Makala

SHINA LA UHAI: HPV, virusi vinavyoendelea kuwa adui wa mtoto wa kike

December 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na PAULINE ONGAJI

ALIPOGUNDUA kwamba alikuwa katika kiwango cha nne (stage four) cha maradhi ya kansa ya mlango wa uzazi mwaka wa 2015, Rose, 41, aliishiwa na matumaini ya kuendelea kuishi.

Ili kuokoa maisha yake alilazimika kuanza matibabu mara moja, tiba iliyohusisha upasuaji, taratibu za tibakemia (chemotherapy) na tibaredio (radiotherapy), ambapo mwishowe alipoteza kizazi chake na hivyo hawezi kupata watoto tena.

Kwa bahati nzuri mama huyu wa watoto wanne tayari alikuwa ashakuwa mzazi. Lakini kwa maelfu ya wasichana na wanawake wanaopatikana na maradhi haya, mambo huwa tofauti kwani mbali na kupoteza uwezo wao wa kupata watoto, maisha yao huwa hatarini.

Utafiti wa Wizara ya Afya unaonyesha kwamba maradhi haya husababisha vifo vya wanawake wanane kila siku nchini Kenya, idadi ambayo ni sawa na vifo 3,286 kila mwaka. Aidha, visa vipya 5,250 vya aina hii ya kansa huripotiwa nchini kila mwaka.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani, hapa nchini kansa ya lango la uzazi ndio aina ya saratani inayoathiri sana wasichana na wanawake kati ya miaka 15-44. Barani Afrika takwimu zinaonyesha kwamba Kenya, Malawi na Zimbabwe ndio mataifa ambayo huchangia idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na kansa hii.

Na ili kukabiliana na janga hili katika siku zijazo, mwezi Oktoba, serikali ya Kenya kupitia Wizara ya Afya ilizindua kampeni ya kutoa chanjo dhidi ya aina ya virusi vya Human papilloma virus (HPV) vinavyosababisha maradhi ya kansa ya lango la uzazi.

Ni kampeni zilizonuiwa kulenga watoto wasichana wa miaka kumi, hatua iliyoonekana kama ufanisi mkuu kwa Kenya.

Kwa hivyo, fursa hii ilipojitokeza, Bi Priscilla*, alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba bintiye mwenye miaka kumi yuko miongoni mwa waliopokea chanjo hii.

“Nimeshuhudia kansa hii kwa macho na nimepata fursa ya kuona wanawake ninaofahamu wakiugua, na hivyo lazima ningehakikisha kwamba binti yangu anaipokea. Na utakapofika wakati wake kupokea dozi nyingine ya chanjo mwaka ujao, bila shaka nitahakikisha kwamba anafanya hivyo,” aeleza.

Lakini japo kwa Bi Priscilla matumaini ya bintiye kuepuka maradhi haya siku zijazo yako juu, kuna baadhi ya watu waliojitokeza kupinga vikali hatua hii ya serikali.

Kwanza kabisa Kanisa Katoliki halikuficha pingamizi zake dhidi ya chanjo hii. Aidha, muungano wa madaktari wa kikatoliki nchini (KCDA), ambao umekuwa ukishinikiza umuhimu wa kutoshiriki ngono kabla ya ndoa, ulihoji kwamba watoto hawapaswi kukumbwa na wasiwasi wa kuambukizwa virusi vya HPV.

Kwa upande mwingine, kulichipuka kikundi cha wanaharakati waliokuwa wakishuku umuhimu wa chanjo hii ambayo inanuiwa kukinga wasichana kutokana na aina chache za virusi vya HPV.

Emily ni mmoja wao. Ni mwanaharakati dhidi ya maradhi ya kansa na mmoja wa watu wanaopinga vikali chanjo hii. Anashuku umuhimu wa chanjo hii.

“Kwa nini tunaharakisha kuwapa wasichana wetu chanjo hii ilhali inawakinga kutokana na aina mbili pekee za virusi vya HPV? Nini kitakachowalinda kutokana na aina zingine hizo?”

Kulingana na Shirika la Afya Duniani WHO, hapa nchini aina ya virusi vya HPVType 16 husababisha takriban nusu ya visa vya maradhi ya kansa ya lango la uzazi. Kwa upande mwingine, HPVType 45 husababisha asilimia 15.9 ya visa vya maradhi ya kansa, huku aina ya Type 18 ikichangia asilimia 15 ya visa vya kansa ya lango la uzazi.

Kuna aina mbili za chanjo dhidi ya virusi hivi, ambazo zimeidhinishwa na WHO. Mojawapo ya chanjo hizo ni ile inayolenga Type 16 na 18 ambazo zinasababisha asilimia 71 ya kansa zote za lango la uzazi nchini.

Aidha, kuna chanjo nyingine yenye uwezo wa kukinga kutokana na aina sita za virusi vya HPV, miongoni mwao 6, 11, 16 na 18, pamoja na vidutu vya sehemu nyeti (genital warts).

