Mke wangu yuko kwa simu akipika, simu chooni, simu tukila uroda!
Mke wangu ana tabia ambayo inaniudhi sana, haachi simu hata sekunde moja, jicho liko kupekuapekua rununu yake kila wakati. Hata tukiwa mazungumzoni au chumbani, amekwamilia tu kwa simu. Nimsaidieje?
Huenda anatawaliwa na simu. Zungumza naye na ikiwa jitihada hizi hazitafuadafu, basi mtahitaji ushauri kutoka kwa mshauri nasaha.
Lazima anizalie mtoto kwanza ndio nimuoe
Nimekuwa katika uhusiano na huyu binti kwa miaka mitatu. Tunapendana sana na hata tushatambulishana kwa jamaa zetu. Amesisitiza tuoane, japo hataki kunizalia kwanza. Siwezi!
Inashangaza kwamba unataka kumbebesha binti wa wenyewe mzigo ili umuoe. Ana uhakika upi kwamba akishakuzalia utamuoa? Huo ni mzaha wewe!
Anafura kila nikiposti picha zetu mitandaoni
Mume wangu amekuwa akizua vurugu kila nikichapisha mtandaoni picha zetu tukiwa pamoja. Nimeanza kushuku ana uhusiano wa pembeni. Nifanyeje?
Nani aliyekuambia kwamba ukimposti mtandaoni ni hakikisho la penzi lake kwako? Mapenzi yenu katika uhusiano yanapaswa kuwa siri yenu wawili na wala sio jambo la kuutangazia ulimwengu.
Mavyaa balaa, mwanawe anamsikiza kuniliko
Mume wangu amekuwa kero siku hizi, hanisikii kamwe. Badala yake, anatii kila kitu ambacho mamake anamwambia mamake, na hali hii inaniudhi.
Katika uhusiano na hata ndoa, ni upumbavu kwa mke kuanza kushindana na mama mkwe. Japo kuna mambo ambayo ni ya siri kati yako na mumeo, mpe mamake pia nafasi ya kuhusika na maisha ya mwanawe.