku akisisitiza kuwa usalama wa wanafunzi ni suala linalopasa kuzingatiwa wakati wa ujenzi wa miundomsingi shuleni, Bi Mohamed aliagiza kwamba ujenzi wa majengo yote mapya shuleni uzingatie muundo bora utakaotoa mandhari faafu kwa wanafunzi kusoma.

Kuporomoka kwa darasa la Shule ya Msingi ya Precious Talents kunamaanisha kuwa agizo la Waziri Mohamed halikuzingatiwa na maafisa wa Wizara ya Elimu wakati huo na hata sasa ambapo wizara hiyo inasimamiwa na Profesa George Magoha.

Kimsingi, usalama wa wanafunzi ni hitaji muhimu katika mchakato mzima wa kufanikishwa kwa azma ya elimu bora kwa watoto wote.

Kwa hivyo, walimu, wasimamizi wa shule na wizara ya elimu katika ngazi za serikali na zile za kaunti zinapasa kuhakikikisha kuwa madarasa, vyoo, mabweni, mabwalo (dinning halls) na miundomsingi mingineyo imejengwa kwa kuzingatia kanuni zilizoidhinishwa na asasi husika za serikali.

Japo, wizara za elimu katika serikali za kaunti na Serikali Kuu kwa ushirikiano na idara za ujenzi, zinapasa kuhakikisha hilo linazingatiwa, maafisa husika wamezembea kazini.

Hali hii imechangia wajasiriamali wanaoanzisha shule za kibinafsi, hasa katika mitaa ya mabanda, kuendelea kujenga majengo mabovu ambayo ni hatari kwa usalama wa wanafunzi.

Ikumbukwe kwamba baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 ambapo shule kadha, katika maeneo yaliyoathiriwa, zilibomolewa na shughuli za masomo kutatizika, Wizara ya Elimu ilitayarisha mwongozo kuhusu utaratibu unaopasa kutumiwa kuhakikisha uwepo wa usalama katika shule zote za umma nchini.

Mwongozo huo unaelezea, kwa undani, kuhusu vigezo vinavyopasa kuzingatiwa wakati wa ujenzi wa madarasa, mabweni na miundomsingi shuleni na wajibu wa walimu, wasimamizi wa shule na bodi za wasimamizi katika kuhakikisha kwamba wanafunzi wanasoma katika mazingira salama.

Lakini kwa mara nyingine, uchunguzi umebaini kuwa yaliyomo kwenye mwongozo huo yamepuuzwa, haswa na wamiliki wa shule za kibinafsi, hususan katika kaunti ya Nairobi yenye uhaba mkubwa wa shule za umma.

Hakuna hatua yoyote ambayo imechukuliwa dhidi ya watu kama hao, ambao huongozwa na uchu wa kuchuma faida wala si haja ya kuwawezesha watoto kupata elimu.

Mkasa kama vile ule wa Shule ya Msingi ya Precious Talents unaweza kuzuiwa au athari kupunguzwa ikiwa sheria na kanuni zilizowekwa zingezingatiwa katika ujenzi wa miundomsingi shuleni. Ni wajibu wa maafisa wa serikali husika, wadau katika sekta ya elimu na wananchi kwa jumla kuhakikisha kwamba kanuni hizi za usalama zinazingatiwa.

You can share this post!

Familia 45 nje baridini baada ya moto kuteketeza nyumba zao...

Kenya iko tayari kwa uwekezaji wa Amerika, Rais Kenyatta...

adminleo