SEKTA YA ELIMU: Serikali ichukue hatua madhubuti kuhusu suala la usalama shuleni
Na CHARLES WASONGA
RIPOTI iliyoandaliwa kwa udhamini wa Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (Kuppet) imethibitisha kuwa shule nyingi nchini ni hatari kwa maisha ya watoto na hatua zapaswa kuchukuliwa kukabiliana na hali hiyo.
Mamia ya watoto hufariki kila mwaka katika mikasa kama vile ajali ya mabasi, mioto inayoteketeza mabweni, kuangukiwa na majengo mabovu na kudhuluma wazotendewa na walimu, wafanyakazi shuleni na hata wanafunzi wenzao.
Ripoti hiyo imejiri baada ya mkasa wa kuporomoka kwa darasa la Shule ya Msingi ya Precious Talent Acadeny, Dagoreti,Nairobi mnamo Septemba mwaka huu ambapo wanafunzi wanane walifariki na wengine 60 wakajeruhiwa.
Pia itakumbukwa kuwa mnamo, 2017 wasichana 10 walifariki katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi baada ya moto kuzuka katika bweni la usiku wa manane.
Na katika mwaka uo huo, zaidi ya shule 100 ziliripoti visa vya mabweni kuteketea ambapo mali ya thamani ya mamilioni ya fedha iliharibika.
Baada ya darasa kuporomoka, Dagoreti, Waziri wa Elimu Profesa George Magoha alitoa amri kwamba majengo yote ya shule yakaguliwe kubaini ikiwa yametimiza viwango hitajika vya usalama. Hatimaye zaidi ya shule 200, nyingi zao za kibinafisi, zilifungwa kote nchini.
Kinaya ni kwamba maafisa waliozembea kazini, ndipo maafa kama haya yakatokea, hawajachukuliwa hatua zozote kufukia sasa.
Kufungwa kwa shule hizo kuliathiri maelfu ya wanafunzi, walimu na wazazi, pamoja na mamia ya watahiniwa wa mitihani ya kitaifa.
Ni kufuatia mkasa huo ambapo chama cha Kuppet kilianzisha uchunguzi katika shule 213 na matokeo yakathibitisha yale ambayo yamekuwa yaliangaziwa katika vyombo vya habari kwamba: Shule nyingi sio salama kwa wanafunzi.
Shule hizo zinapatikana katika kaunti 21, ambazo ni; Meru, Vihiga, Taita Taveta, Isiolo, Tharaka Nithi, Makueni, Nyandarua, Nyeri, Kirinyaga, Muranga, Samburu, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Laikipia, Kericho, Busia, Siaya, Homabay, Migori, Nairobi na Embu. Kati ya shule hizo, 153 ni za upili, 46 ni za msingi, 12 ni shule za chekechea na mmoja ni chuo cha kadri.
Akitoa matokeo ya uchunguzi huo wiki jana, mtaalam wa masuala ya elimu kutoka Shirika la Ushauri la Tathmini Consulting Jonathan Wesaya Maina, alisema ni asilimia 39 pekee za shule zote zilikaguliwa zimekuwa zikitekeleza mwongozo kuhusu usalama shuleni uliotolewa na Wizara ya Elimu, mwaka wa 2010.
Na asilimia 67 ya shule zilisema hazina bajeti ya kutosha ya usalama, asilimia 28 za shule hazikuwa na mgao wowote fedha za kushughulikia usalama na ni asilimia tatu pekee za shule zilibainika kuwa na mgao tosha wa bajeti wa kufadhili shughuli za usalama shuleni.
Wakati huo huo, asilimia 97 ya shule za upili zilisema fedha ambazo zilipokea hazikutosha kukidhi mahitaji ya idadi kubwa ya wanafunzi katika taasisi hizo baada ya serikali kuanza kutekeleza sera ya kuhakikisha wanafunzi wote waliofanya mtihani wa darasa la nane wanajiunga na shule za upili (maarufu kama 100 per cent transition policy). Na baadhi ya shule hazikuwa na vyoo salama.
“Ipo haja kwa idara ya kusimamia ubora (Quality Assurance and Standard) kupewa rasilimali zaidi ili iweze kuendeleza ukaguzi shuleni kuhakikisha kuna usalama. Shule pia zinapasa kutengewa fedha zaidi za kufadhili ukarabati wa majengo na miundo msingi mingine muhimu katika taasisi hizo,” Maina anapendekeza.
Vile vile, anapendekeza kuwa wanafunzi, walimu na wafanyakazi wa shule wapewe mafunzo kuhusu mbinu za kukabiliana na mikasa na moto na majanga mbalimbali.
“Ama kwa hakika mbinu ya kukabiliana na Usimamizi wa Majanga unapasa kufunzwa kama somo mahsusi shuleni ili wanafunzi wafahamu athari ambazo zinaweza kusababisha na matukio kama hayo,” anaongeza.