SEKTA YA ELIMU: Kufungwa kwa vyuo vikuu 32 ni hatua faridi ya kuleta mageuzi ya elimu vyuoni
Na CHARLES WASONGA
HATIMAYE serikali imepambazukiwa na ukweli kwamba ilikosea pakubwa kwa kuanzisha vyuo vikuu vingi pasina kuweka mipango ya kudumu ya kuvifadhili wala kuviwezesha kuzalisha mapato kivyao.
Hii ndio maana akiwasilisha bajeti bungeni wiki jana Waziri wa Fedha Henry Rotich alitangaza kuwa serikali itaviunganisha vyuo vikuu 32 vya umma na kufungwa mabewa kadhaa.
“Tutatekeleza mageuzi katika sekta ya vyuo vikuu kwa kuchunguza usimamizi wa kifedha katika vyuo vikuu, miradi inayoendelezwa kwa lengo la kuipanga upya. Pia tutatekeleza mipango itakayopelekea kuunganisha kwa vyuo vikuu ambavyo haviwezi kujisimamia kufuatia kupungua kwa wanafunzi. Mabewa kadhaa pia yatafungwa chini ya mpango huo,” akasema Bw Rotich.
Hatua hii inafaa ikizingatiwa kuwa vingi vya vyuo vikuu vya umma vinakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile ukosefu wa fedha, mahadhiri waliohitimu na miundo mbinu na vifaa vya mafunzo.
Hali hii inachangiwa na kupungua kwa ufadhili kutoka kwa serikali kuu na kupungua kwa idadi ya wanafunzi baada ya kuimarishwa kwa usimamizi wa mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE). Mikakati iliyowekwa kuanzia mwaka wa 2016 ilipunguza visa vya udanganyifu na hatimaye wanafunzi waliopata alama za C+ kwenda juu.
Wakati huu kuna takriban vyuo vikuu 73 nchini, idadi kubwa ya vyuo hivyo ikiwa ni vile vilivyoanzishwa kuanzia mwaka wa 2,000, kimsingi, kutokana na sababu za kisiasa wala sio haja ya kuzalisha nguvu kazi bora faafu kwa ustawi wa nchi.
Ajabu ni kwamba baadhi ya vyuo hivyo vinafundisha kozi ambazo haziambatani na mahitaji ya soko la ajira au malengo ya maendeleo ya serikali, licha ya kufadhiliwa kutokana na pesa za umma.
Hii ndio maana juzi Waziri wa Elimu George Magoha aliamuru Tume ya Kusimamia Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) kufutilia mbali zaidi ya kozi 133 “zisizo na manufaa” zifutiliwe mbali.
Kutokana na changamoto za kifedha zinazozikumba vyuo vikuu hivi mapema mwaka huu manaibu chansela wa vyuo vikuu vya umma waliitaka serikali kuongeza karo inayotozwa wanafunzi wanaofadhiliwa na serikali.
Pendekezo
Baraza la Manaibu Chansela lilipendekeza wanafunzi hao wawe wakilipa karo ya mafunzo ya Sh48,000 kila mwaka badala ya Sh16,000 wanazolipa sasa, pendekezo ambalo lilipingwa vikali na wanafunzi.
Hii ni kwa sababu tangu 2016 idadi ya wanafunzi wanaojifadhili wenyewe (self sponsored) imepungua kwa kiwango kikubwa baada ya idadi ya wanafunzi wanaopata alama ya C+ kwenda juu kupungua. Awali, vyuo vikuu vya umma vilikuwa vikivuna hela nyingi kutokana kwa tapo hili la wanafunzi.
Majuzi Katibu Mkuu wa Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu (UASU) Constantine Wasonga aliiambia Kamati ya Bunge kuhusu Elimu h kwamba vyuo hivyo vinakabiliwa na changamoto ya kifedha kiasi cha kushindwa kuwasilisha michango ya wahadhiri kwa hazina ya Bima ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF) na ya pensheni (NSSF).
Isitoshe, aliiambia wanachama wa kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Tinderet Julius Melly kuwa kuwa kufikia Aprili mwaka huu vyuo hivyo havikuwa vimewasilisha jumla ya Sh481.3 milioni kwa mashirika ya akiba na mikopo ya (Saccos) hali ambayo imeathiri uwezo wa wahadhiri kupata mikopo ya kujiendeleza.
Ingawa hatua ya serikali kuunganisha vyuo vikuu itapelekea jumla ya wafanyakazi 27,000 wakiwemo wahadhiri takriban 9,000 ni mwanzo wa mageuzi ambayo yatarejesha hadhi ya vyuo hivyo.