• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 2:35 PM
SHERIA: Wosia wa maandishi una nguvu kuliko ule wa matamshi

SHERIA: Wosia wa maandishi una nguvu kuliko ule wa matamshi

Na BENSON MATHEKA

LEO katika makala haya ninataka kuangazia kuhusu aina za wosia zinazotambuliwa katika sheria ya urithi ya Kenya.

Sheria inasema wosia unaweza kuwa kwa maneno au maandishi hivyo kuna aina mbili za wosia. Hata hivyo, kila aina ya wosia huwa inaidhinishwa ikitimiza vigezo au masharti fulani ya kisheria.

Wosia wa matamshi

Kulingana na sheria ya urithi ya Kenya, wosia unaohusu maneno anayoacha mtu kuhusu anavyotaka mali yake irithiwe hauwezi kukubaliwa ikiwa haukushuhudiwa na watu wawili au zaidi.

Wosia huu unaweza kuwa kwa kurekodiwa au mtu kuagiza mwingine atakavyotaka mali yake isimamiwe, watakaorithi na kiasi watakachorithi.

Aidha, mtu akitoa maneno kuhusu mali yake miezi mitatu kutangulia kifo chake, basi maneno hayo huwa hayatambuliwi kama wosia isipokuwa maafisa wa kijeshi au mabaharia wakifa wakiwa kazini.

Hii inamaanisha kuwa wosia kama huu unafaa kuandaliwa mapema zaidi lakini sio miezi mitatu kabla ya mtu kuaga dunia.

Sheria ya urithi ya Kenya inasema wosia wa maneno, hauwezi kukubaliwa iwapo unatofautiana na ulioandikwa na aliyeutoa kabla au baada ya kuutoa. Hii inaamanisha kuwa wosia wa maandishi una nguvu kisheria kuliko ule wa matamshi.

Mzozo ukiibuka kuhusu wosia wa matamshi, sheria inasema unaweza kukubaliwa ukithibitishwa na mashahidi ambao walikuwa na uwezo wa kuushuhudia.

Wosia wa maandishi

Sheria inasema hauwezi kukubaliwa iwapo aliyeuandika hakutia sahihi au alama ya kidole chake. Wosia wa maandishi unaweza pia kutiwa sahihi na mtu mwingine kwa niaba ya anayeutoa na hii ni lazima iwe mbele ya anayeutoa.

Kulingana na sheria ya urithi ya Kenya, sahihi katika wosia, iwe ya anayeutoa au mtu anayeiweka kwa niaba yake ni lazima ionekana kwamba ilinuiwa kuthibitisha wosia huo na maandishi yenyewe.

Ni sharti kuwe na mashahidi wawili au zaidi kuthibitisha kuwa waliona mwenye wosia akitia sahihi yake au waliona akiagiza mtu mwingine kutia sahihi kwa niaba yake na mbele ya mwenye wosia.

Mashahidi ni lazima watie sahihi zao mbele ya mwenye wosia.

You can share this post!

Baraza tawala lavunja chama cha Bashir, kunadi mali yake

UMBEA: Usiwe zuzu wa mapenzi, kama wataka mume jibebe...

adminleo