Makala

SHERIA: Mume au mke ana haki ya kuomba talaka

March 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

“NI nani kati ya mume na mke anafaa kuwasilisha kesi ya talaka kortini,” anauliza Joseph Kariuki akiwa Lamu.

Naye Gitau S akiwa Molo anataka kujua iwapo mtu anaweza kuwasilisha kesi ya talaka kwa niaba ya rafiki yake.

Kuhusu swali la Bw Kariuki, upande wowote; yaani mume au mke anaweza kuwasilisha kesi ya talaka kortini akiwa na sababu za kutosha zenye msingi wa kisheria.

Kumbuka sheria ya ndoa inasema mume na mke wana haki sawa kisheria wakati wa kufunga ndoa, wakiwa kwenye ndoa na wakati wa kuvunja ndoa.

Hivyo basi, kila mmoja ana haki ya kuchukua hatua ya kisheria kuhusu ndoa yao ikiwa ni pamoja na kuwasilisha ombi la talaka.

Katika swali la pili la Bw Gitau, sheria inatambua mume na mke kama wahusika wakuu katika ndoa. Ndio maana inasema ndoa ni muungano wa hiari kati ya mwanamume na mwanamke.

Kile ambacho mtu anaweza kufanya ni kumsaidia rafiki au jamaa kujua jinsi ya kuwasilisha ombi la talaka iwapo mhusika mwenyewe anahisi kuna sababu zenye msingi wa kisheria kuvunja ndoa yake.

Msaada huu ni lazima uwe wa kisheria.

Ni makosa kulazimisha rafiki au mtu yeyote kutaliki mume au mke. Kimsingi, kuomba talaka ni kumuacha mume au mke kwa zaidi ya miaka miwili kwa hiari au kwa amri ya mahakama.

Katika hali kama hii, ndoa hiyo huchukuliwa kuwa imevunjika kabisa.

Aidha ni lazima iwe miaka miwili inayotangulia tarehe ya kuwasilisha kesi ya talaka.

Misingi mingine ya kuvunjika kwa ndoa kiasi cha kutorekebika ni mke au mume akiwa mzinifu, akiwa katili kwa mwenzake au kwa watoto wao au kumnyima haki zake.

Ndoa huchukuliwa kuwa imevunjika kabisa mume au mke akifungwa jela miaka saba au akifungwa jela maisha.

Sheria inasema mtu akisukumwa jela maisha, ndoa yake huwa inavunjika kiwango cha kutoweza kurekebishwa na hii ni mojawapo wa msingi ambao mahakama huzingatia kuamua kesi ya kutoa talaka.

Sheria pia inasema mtu anaweza kuomba talaka ikithibitishwa mume au mke wake anaugua maradhi ya akili yasiyoweza kupona.

Hii ni lazima ithibitishwe na madaktari wawili waliohitimu, mmoja akiwa mtaalamu wa masuala ya akili.