SEKTA YA ELIMU: Serikali isifanye masihara na usalama wa wanafunzi shuleni
Na CHARLES WASONGA
VIFO vya wanafunzi 14 katika Shule ya Msingi ya Kakamega Jumanne wiki iliyopita kwa mara nyingine ni ithibati kuwa wahusika hawajachukua hatua hitaji kuimarisha usalama wa wanafunzi katika taasisi za elimu nchini.
Wengine kadhaa pia waliangamia wakati wakipata matibabu.
Ni bayana kuwa maafisa wa elimu, walimu, wazazi na wadau wengine hawajatekeleza kanuni za usalama katika taasisi za masomo zilizoorodheshwa katika Hati ya Mwongozo kuhusu Usalama Shuleni.
Hati hiyo iliyozinduliwa mnamo 2009 na aliyekuwa Waziri wa Elimu Prof Sam Ongeri, kati ya mambo mwengine, imependekeza jinsi madarasa na mabweni yanapasa kujengwa ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi. Vile vile, imeorodhesha wajibu wa wasimamizi wa shule, walimu, wanafunzi wenyewe, bodi za usimamizi na jamii zinazopakana na shule katika kuhakikisha usalama wa wanafunzi.
Kisa cha Kakamega ambacho kimetokea miezi michache baada ya mkasa wa kuporomoka kwa darasa la Shule ya Msingi ya Precious Talent Academy, Dagoreti, Nairobi, kinaonyesha kuwa mikakati ya usalama iliyoorodheshwa katika mwongozo huu haikuzingatiwa.
Kwa mfano, wasimamizi wa shule hiyo yenye wanafunzi wengi, na majengo ya orofa, hawakuhakikisha maeneo maalum ya watoto kutorokea salama panapotokea hatari yoyote ile.
Kwamba watoto hao walifariki na wengine 47 wakajeruhiwa baada ya kukanyagana wenyewe kwa wenyewe wakiondoka madarasani kunaonyesha wazi kuwa usamamizi wa shule haujaweka miundo mbinu faafu ya kuzuia matukio kama hayo.
Itakumbukwa kwamba baada ya mkasa wa Shule ya Msingi ya Precious Talent ambapo wanafunzi wanane walifariki na wengine 60 wakajeruhiwa Waziri wa Elimu Profesa George Magoha alitoa amri kwamba majengo yote ya shule yakaguliwe kubaini ikiwa yametimiza viwango hitajika vya usalama.
Hatimaye zaidi ya shule 200, nyingi zao za kibinafisi, zilifungwa kote nchini baada ya kubainika kuwa majengo yao hayakuwa salama. Lakini kinachoibua maswali ni kwamba hadi wakati huu Waziri Magoha hatoa ripoti kuhusu tathmini ya usalama wa shule nchini.
Ripoti kama hiyo ingewawezesha wadau kuibua mbinu na mikakati mipya ya kuimarisha usalama wa wanafunzi katika taasisi za elimu nchini. Hapa, Wizara ya elimu imeonekana kuzembea katika wajibu wake.
Vile vile, itakumbukwa kuwa baada ya mkasa wa moto uliotokea katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi, Nairobi, ambapo wasichana wanane walifariki mwaka wa 2018, aliyekuwa waziri wa Elimu Amina Mohamed aliahidi kuwa serikali ingechukua hatua zifaazo kuhakikisha kuna usalama katika taasisi za masomo.
Huku akisisitiza kuwa usalama wa wanafunzi ni suala linalopasa kuzingatiwa wakati wa ujenzi wa miundomsingi shuleni, Bi Mohamed aliagiza kwamba ujenzi wa majengo yote mapya shuleni yazingatie muundo bora utakaotoa mandhari faafu kwa wanafunzi kusoma.
Vifo vya wanafunzi ambavyo vimetokea katika shule mbalimbali nchini baadaye vinamaanisha kuwa agizo la Waziri Mohamed halikuzingatiwa na maafisa wa Wizara ya Elimu wakati huo na hata sasa ambapo wizara hiyo inasimamiwa na Profesa Magoha.
Kimsingi, usalama wa wanafunzi ni hitaji muhimu katika mchakato mzima wa kufanikishwa kwa azma ya elimu bora kwa watoto wote. Mazingira salama, hasa ni muhimu kwa wanafunzi wa madarasa ya chini kutokana na umri wao mdogo.
Kwa hivyo, walimu, wasimamizi wa shule na wizara ya elimu katika ngazi za serikali na zile za kaunti zinapasa kuhakikikisha kuwa madarasa, vyoo, mabweni, bwalo (dinning hall) na miundomsingi nyinginezo zimejengwa kwa kuzingatia kanuni zilizoidhinishwa na asasi husika za serikali.