• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 5:46 PM
SHAKA ZULU KIUMBE: Mwanamuziki, mwigizaji na mpishi hodari

SHAKA ZULU KIUMBE: Mwanamuziki, mwigizaji na mpishi hodari

Na JOHN KIMWERE

BILA shaka ni miongoni mwa wasanii wanaoibukia wanaoendelea kuvumisha jukwaa la muziki wa kumtukuza Mungu kwa mitindo ya kizazi kipya inayoendelea kuchangamsha wengi. Kadhalika anajivunia kutunukiwa kipaji cha uigizaji.

Hayo tisa, kumi anaendesha biashara ya kuuza nguo mjini Mombasa pia ni mwanafunzi katika taasisi ya Kenya Course National Polytechnic anakosomea kuhitimu kwa cheti kama mpishi.

Katika mpango mzima chipukizi huyu, Nzulu Munywoki ambaye kimuziki anakwenda kwa jina Shaka Zulu Kiumbe anapania kujituma mithili ya mchwa huku akilenga kutamba kote Afrika Mashariki na Dunia nzima kwa jumla.

Pia anadokeza kuwa anataka kuibuka kati ya wanamuziki mahiri nchini na kutumia muziki kama kitengo uchumi.

Mtunzi huyu ambaye ametia wino kandarasi ya mwaka mmoja na lebo ya Mketu Production (MK2) ya mjini Mombasa wiki iliyopita aliachia teke moja inayokwenda kwa jina ‘Njiwa’ aliyomshirikisha msanii Mwanzilishi the Don (Mwanza Kambi).

”Ninaamini nina uwezo tosha kufanya vizuri katika muziki na kufikia upeo wa juu kama ilivyo kwa wanamuziki wengine wanaotunga nyimbo za kumtukuza Mungu,” anasema na kuongeza kuwa anahisi nyimbo hiyo itafanya vizuri kuliko zingine alizowahi tunga.

Ingawa hajapata mashiko katika ulingo wa muziki anajivunia kunasa tuzo mbili kutokana na tambo zake.

Mwaka 2018 nyimbo yake ‘Nora’ ilimwezesha kutwaa tuzo ya Mukuru Awards, kitengo cha msanii bora wa kiume wa mwaka. Ujio wa tuzo hilo ulikuwa baada ya teke yake ‘Nipe’ kumpa tuzo ya Tetemesha Awards 2016 kitengo cha Nyimbo bora ya mwaka.

Anaamini kuwa mwaka ujao atakuwa miongoni mwa orodha ya wasanii watakaoteuliwa kuwania tuzo kwenye hafla ya Coast Awards.

”Kusema kweli nalenga kutumia nafasi ya kuwa chini ya lebo mpya angalau nirekodi nyimbo zitakaonijenga kimuziki,” alisema.

Chipukizi huyu anayeelekea kutinga umri wa miaka 27 amefaulu kughani takribani nyimbo kumi zikiwamo:’Nipe’, ‘Nora,’ ‘Wao,’ ‘Mwanadamu,’ ‘Kutanga,’ ‘Intimadation,’ ‘Usiniache,’ na ‘Nimempata,’ kati ya zingine. “Hata hivyo nimerekodi na kutoa video tano ‘Nipe’ ‘Wao,’ ‘Nora,’ ‘Intimadation,’ na ‘Njiwa.’

Chipukizi huyu alianza kutunga muziki wa injili maana alililewa maisha ya Kikristo tangu akiwa mtoto.

”Sina nia ya kubadilisha mtindo wangu mbali napania kuendelea kutunga nyimbo zinazoweza kusikizwa na watu wote watoto na wazazi tofauti na wengine wetu,” akasema.

Anakiri kwamba muziki unalipa lakini baada ya msanii kuweka msingi mzuri ingawa kwa wengi wao huchukua muda mrefu.

Kijana huyu anasema anapenda kuketi na kusikiza nyimbo za Mungu za wasanii wengine kama ‘Vanity,’ ‘Kazi ya msalaba,’ na ‘Boda boda’ ‘Ugali sosa,’ tugho zao waimbaji Daddy Owen na Man Ingwe.

