Seneta alia wanajeshi wa Jubbaland wameteka Mandera, Murkomen akana
SENETA wa Mandera Ali Roba amelalamikia kile anachokitaja kama uwepo wa wanajeshi wa Jubbaland, Somalia ndani ya mji wa Mandera, akisema hali hiyo ni hatari kwa wakazi na inahujumu uhuru wa Kenya.
Alitoa kauli hiyo huku Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen akisema serikali haina habari kuhusu uwepo wa wanajeshi kama hao nchini na inaendesha uchunguzi kubaini ukweli kuhusu madai hayo.
Kwenye taarifa aliyoweka katika kurasa zake za mtandao wa kijamii Jumatano, Septemba 3, 2025, Seneta Roba alisema biashara katika mji wa Mandera zimeathirika na familia kutoroka makwao kwa hofu ya madhara ya silaha zinazotumiwa na wanajeshi hao wa Jubbaland.
“Taharuki imetanda katika mji wote huku wanajeshi wa Jubbaland na wale wa Serikali ya Somalia wakijiandaa kwa vita,” akasema.
“Ni usaliti mkubwa kwa watu wetu kwa serikali kuruhusu wanajeshi wa Jubbaland kuendesha shughuli zao Mandera na kuweka maisha na mali ya Wakenya hatarini,” akasema Seneta Roba.
Seneta huyo ameitaka Serikali ya Kenya kuwaondoa wanajeshi wa Jubbaland Mandera na ilinde mipaka yake.
Bw Roba ameonya kwamba serikali isipowaondoa wanajeshi hao italazimika kuwajibikia madhara yoyote yatakayotokana na uwepo wa wanajeshi wa kigeni Mandera.
“Aidha, wakazi watalazimika kujilinda endapo serikali itafeli kuchukua hatua. Maisha ya watu wetu hayafai kuhatarishwa eti kwa sababu tunaunga mkono serikali hii ya Kenya Kwanza,” Bw Roba akaongeza.
Lakini akiongea katika kaunti ya Busia, Waziri Murkomen alielezea kuwa serikali itahakikisha uwepo wa usalama mjini Mandera na maeneo yote ya mpakani.
“Kufikia sasa hamna wanajeshi wa kigeni Mandera au popote pale. Lakini maafisa wa usalama wameanzisha uchunguzi kufuatia kuibuka kwa madai kwamba kuna wanajeshi wa kigeni eneo hilo,” Bw Murkomen akawaambia wanahabari.
Waziri alisema sera ya serikali ni kuhakikisha kuwa wahalifu hawaingii nchini, isipokuwa wale wanaotafuta hifadhi.
“Ikiwa kuna wale wanaotafuta usalama nchini kutokana na vita vinavyoendelea kati ya wanajeshi wa Jubbaland na Somalia, watu kama hawa watasaidiwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa,” Bw Murkomen akasema.
Mnamo Ijumaa wiki jana, Gavana wa Mandera Adan Khalif aliitaka serikali kuwaonda wanajeshi wa Jubbaland mjini Mandera.
Alidai wanajeshi hao wamepiga kambi katika eneo la Boder Point One na wanazua hofu kiasi cha kuchangia kufungwa kwa shule moja.
“Mandera haiwezi kuwa uwanja wa vita kati ya vikosi vya Somalia. Hatuna maslahi yoyote katika migogoro ya Somalia. Tunataka amani,” alisema Gavana Khalif.
Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga pia wametoa kauli zao kuhusu suala hilo wakimtaka Rais William Ruto kuamuru kuondolewa kwa wanajeshi hao wa kigeni.
Mnamo Jumanne, wakazi wa Mandera walifanya maandamano kushinikiza serikali ichukue hatua wakisema wamekoseshwa amani na uwepo wa wanajeshi hao.
Uhasama kati Jubbaland inayojitawala na Serikali ya Somalia umesababisha mapigano kati ya wanajeshi wao. Mara kadhaa mapigano hayo husambaa hadi Mandera, Kenya.