SHERIA: Ukioa wawili huwezi kubadilisha ndoa iwe ya mke mmoja
Na BENSON MATHEKA
MSOMAJI Joyce Kariithi wa Embu anataka nifafanue jambo kuhusu ndoa za wanawake wengi, yaani ndoa ambayo mwanamume anaruhusiwa kisheria kuoa zaidi ya mke mmoja.
Bi Kariithi anataka kujua ikiwa mwanamume aliye na wake wengi anaweza kubadilisha ndoa yake kuwa ya mke mmoja.
Anasema mume wa rafiki yake ana wake wawili na kuna fununu kwamba anapanga kufunga ndoa kanisani na mke wa pili.
Katika makala yaliyotangulia nimewahi kueleza kuwa ndoa ya wake wengi inaweza kubadilishwa kuwa ya mke mmoja kabla ya mume kuoa mke wa pili.
Ni muhimu kuelewa kuwa sheria inaeleza kwamba ndoa ya kitamaduni na ya Kiislamu huchukuliwa kuwa ya wake wengi.
Hii inamaanisha kwamba mwanamke akikubali kuolewa katika ndoa ya kitamaduni au Kiislamu, mumewe anaweza kuoa mke wa pili.
Sheria inaeleza kuwa ndoa ya wake wengi haiwezi kubadilishwa kuwa ya mke mmoja ikiwa mume tayari ana wake wawili.
“Mtu akiwa katika ndoa ya wake wengi, hataweza kushiriki ndoa nyingine ya mke mmoja,” ndivyo inavyosema sheria ya ndoa ya Kenya.
Akiuka sheria
Kwa hivyo, ikiwa mume wa rafiki ya Bi Kariithi ana wake wawili, anakiuka sheria kwa kutaka kuoa mke kanisani au katika ofisi ya msajili ambayo chini ya sheria ya ndoa ya Kenya ni ndoa ya mke mmoja.
Ndoa kama hiyo ikifanyika, itakuwa ndoa batili ambayo inaweza kuzimwa na mahakama kwa sababu kisheria haiwezi kutambuliwa.
Kulingana na sheria ya ndoa mtu akiwa katika ndoa ya mke mmoja hawezi kuoa mke wa pili hadi ndoa ya kwanza ivunjwe kisheria mahakamani. Watu wanaoishi na watu ambao waliolewa au kuoa kanisani kabla ya kupata talaka huwa wanajidanganya kwa sababu kisheria, wao huwa katika uhusiano haramu.
“Mtu akiwa katika ndoa ya mke mmoja inayodumu (ambayo haijavunjwa mahakamani na cheti cha talaka kutolewa) hawezi kuoa mke wa pili katika ndoa ya wake wengi,” inaeleza sheria ya ndoa.