Makala

SEKTA YA SUKARI: Ripoti ya kufufua sekta ya sukari yatoa tumaini jipya kwa wadau

February 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na AG OWINO

MAPENDEKEZO ya mageuzi katika sekta ya sukari ambayo yamekuwa yakisukumwa na Tume ya Kubinafsisha Mashirika ya Serikali almaarufu Privatisation Commission yamekuwa donda sugu kwa wakuzaji miwa.

Tume hii ilikuwa ikikusanya maoni ya wadau katika maeneo ya ukuzaji miwa tangu 2016.

Mara nyingi wanasiasa walichochea wadau kila iliporatibiwa kwamba tume hii ingechukua maoni ya wakulima kuhusu kuboresha kampuni haswa za serikali za Nzoia, Chemelil, Muhoroni, SoNy na Miwani.

Mtu yeyote ambaye alionekana kuuliza maswali kuhusu jinsi walivyopanga kubinafsisha kampuni hizi alikemewa vikali.

Hivyo basi, wakati Rais Uhuru Kenyatta alipoteua Jopokazi la Sukari, alibadili mwelekeo kwani walioteuliwa walikuwa wale walio na uhusiano wa karibu na sekta ya sukari.

Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, ambaye alikuwa mwenyekiti wa tume hii ni mzaliwa wa Kakamega, eneo la ukuzaji miwa. Wengine kama Nabii Nabwera ni mkazi wa Bungoma na mtoto wa Mheshimiwa Burudi Nabwera ambaye kwa wakati mmoja alikuwa mwenyekiti wa kampuni ya Sukari ya Nzoia.

Daktari Jenrose Omondi ni mkazi wa Siaya na ni afisa katika Tume ya Ubinafsishaji. Bw Okoth Obado ni gavana wa Migori na wakati mmoja alikuwa mwakilishi wa wakulima wa miwa ambaye ana ushawishi mkubwa miongoni mwa wakulima na wakazi wa Migori. Naye Dkt Otuoma ni mkazi wa Busia, eneo la miwa ambalo lina kampuni mbili za sukari.

Kamati hiyo ya watu 21 ilikuwa pia na magavana wengine kutoka kaunti za Bungoma, Nandi na Kisumu.

Kulipwa kwa mishahara

Habari njema kwa wakulima wa miwa na wafanyakazi wa sukari ni kwamba ripoti hii iliyopokezwa Rais Jumatatu, inapendekeza kuwekezwa kwa fedha na serikali ili waweze kulipwa haraka iwezekanavyo.

Mwaka jana, serikali ilitoa pesa za wakulima na kusahau wafanyakazi. Hadi sasa, kampuni zinazomilikiwa na serikali hazijalipa wafanyakazi kwa baina ya mwaka mmoja na miwili.

Mara ya mwisho serikali kutuma pesa kugharimia mahitaji katika kampuni hizi ilikuwa mwaka wa 2017.

Kulingana na ripoti hii, kufikia mwezi wa Juni mwaka wa 2018, Kampuni ya Sony ilikuwa na deni la Sh506 milioni la wafanyakazi, Nzoia Sh330 milioni, Chemelil Sh486 milioni na Mumias Sh1.24 bilioni.

Kampuni ya Mumias, hata hivyo, kwa sasa, iko chini ya mrasimu wa benki ya KCB.

Nzoia hata hivyo imejitahidi na sasa inapanga kuwalipa wafanyakazi wao nusu ya mshara mwezi ujao.

Mbinu za kimataifa

Inaonekena Jopo hili pia liliiga mbinu zinazotumiwa katika nchi zenye umahiri katika ukuzaji wa miwa katika kutoa mapendekezo yao. Kwa mfano, katika nchi ya Mauritius, India na Brazil miwa hukuzwa kwa kutumia unyunyiziaji maji na wakulima hawategemei mvua.

Ripoti hii inapendekeza kujengwa kwa mabwawa ili kuhakikisha miwa inapata maji ya kutosha. Ingawa mvua haijakuwa tatizo kwa sekta ya miwa nchini kwa miaka 10 iliyopita, huwa hainyeshi kama inavyotakikana.

Tumeshuhudia mvua ikinyesha kwa wingi kwa wakati mmoja kisha kufuatiwa na kipindi kirefu cha kiangazi. Miwa hata hivyo huhitaji mvua katika miezi ya kwanza na baadaye kuhitaji mvua kiasi tu inapokaribia kuvunwa.

Unyunyiziaji maji huwezesha miwa kupata maji sawa na mahitaji yake. Pengine huu utakuwa wakati mzuri kufuatilia wadau kutoka Misri ambao wakati mmoja waliandamana na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa kutathmini uwezekezano wa kujengwa kwa bwawa la maji kwa kilimo katika Kaunti ya Bungoma.

Kanda za ukuzaji miwa

Pia imependekezwa kurudishwa kwa kanda za ukuzaji miwa ambazo ziliondolewa na aliyekuwa na Waziri wa Kilimo kwa wakati mmoja Willy Bett lakini kwa mtindo tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Kanda za ukuzaji miwa zimekuwa zikipingwa vikali na kampuni za kibinafsi ambazo zimekuwa zikidai kwamba kampuni za

serikali hudhulumu wakulima kwa kuchelewa kuvuna miwa yao pamoja na malipo.

