Hili dume ni kupe nataka kulitema, waonaje Shangazi?
Mambo Shangazi? Nina mpenzi lakini nahofia uhusiano wetu hautadumu. Mwanamume huyo ana kazi nzuri lakini mara nyingi tunatumia pesa zangu. Ninampenda lakini nahisi ananitumia vibaya.
Katika hali ya kawaida mwanamume ndiye anafaa kugharamia mahitaji ya mpenzi wake. Akizoea kukutegemea hatabadilika akiwa mume wako. Ni heri umuepuke mapema.
Kumbe rafiki alikuwa anasubiri tukosane ili amnyakue!
Nilikosana na mpenzi wangu mwezi uliopita. Siku chache baadaye mwanamke rafiki yangu aliniambia mpenzi wangu anamtaka. Amekuwa akimtamani na ninajua ni yeye aliyefanya tukosane. Nimeamua kuvunja urafiki wetu. Waonaje?
Sasa umejua huyo si rafiki ni adui. Inaonekana amekuwa akijaribu juu chini kuhakikisha mmeachana ndipo ampate. Hatimaye amefaulu. Ni heri uvunje urafiki huo kwa sababu hauna manufaa kwako.
Natamani kuolewa tena
Niliachana na mume wangu miaka miwili iliyopita nilipogundua alikuwa na mpango wa kando. Nina miaka 36 na watoto wawili na ninatamani sana kuolewa tena.
Wewe bado ni mwanamke mchanga na ukitaka kuolewa tena ni sawa. Najua unahofia kuvunjwa moyo tena. Ushauri wangu ni kwamba uwe na subira unapotafuta mpenzi ili upate mume mzuri.
Ana mimba na siko tayari kumuoa, nifanyeje?
Mpenzi wangu anatafuta kazi mjini na nimekuwa nikiishi naye nyumbani kwangu. Nimegundua ana mimba na sijui nitafanya nini kwa sababu bado sijaamua kuoa. Naomba ushauri wako.
Iwapo ulijua hukuwa tayari kuoa ungeepuka mimba hiyo kwa kutumia kinga. Sasa mwenzako anakutegemea wewe. Itabidi uendelee kumtunza huku ukipanga kuhalalisha ndoa yenu.