Shangazi Akujibu

NIPE USHAURI: Mke wa jirani hupenda kuja kwangu akidai kuhisi upweke; naogopa

May 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Shikamoo shangazi. Nilimaliza shule mwaka uliopita na ninaishi mjini nikitafuta kazi. Kuna mke wa jirani yangu mtaani ambaye anataka tuwe wapenzi. Mumewe anafanya kazi mbali na amezoea kuja kwangu akidai anahisi upweke. Nifanyeje?

Wewe bado ni mdogo na unafaa kuepuka mambo yanayoweza kukuletea shida maishani. Huyo ni mke wa mtu na ni hatari kupendana naye kwa sababu hatimate mumewe atajua. Kataa ombi lake na umkataze kuja kwako.

Nimeoa mwaka mmoja tu lakini mke ananishuku

Ni karibu mwaka mmoja sasa tangu nilipooa. Nikichelewa nje na marafiki hasa wikendi mke wangu huzua ugomvi akidai ninakuwa na wanawake. Nifanyeje?

Ndoa yenu bado ni changa na ni lazima mke wako anahisi upweke ukimuacha nyumbani peke yake. Itakuwa vyema kuandamana naye wikendi ili awajue marafiki zako na kuondoa hofu kuhusu wanawake wengine.

Huyu ananipenda kweli?

Niligundua mpenzi wangu ana mke na nikaamua kuendelea na uhusiano huo kwa sababu anatosheleza mahitaji yangu. Sasa amenikataza kuwasiliana naye kwa simu akihofia mkewe atagundua. Ananipenda kweli?

Umeamua kuendelea na uhusiano huo hata baada ya kugundua huyo ni mume wa mtu. Wewe sasa ni mpango wa kando na hufai kufanya chochote kinachoweza kuhatarisha ndoa yake. Mambo ni mawili – utii maagizo yake ama uachane naye utafute wako.

Mke wangu hajarudi!

Mwezi uliopita tuligombana na mke wangu na akarudi kwao. Nilimfuata huko tukazungumza na akaahidi kurudi. Wiki mbili zimepita na hajarudi. Nikimpigia simu pia hajibu. Nifanyeje?

Kulingana na maelezo yako, ndoa yenu imekuwa na matatizo kwani unasema mmekuwa mkigombana. Inawezekana kuwa ameshauriana na wazazi wake na wakaamua aachane na ndoa hiyo. Ni vyema urudi kwao ili ujue msimamo wake.