SEKTA YA ELIMU: TVET vyaweza kufaulishwa kwa rasilimali tosha na uhamasishaji
Na CHARLES WASONGA
VYUO vya Kiufundi (TVET) vinaendelea kuandikisha idadi ndogo ya wanafunzi, kulingana na matokeo ya tafiti zilizofanywa majuzi.
Hii ni licha ya kwamba serikali imekuwa ikiwahimiza wanafunzi ambao hawakupata alama za kuwawezesha kujiunga na vyuo vikuu kujiunga na vyuo vya kadri haswa TVET.
Kulingana na tafiti hizo nne hali hiyo inashuhudiwa zaidi miongoni mwa wanafunzi kutoka jamii masikini na maeneo yaliyoachwa nyuma kimeandeleo hapo zamani. Maeneo hayo ni kama vile kaunti za Turkana, Garissa, Mandera, Wajir na Pokot Magharibi.
Mashirika yaliyodhamini tafiti hizo ni; Wakfu wa Zizi Afrique, “Dalberg International”, “African Population and Health Research Centre” na “East Africa Institute of the Aga Khan University” .
Kimsingi, mashirika haya yalilenga kubaini uwepo wa ujuzi na maarifa ambayo vijana wanapaswa kuwa nayo ili waweze kuajiri, kujiajiri au kudumisha ajira wanazoshikilia sasa ili kuchangia ustawi wa kijamii.
Watafiti walizuru vyuo anuwai vya kitaifa, vyuo vya kiufundi katika maeneo ya miji na vile vilivyoko vijijini.
“Ilibainika kuwa idadi kubwa ya vijana kutoka kaunti zilizoko katika maeneo kame nchini hukosa nafasi ya kujiunga katika vyuo kiufundi. Na wengi wao ni wanafunzi wa kike ambao huingizwa kusumba potovu kwamba kozi za kiufundi ni za wavulana pekee,” anasema Ahmed Barow aliendesha utafiti kwa niaba ya taasisi ya East African Institute of Aga Khan katika kaunti kadha za eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya.
Aidha, mtaalamu huyu pia aligundua kuwa vyuo vichache vya kiufundi vinavyopatikana eneo zima la kaskazini mashariki mwa Kenya havina vifaa na wakufunzi wa kutosha, hali inayodumaza viwango vya mafunzo katika taasisi hizo.
Wiki jana, Waziri wa Elimu Profesa George Magoha alionekana kukubaliana na matokeo ya tafiti hizi, aliposikitikia idadi ndogo ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya TVET licha ya kwamba “kuna uhaba mkubwa wa mafundi nchini”.
Akihutubu katika kongamano kuhusu tathimini ya utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu unaohimiza umilisi na utendaji (CBC) Waziri huyo alisema kuwa mwaka jana, jumla ya vyuo 1,000 vya kiufundi nchini vilisajili wanafunzi 275,000 pekee huku vyuo vikuu ambavyo ni idadi yavyo ni chini ya 40 vilisajili zaidi ya wanafunzi 562,000.
“Inaonekana kuwa idadi kubwa ya wanafunzi bado wanang’ang’ania kujiunga na vyuo vikuu kusomea kozi ambazo baadhi yazo haziambatani na hitaji la soko la ajira nchini. Wazazi wanafaa kuwashauri watoto wao kwamba kozi za kiufundi ndizo zinaingilia na ajenga za maendeleo nchini,” akasema.
Aidha, Rais Uhuru Kenyatta aliwashauri wazazi kukoma kuweka shinikizo kali kwa watoto wao kwamba sharti wajiunge na vyuo vikuu badala akiwataka kuwaelekeza kusomea kozi za kiufundi.
Tafiti zilizodhamini na mashirika manne yaliyotajwa hapa pia zilibaini kuwa kuna idadi ndogo ya wanafunzi wa kike katika vyuo anuai vya kitaifa huku wengine wao wakisomea kozi “nyepesi” kama ususi, ukarani, upishi na ufundi wa nguo.
Itakumbukwa kwamba ripoti ya Tume ya Kitaifa kuhusu Jinsia na Usawa (NGEC) iliyotolewa mnamo 2016 ilitambua vijana kama miongoni mwa makundi yenye mahitaji maalum lakini yametengwa katika nyanja mbalimbali.
Kulingana na ripoti licha ya serikali kuendeleza sera ya elimu bila malipo katika shule za msingi na iliyopunguzwa gharama katika shule za upili, vijana wengi bado hukosa nafasi ya kupata mafunzi ya kuwawezesha kujitemea maishani. Hali hii imepelekea wengi wao kukosa ajira na hivyo kuwa na uwakilishi finyu katika asasi za kisiasa na kiutawala.
Lakini wadadisi wamemkosoa Waziri Magoha na Rais Kenyatta wakisema ni wao wamefeli kutenga rasilimali tosha za kupiga jeki sekta ya TVET.