SHERIA: Huwezi kumzuia kuoa au kuolewa akitimiza umri
Na BENSON MATHEKA
LOISE , msomaji kutoka Kuria anataka kujua ikiwa ni makosa kwa mzazi kumkataza binti yake kuolewa katika ndoa ya kitamaduni na mtu anayejua hana tabia nzuri.
Anasema binti yake anapanga kuolewa na mwanamume ambaye ana rekodi ya uhalifu na kufukuza wanawake. Anahisi kuwa binti yake anavutiwa na mali ya mwanamume huyo na atateseka kama wanawake waliotangulia kuolewa naye.
Sheria ya ndoa ya Kenya inasema ndoa ni muungano wa hiari uwe wa kitamaduni, Kikristo, Kiislamu, Kijamii au ndoa yoyote inayotambuliwa kisheria.
Ni vigumu kumzuia mtu kuolewa na anayemtaka.
Kile ambacho msomaji huyu anaweza kufanya ni kukataa kupokea mahari kwa sababu inachukuliwa kuwa thibitisho la ndoa ya kitamaduni.
Hii ni baada ya juhudi za kumshawishi au kumshauri binti yake kukosa kuzaa matunda.
Ndoa ya kitamaduni ni lazima itimize mahitaji yote ya kisheria. Ni muhimu kufahamu kwamba hakuna mzazi anayefaa kukataza au kushurutisha binti au mwanawe kuoa au kuolewa.
Kisheria, mzazi hawezi kulazimisha au kukataza binti yake kuolewa na mwanamume anayemtaka hasa katika ndoa ya kitamaduni ambayo inaruhusu wanaume kuoa wake wengi.
Ndoa kitu cha hiari
Kwa sababu ndoa ni hiari, kile ambacho mzazi anaweza kufanya ni kutoshiriki utaratibu wa ndoa.
Muungano kati ya mwanamume na mwanamke usiofuata utaratibu wa ndoa hautambuliwi kisheria hata ukiwa wa kitamaduni.
Sawa na jinsi sheria ya ndoa haiwaruhusu wazazi kuwachagulia watoto wao wachumba, pia haitoi nafasi kwao kuwakataza kuolewa na wanaochagua.
Sheria inasema kwamba ni lazima watu wawili wakubaliane wenyewe bila kulazimishwa kuoana.
Kukataza, kulazimisha mtu kuoa au kuolewa ni kuvunja sheria ya ndoa ya Kenya na mtu anaweza kufungwa jela akipatikana na hatia au kutozwa faini.
Hata hivyo ni muhimu kumshauri mtu na kuacha afanye uamuzi wake mwenyewe