Katika masuala ya maigizo ameshiriki filamu tatu ambapo anajivunia kushiriki moja mwaka 2017 kwa jina ‘Mahasidi’ akiwa muhusika mkuu iliyobahatika kupeperushwa kupitia K24 TV.

Pia mwaka 2018 alishiriki nyingine iliyokwenda kwa jina ‘One in a milioni’ iliyopeperushwa kupitia Maisha Magic. Kadhalika alishiriki filamu ‘Nganya’ chini ya kampuni moja kutoka Uturuki.

Kijana huyu amekutana na changamoto gani? Anasema imekuwa vigumu kazi za waimbaji wanaokuja kwenye gemu kukubalika na wapenzi wa nyimbo za burudani.

Aidha anadokeza kuwa kutoa video za maana ni gharama kubwa kwa wasanii chipukizi ambapo hulemea wengi wao.

”Bila kuweka katika kaburi la sahau wasanii chipukizi hupitia pandashuka chungu nzima hasa kwa kuzingatia jamii huwachukulia wanamuziki kuwa wenye pesa. Unapoitwa msanii baadhi yetu mitaani hutarajia huishi maisha ya hadhi ya juu pia uwe unamiliki gari lakini sivyo,” alisema.

Kadhalika anadokeza hatawahi sahau mwaka 2016 alipojikuta kwenye wakati mgumu baada ya mama mmoja kumsimamisha na kumwomba msaada wa Sh120,000.

Anasema mama huyo alimwomba msaada huo ili kumrejesha mwanae shuleni ilhali binafsi alikuwa hawajawahi kupata pesa kiwango hicho.

Kadhalika anasema kuwa baadhi ya wafuasi wao wa kike huibuka balaa kwa wanamuziki wakiume hasa baada ya kuwataka kimapenzi.

Licha ya kutofanya makubwa chipukizi huyu sio mchoyo wa mawaidha. Anashauri wanamuziki chipukizi wajiamini kwa kazi zao bila kusikiza baadhi ya wenzao wasiwatakia mema.

”Ningependa kuwaambia watunzi wanaoanza kujituma katika masuala ya muziki wafahamu kwamba hakuna chochote kizuri hupatikana rahisi lazima wajitahidi kadiri ya uwezo wao,” alisema.

Anasema ili wasanii wafaidi kutokana na tambo zao wanastahili kuungane na kuanzisha mtandao wa kutupia kazi zao na kufanya rahisi kwa wafuasi wao kuzipata kwa ada fulani.

Anawataka wasanii wa kike ambao tayari wamejiunga na ulingo wa nyimbo za kumtukuza Mungu wafahamu sekta hii imejaa pandashuka na majaribio tele wala wasikubali kupondwa na maprodusa.

Vile vile anasema kwamba maprodusa na MaDJ hawana jingine mbali wanastahili kujifunga nira na kushirikiana kufanya kazi bega kwa bega ili kuinua wanamuziki chipukizi nchini.

Kadhalika aliongeza kuwa ni jambo lililo wazi kwamba vyombo vya habari nchini vimezipigia chini nyimbo za wanamuziki wanaoinukia kwa madai yasio na msingi.

Anawaambia wafuasi wake kuwa anapania kuonekana katika ujio tofauti mwaka ujao tofauti na miaka iliyopita maana anahisi amekaa vizuri baada ya kusaini mkataba na lebo mpya.

Chipukizi huyu aliyezaliwa mjini Mombasa, alisomea Shule ya Msingi ya Miritini, Mombasa mwaka 2001 hadi mwaka 2009. Kisha Shule ya Upili alisomea Peter Kibukosya mwaka 2010 hadi 2013.

You can share this post!

NORAH OWADE: Mpodoaji wa kisasa asaka makuu katika uigizaji

Re-Union yahifadhi taji kwa mara ya tatu mfululizo

adminleo