SHINA LA UHAI: Homa ya nyongo ya manjano katika watoto wachanga
Na BENSON MATHEKA
RANGI ya ngozi yako ikigeuka kuwa ya manjano na ujihisi kuwa mchovu huku mkojo wako ukibadilika na kuwa mweusi, una sababu ya kumuona daktari upesi.
Wataalamu wanasema hizi ni baadhi ya dalili za homa ya nyongo ya manjano(Jaundice).
Rangi ya macho pia inaweza kuwa ya manjano kwa watu wanaopatwa na ugonjwa huu.
Ugonjwa huu unaweza kumpata mtu wa umri wowote na jinsia yoyote na wataalamu wanasema chanzo chake kinaweza kutokana na tatizo la baadhi ya viungo muhimu vya mwili hasa ini au nyongo.
Rangi ya majano hutokana na kiwango cha Bilirubin kwenye damu, ambayo kulingana na wataalamu ni aina ya uchafu unaobaki kwenye damu baada madini ya chuma (iron) kuondolewa.
Kulingana na wataalamu, mtu aliye na dalili hizi ni lazima afanyiwe vipimo tofauti ili kubaini hasa chanzo chake.
Hii ni kwa sababu hali hii inaweza kusababishwa na matatizo ya viungo tofauti vya mwili vinavyohusika na kusafisha damu.
Kulingana na Dkt Ravi Shah, ili kutibiwa maradhi haya, ni lazima daktari afanye vipimo tofauti kubaini kiini chake.
“Kwanza, sababu kuu huwa ni kuwa mwili haukabiliani na Bilirubin ipasavyo, yaani uchafu unabaki kwenye damu baada ya kuondolewa kwa madini ya chuma. Hii huwa sana sana inaanzia kwenye ini na madaktari huchunguza mgonjwa kujua hali ya ini au ikiwa ana maradhi ya Hepatitis,” aeleza
Anasema ini huwa linasafisha damu na kutoa uchafu na wakati Bilirubin inafika kwenye ini, kuna kemikali nyingine zinazochanganyika nayo.
Daktari huyu afafanua kuwa damu ikiwa na viwango vya juu vya Bilirubin , uchafu huu unaweza kuingia katika tishu za mwili na kusababisha hali inayofahamika kitaaluma kama hyperbilirubinemia.
“Hii ndiyo hasa inayosababisha rangi ya manjano kwenye ngozi na macho,” asema.
Dkt Shah anasema mtu akiwa na hali hii huwa ana tatizo lingine la kiafya linalosababisha mwili kuwa na Bilirubin kwa wingi au linalozuia ini kushindwa kuiondoa mwilini.
Anasema mtu anaweza kupata homa ya nyongo ya manjano ikiwa:
• Ana ini lililovimba
Hii inaweza kuzuia uwezo wa ini wa kuondoa bilirubin na kuifanya irundikane katika damu.
• Kuvimba kwa kijifereji cha nyongo
Hii huzuia nyongo kufanya kazi na kuondolewa kwaBilirubin na hivyo kusababisha homa ya nyongo ya majano.
• Kuzibwa kwa vijifereji vya nyongo
Hii huzuia ini kuondoa Bilirubin.
• ‘Hemolytic Anemia’
Hii ni hali ambayo seli nyekundu za damu huharibiwa kwa wingi na upesi kuliko mwili unavyoweza kuziunda. Kiwango cha Bilirubin huwa kinaongezeka seli nyekundu za damu zikiharibiwa.
Wataalamu wanasema hali hii inaweza kurithiwa katika familia japo inaibuka katika vipindi tofauti maishani.
Watafiti wanasema kuna wakati mwili unaweza kugeuka kuwa rangi ya manjano kwa muda kwa watu wanaokula baadhi ya vyakula kwa wingi.
Watu wanaokula karoti, tikitimaji au malenge kwa wingi wanaweza kupata hali hii lakini kwao huwa sio tishio kwa maisha yao.
Matibabu
Kulingana na wataalamu, hali hii hutibiwa kwa kutegemea kinachoisababisha.
“Ikiwa ni ini linasababisha homa ya manjano, lazima lishughulikiwe na mara nyingi huisha tatizo haswa likitibiwa,” aeleza Dkt Shah.
Ili kuepuka hali hii, wataalamu wanashauri watu kuhakikisha wamepata lishe bora. “Homa ya nyongo ya manjano inatokana na utendakazi wa ini. Ni muhimu kwa watu kudumisha lishe bora, kufanya mazoezi kila wakati na kutokunywa pombe kwa wingi,” aeleza Dkt Shah.
Wataalamu wanasema ukianza kuwashwa na ngozi sana na kujikuna vikali ukiwa na hali hii, huwa imefikia hali ya dharura. Unaweza pia kushindwa kulala na baadhi ya watu huwa na mawazo ya kutaka kujitia kitanzi.
Aina zake
Kulingana na tovuti ya Medical News Today kuna aina tatu za homa ya nyongo ya manjano zinazotambuliwa.
1. Ini linapojeruhiwa au kuugua
2. Kuharibiwa kwa wingi kwa seli nyekundu za damu (Hemolytic Jaundice)
3. Kuziba kwa kifereji cha nyongo (bile duct) inayofahamika kama Obstructive Jaundice.
Homa ya nyongo ya manjano kwa watoto
Hali hii inawatatiza watoto wanapozaliwa na kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), asilimia 60 ya watoto wanaozaliwa huwa na homa ya manjano huku asilimia 80 ya wanaozaliwa kabla ya kufikisha miezi tisa wakiwa nayo.
Kulingana na mtaalamu wa afya ya watoto Dkt Nebris Suda wa hospitali ya Calvary, Nairobi, watoto huanza kuonyesha dalili za hali hii saa 72 baada ya kuzaliwa.
“Hii ni kwa sababu seli nyekundu za damu huwa zimeharibiwa. Hii husababisha ongezeko la Bilirubin . Pia, ini huwa halijakomaa na kwa hivyo kukosa uwezo wa kuondoa bilirubin kutoka kwa mwili,” aeleza.
Anasema kwa watoto, dalili za hali hii huwa zinaisha baada ya wiki mbili. Hata hivyo, walio na viwango vya juu zaidi vya Bilirubin huwa wanahitaji matibabu ama kuwekwa damu.
“Hii ni kwa sababu ikikosa kutibiwa, inaweza kusababisha uharibifu wa kudumu wa akili,” asema.
Mgonjwa akifika hospitali akiwa na dalili za maradhi haya, anafaa kueleza daktari historia yake ya kiafya hasa kuhusu matatizo ya tumbo.
Uchunguzi wa mwanzo huhusu hali ya ini. Baadhi ya vipimo huwa ni vya kubaini viwango vya Bilirubin , hali halisi ya damu, Full Blood Count (FBC) au Complete Blood Count (CBC) ili kubaini viwango vya seli zote za mwili (seli nyeupe za damu, seli nyekundu za damu na seli chembe sahani na pia huonyesha wingi/kiwango cha damu-himoglobini).
Madaktari pia hupima ili kubaini ikiwa mgonjwa ana Hepatitis A, B na C maradhi yanayohusiana na ini.
“Kwa kawaida, maradhi ya ini ni chanzo cha hali hii na madaktari wakibaini hali ya kiungo hiki huwa katika hali nzuri ya kumshauri mgonjwa ipasavyo,” asema Dkt Shah.