SHINA LA UHAI: Gharama ya kudumisha figo mpya inavyolemea wengi
Na BENSON MATHEKA
ALIPOPATA mtu wa kumtolea figo mwaka wa 2014, Joseph Ndirangu alidhani alikuwa amemaliza tatizo lililotishia maisha yake.
Japo alimudu gharama ya kusafiri hadi India kwa matibabu hayo na kwa kweli alirejea nchini salama, gharama ya kutunza figo aliyopachikwa imeanza kumlemea.
Kama watu wengine wanaopachikwa figo kuokoa maisha baada ya zao kukosa kufanya kazi, Ndirangu anasema anahitajika kumeza dawa kila siku kudumisha figo hiyo katika hali njema.
“Ninahitajika kumeza dawa za kuwezesha figo niliyopachikwa kufanya kazi. Sio kumeza kwa siku moja, nameza kila siku kwa muda ambao nitakuwa hai,” asema Ndirangu.
Bei ya dawa hizo, aeleza, ni Sh1,500 kwa siku na kwa mwezi mmoja huwa anahitaji Sh45,000.
“Kwa kila mwaka ninahitaji Sh500,000 kuwa hai. Sio mimi pekee, ni kila mtu aliyepachikwa au anayepanga kupachikwa figo,” asema Ndirangu.
Ili kupata pesa za kununua dawa hizi, huwa anategemea wasamaria wema kwa kuwa hana mapato baada ya kustaafu. Anasema pesa alizokuwa ameweka akiba zimeisha kwa sababu ya gharama kubwa ya dawa.
“Wakati huu wa hali ngumu ya kiuchumi kwa sababu ya janga la corona ni vigumu kupata mtu wa kunisaidia. Nahofia maisha yangu iwapo nitakosa dawa,” asema.
Simon Kimani, aliyestaafu mwaka jana miaka miwili baada ya kupachikwa figo nchini India anasema anatatizika kupata pesa za kununua dawa za kudumisha kiungo hicho.
“Matatizo ya figo ni mzigo kwa masikini. Ni wachache wanaoweza kumudu gharama ya matibabu na utaratibu wa kupachikwa figo nchini na ng’ambo,” asema Kimani, mfanyakazi wa zamani wa kampuni ya Unilever. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) watu 80,000 hupachikwa figo kote duniani kila mwaka. Asilimia 46 ya wanaopachikwa figo huwa wanazipata kwa watu wanajitolea kutoa figo zao kuokoa maisha ya wengine. Ingawa shirika la kitaifa la bima ya afya (NHIF) hulipa gharama ya kima cha Sh500,000 kwa wanaopachikwa figo katika Hospitali Kuu ya Kenyatta, haigharamii dawa za kudumisha figo hiyo.
“Dawa hizo ni ghali mno. Zinagharimu zaidi ya Sh45,000 kwa mwezi na hii hufanya watu walio na matatizo ya figo kuamua kusafishwa kiungo hicho. Sio rahisi kupata mtu wa kujitolea kukupa figo na hata ukimpata, utaratibu wa sheria nchini Kenya ni mrefu ikiwa anayejitolea si jamaa wako wa karibu,” asema mtaalamu wa magonjwa ya figo Dkt Patricia Kimeu.
Anasema japo Hospitali Kuu ya Kenyatta imepunguza gharama ya kupachikwa figo, watu wengi huwa wanaamua kusafiri hadi India kwa sababu wanaweza kununua figo kwa urahisi. Kulingana na hospitali kuu ya Kenyatta, watu 20 huwa wanafanyiwa upasuaji wa kupachikwa figo kila mwaka tangu 2018. Wataalamu wa figo wanasema mtu hutumia dawa akiwekwa figo isiyo yake ili iweze kufanya kazi vyema.
“Mojawapo ya hatari za kupachikwa figo ni kwamba mwili wako unaweza kuikataa inayowekwa. Hii ni kwa sababu kinga ya mwili inaweza kugundua figo hiyo inatoka kwa mtu mwingine. Ili kuzuia hili kutendeka hata baada ya upachikaji kufaulu, mtu anafaa kutumia dawa kutuliza kinga ya mwili wake na kuisawazisha na figo mpya,” asema Dkt Kimeu.
Anasema kwamba mtu anafaa kumeza dawa hizo kila siku anavyoagizwa na daktari ili figo mpya iweze kufanya kazi.
Kukosa kumeza dawa kwa wakati, afafanua, huweka mtu katika hatari ya kupoteza figo yake mpya.
“Ukikosa kumeza dawa, muone daktari wako mara moja,” aeleza.
Kulingana na Shirika la kimataifa la Kidney Fund, dawa hizo huwa zinahakikisha mwili wa mtu haukatai figo mpya. Kupitia tovuti yake www.kidneyfund.org, shirika hilo linasema ingawa zina madhara kwa mwili kwa sababu ya kupunguza kinga ya mwili, dawa hizo ni muhimu kuhakikisha usalama wa figo anayopachikwa mtu.
Dkt Kimeu anasema anayetumia dawa hizo huwa katika hatari ya kuambukizwa maradhi mengine na kwa hivyo anafaa kuhakikisha anapata lishe bora kila wakati.
“Mtu huwa katika hatari ya kuambukizwa maradhi kwa kuwa zinafanya kinga yake ya mwili kupungua. Watu wanaozitumia wanashauriwa kumuona daktari wakianza kupata matatizo ya tumbo. Daktari anaweza kupunguza kiwango cha dawa au kukubadilishia dawa,” asema Dkt Kimeu.
Wataalamu wanasema watu wanaopachikwa figo huendelea na maisha yao ya kawaida wakitumia dawa hizo ipasavyo na bila kuchelewa.
“Tatizo huwa mtu anapokosa pesa za kununua dawa hizo kwa sababu uwezekano wa figo hiyo kuacha kufanya kazi huwa mkubwa mno,” aeleza Dkt Kimeu.
“Wakati mwingine unapata daktari anahitaji kubadilisha dawa hizo baada ya figo kusita kufanya kazi kisha inarudi hali ya kawaida mtu akizitumia inavyohitajika,” asema.
Kwa sababu ya gharama ya kudumisha figo mpya katika mwili, watu wengi wanaopata matatizo ya figo huamua kuwa wakisafishwa kila baada ya muda, huduma ambayo inaendelea kuwa nafuu nchini kufuatia juhudi za serikali za kaunti.
Kwa wakati huu, hospitali nyingi za kiwango cha level five katika kaunti ziko na mashine za kusafisha damu.
Ingawa utaratibu wa kupata figo kutoka kwa watu wasio wa familia ni mrefu humu nchini, wataalamu wanasema umuhimu wa zoezi hilo kufanyiwa nchini ni kuwa mgonjwa anaweza kufuatiliwa kwa muda kuhakikisha figo anayopachikwa inafanya kazi vyema.
Kulingana na Dkt Anthony Were anayesimamia kitengo cha maradhi figo katika hospitali kuu ya Kenyatta, mgonjwa huwa anachunguzwa kwa mwezi mmoja kuhakikisha figo anayowekwa inafanya kazi vyema katika mwili wake. “Kuna figo zinazoacha kufanya kazi miezi sita baada ya mgonjwa kuhakikishiwa yuko salama,” asema.