SHERIA: Sheria hairuhusu kuoa au kuolewa kabla ya talaka
Na BENSON MATHEKA
JE, ni hatua gani za kisheria zinazofaa kuchukuliwa mtu akioa mke wa pili kabla ya kumtaliki mke wa kwanza au mke anayeolewa akitengana na mumewe bila talaka?
Wafula, Bungoma
Kulingana na sheria ya ndoa ya Kenya, mtu hafai kuoa mke wa pili kabla ya talaka ikiwa amefunga ndoa ya kijamii au ya Kikristo.
Mtu akifanya hivyo, huwa anajiingiza katika kosa la kuwa na wake au waume wawili (Bigamy) na anaweza kushtakiwa kortini kwa makosa kadhaa.
Kwanza, akifanya harusi anaweza kushtakiwa kwa kutoa habari za uongo kwa afisa anayesimamia au kuongoza harusi. Hii ni kwa sababu kabla ya kufanya harusi, wanandoa hutakiwa kutoa habari kwa msajili wa ndoa au mtu anayesimamia eneo la ibada anakofanyia harusi akieleza ikiwa amewahi kupata talaka au ikiwa ni mjane.
Kisheria mtu akidanganya anapotoa habari hizi huwa anatenda uhalifu kwa kutoa habari za kupotosha.
Anaweza pia kushtakiwa kwa kutoa habari za uongo kwa mchumba anayeoa kama mke wa pili au kwa mume ikiwa mwanamke anakubali kuolewa kabla ya kupata talaka.
Kwa wanaoamua kuishi na wanawake au wanaume wengine kama mume na mke wakitengana na waume au wake zao bila kufunga harusi, huu ni mpango wa ‘njoo tuishi’ ambao ni mahakama inayoweza kuamua iwapo unatimiza mahitaji ya ndoa.
Kile sheria inasisitiza ni watu kuhakikisha wamefuata sheria kikamilifu.
Hata hivyo, katika ndoa za kitamaduni, mtu anaweza kuoa wake wengi ikiwa ana uwezo wa kuwatunza.
Sheria ya ndoa ya Kenya haiweki idadi ya wake ambao mtu anafaa kuoa katika ndoa ya kitamaduni.
Katika ndoa za kijamii na Kikristo ni muhimu kwa mtu kupata talaka kwanza kabla ya kuamua kuoa au kuolewa.
Hapa ninataka kusisitiza kwamba kutengana bila cheti cha talaka sio tiketi ya mtu kuoa au kuolewa tena.