Nchini Kenya, chanjo inayotolewa ni Gardasil, kwa majina mengine Gardisil au Silgard au mwunganisho wa chanjo za virusi vya HPV aina 6, 11, 16 na 18. Chanjo ya Gardasil inatengenezwa na kampuni ya by Merck Sharp & Dohme, kampuni ya utengenezaji dawa nchini Amerika.

Chanjo hii inatolewa kwa dozi mbili kuambatana na miongozo ya kimataifa ya WHO, na huzuia maambukizi ya baadaye dhidi ya maambukizi ya virusi vya HPV kwa kuchochea uzalishaji wa seli zinazoitwa antibodies ambazo hukabiliana na virusi hivi.

Ukweli kuhusu chanjo hii- WHO

Kulingana na ripoti iliyozinduliwa na WHO miaka miwili iliyopita, chanjo hii imeonekana kuwa na faida ambapo kumekuwa na upungufu wa matatizo ya kiafya yanayosababishwa virusi vya HPV na kansa ya lango la uzazi. Vile vile, visa vya maambukizi ya vidutu vya sehemu nyeti vimepungua kwa zaidi ya asilimia 90.

Kwa mujibu wa ripoti hii, utafiti uliofanywa ulionyesha upungufu wa maambukizi ya virusi vya HPV na vidutu vya sehemu nyeti kwa asilimia 90, miongoni mwa wasichana walio katika umri wa kubalehe nchini Australia, Ubelgiji, Ujerumani, Uswidi, Uingereza, Amerika na New Zealand.

Aidha, uchunguzi wa kubaini matatizo ya njia ya uzazi miongoni mwa watu waliopokea chanjo hii, ulionyesha kwamba visa hivi vilipungua.

Kwa mfano, nchini Australia na Denmark ambapo chanjo dhidi ya virusi vya HPV ilizinduliwa mapema na mradi huo kufikia watu wengi, kulikuwa na upungufu wa asilimia 80% ya matatizo ya njia ya uzazi yanayotokana na virusi hivi; shida za kiafya ambazo zina uwezekano mkubwa wa kusababisha kansa ya lango la uzazi, endapo hazitatibiwa.

Pengine unajiuliza kwa nini chanjo hii haitolewi kwa wavulana katika mataifa mengi? Kulingana na ripoti hii, madhumuni ni kuzuia kansa ya lango la uzazi. Kulingana na WHO ni muhimu na matumizi thabiti ya rasilimali kwa chanjo hii kutolewa kwa wasichana kati ya miaka 9 na 14.

Aidha, ripoti hii inaonyesha kwamba chanjo hii ina manufaa kwa wanawake na wanaume ikiwa mataifa yana rasilimali za kutosha kuweza kumudu kutoa chanjo hii kwa vikundi hivi vyote.

“Basi kwa nini chanjo ya HPV inatolewa bila malipo kwa kikundi hususan cha wasichana?” auliza mwanaharakati, Emily.

Kulingana na WHO, chanjo hii inapaswa kutolewa kwa wasichana kati ya miaka 9 na 14. “Kuna baadhi ya nchi zinazofuata pendekezo hili na kutoa chanjo kwa wasichana walio katika mabano haya kiumri bila malipo. Kuna mataifa mengine ambayo huongeza na kutoa chanjo kwa wavulana na kwa vijana kufikia miaka 26. Katika nchi zingine, chanjo hii yaweza kutolewa kwa malipo ikiwa wahusika hawahusishwi katika mpango wa chanjo bila malipo,” inasema.

Ulinzi

Japo hakuna uhakika kuhusu kipindi ambacho chanjo hii husalia mwilini, ushahidi mpya unaonyesha kwamba watu waliopewa chanjo hii zaidi ya miaka 10 iliyopita, bado wanapata ulinzi thabiti dhidi ya aina ya virusi vya HPV katika chanjo iliyotumika, hivyo bado wana ulinzi wa kutosha unaowazuia kutokana na vidonda katika lango la uzazi, vile vile vidutu vya sehemu nyeti, na maradhi mengine yanayotokana na aina hizi za virusi vya HPV.

Hakuna ishara kwamba ulinzi huu unapungua miongoni mwa watu waliopewa chanjo na wataalamu wengi wanaamini kwamba chanjo hii itaonyesha uthabiti wake katika kipindi cha miongo kadha ijayo.

Na tofauti na dhana kwamba chanjo hii inaathiri uwezo wa kushika mimba, ripoti hii inasisitiza kwamba chanjo hii inatoa ulinzi kutokana na tatizo hili la uzazi.

Chanjo hii inalinda uwezo wa kushika mimba, kwa kuzuia vidonda vinavyochipuka kwenye lango la uzazi, na ambavyo baadaye husababisha kansa ya lango la uzazi.

Lakini licha ya haya, bado wanawake watakaopata chanjo hii bado watahitajika kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kutambua uwepo wa kansa hii.

“Chanjo hii inalinda dhidi ya aina fulani za virusi vya HPV vinavyosababisha asilimia 71-90% ya kansa ya lango la uzazi, lakini haiwezi kuzuia uwezekano wote wa kupata maradhi haya. Pia, hailindi wanawake kutokana na aina ya virusi vya HPV ambazo tayari walikuwa wameambukizwa kabla ya kupewa chanjo hii,” ripoti hii inasema.