Ili pengine kutoonekana kuegemea upande wowote, pia hapa waliiga mfano katika nchi zilizoendelea. Badala ya kurudisha kanda kama ilivyokuwa zamani, wamegawa maeneo ya ukuzaji kwenye vikundi. Kwa mfano, Eneo la Kati hujumuisha kaunti za Kisumu, Nandi Kusini, Nandi na Kericho. Kampuni za Kibos, Chemelil, Miwani, Soin, Muhoroni zitakuwa hapa.

Kampuni ambazo zimekuwa zikizonania miwa kama Nzoia, West Kenya na Butali zimewekwa kwenye Eneo la Upper Western.

Kampuni nyingine kama Mumias, Busia, Siaya na Ole-Pito zimewekwa kwenye ukanda wa Lower Western.

Kampuni za Trans-Mara, Sori, Sukari (ambayo inamilikiwa na Rai) zimewekwa kwenye eneo la Kusini.

Eneo la Pwani nalo litajumuisha kaunti za Kwale, Tana River, Kilifi na Lamu. Kwale Sugar ndiyo inafanya kazi ya sasa katika eneo hili.

Habari njema

Habari njema kwa mkulima ni kwamba atakuwa huru kusaini mkataba na kampuni yoyote katika eneo alilowekwa. Iwapo kampuni aliyosaini mkataba nayo itakosa kuvuna miwa kwa wakati unaofaa ama kuchelewa kulipa baada ya siku saba,

atakuwa huru kuuzia kampuni nyingine miwa yake. Kwa mfano, iwapo kampuni ya West Kenya itachelewesha malipo ya mkulima ambaye amempa mkataba, atakuwa huru kuuzia miwa kampuni ya Nzoia au Butali lakini hawezi kuuzia Transmara ama Kibos kwa sababu ziko katika maeneo tofauti.

Miwa michanga

Uvunaji wa miwa ambayo haijakomaa sasa itakuwa hatia. Yeyote atakayepatikana akifanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria. Wakulima watahamasishwa kupanda miwa inayokomaa kwa kipindi baina ya miezi 13 na 18.

Ripoti pia inasihi wakulima kuchanganya miwa na mazao mengine mashambani mwao.

Hata hivyo, si watu wote watakaofurahia ripoti hii kwani inapendekeza kuvunjiliwa mbali kwa bodi simamizi za kampuni hizi na kuteua wataalamu wenye ujuzi kwenye bodi hizi.

Licha ya kuzungumzia bodi, ripoti haizungumzii kuteuliwa kwa wakurugenzi wa kampuni za kiserikali. Kwa mfano, ni vigumu kwa mtu wa kabila tofauti na Waluo kuteuliwa mkurugenzi wa kampuni za kanda ya Nyanza.

Katika kampuni za Nzoia, wakurugenziwote katika kipindi cha miaka 12 iliyopita ni kutoka jamii ya Wabukusu.

Ili kupunguza mizigo ya kifedha, wafanyikazi watapunguzwa, ripoti yasema.

Ripoti pia imekopa mtindo katika sekta mbalimbali za kitaaluma kwa kupendekeza kwamba kuwe na mwongozo wa maadili katika sekta ya miwa ambao utafuatwa na wadau wote. Mwongozo huu utengenezwa na wadau wa miwa.

Bima kwa wakulima pia ni habari njema kwani itawakinga wakulima dhidi ya hasara inayotokana na kilimo cha miwa.

Kodi za miwa

Suala na kodi katika miwa imeguswa bila mapendekezo kamili. Ripoti inapendekeza ‘kuangaliwa’ kwa kodi za miwa ambazo kwa jumla ni asilimia 26 ambayo huongeza bei ya sukari nchini.

Tani moja ya sukari kwa sasa hutengenezwa kwa dola 800 badala ya dola 450 katika kiwango cha kimataifa.

Pia inapendekeza kwamba serikali ya kitaifa na za kaunti zisawazishe kodi ili kuimarisha hali ya kiuchumi nchini.

Ingekuwa vyema iwapo wangependekeza kuondolewa kwa kodi hizi moja kwa moja jinsi walivyopendekeza kurudishwa kwa kodi ya maendeleo almaarufu Sugar Development Levy (SDL) ambayo imekuwa ikitumika kwa maendeleo na utafiti katika sekta ya sukari. Kodi hii ndiyo ambayo ilizipa kampuni za sukari pesa za maendeleo.

Nguvu mpya

Tume ya Ubinafsishaji sana imepata nguvu mpya ya kuuza kampuni za serikali baada ya ripoti kupendekeza kwamba ziuzwe haraka iwesekanavyo. Hata hivyo huenda zisiuzwe haraka kwa sababu inapendekeza kubuniwa upya kwa kamati inayohusika na uuzaji ili kujumuisha wadau wote.

Kuagiza sukari kutoka nje

Kampuni za sukari pia hazina habari njema kwa sababu zimekatazwa kuagiza sukari kutoka nje wakati kuna ukosefu. Kampuni zimekuwa zikisema kwamba zinafaa kupewa nafasi ya kuagiza kulingana na uwezo wao wa kusaga badala ya wafanyibiashara.