SHINA LA UHAI: Huduma duni na gharama ‘zapofusha’ wengi
Na LEONARD ONYANGO
MACHO yake yalipoanza kutoa machozi, Joseph Mirerea alidhani kwamba tatizo hilo lilisababishwa na upepo mkali ambao huvuma mara kwa mara katika eneo la Lanet, Kaunti ya Nakuru.
Hata baada ya kununua miwani ya kujikinga na upepo, macho yake yaliendelea kutoa machozi, hali iliyomfanya kushuku kwamba yalikuwa na shida iliyohitaji matibabu ya dharura.
“Nilipoenda hospitalini, niliambiwa kuwa mishipa fulani kwenye macho yangu ilikuwa imelegea kutokana na makali ya baridi ambayo hushuhudiwa kati ya miezi ya Mei na Julai. Nilipewa miwani spesheli ya kunikinga na upepo na sasa ninaendelea vyema,” anasema.
Bw Mirerea alikuwa na bahati kwani Nakuru ni miongoni mwa miji iliyo na idadi kubwa ya wataalamu wa macho.
Takwimu zinaonyesha kuwa wataalamu wengi wa macho wanapatikana katika miji ya Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nakuru na Eldoret.
Esther Wambui, 68, ambaye ni mkaazi wa eneo la Mau, Kaunti ya Narok, anasema kuwa juhudi zake za kupata matibabu ya macho ziligonga mwamba baada ya kukosa fedha ambazo zingemwezesha kufanyiwa upasuaji.
Ajuza huyo sasa anaomba serikali kuingilia kati kwa kuhakikisha kuwa wazee wanapata huduma za bure za matibabu ya macho.
Watu hulipa kati ya Sh100 na Sh200 kupimwa macho katika hospitali za umma na kati ya Sh2,000 na Sh5,000 kwenye hospitali za kibinafsi – hivyo kufanya wengi kukosa matibabu ya mapema kutokana na gharama ya juu.
Wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa kuhusu Afya ya Macho mwaka huu, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alikiri kuwa ni asilimia 20 pekee ya watu walio na matatizo ya macho wanaweza kumudu gharama ya matibabu kwenye hospitali za umma na hospitali za kibinafsi.
Asilimia 80 hungojea huduma kutoka kwa wasamaria wema au hulazimika kuishi na matatizo ya macho kwa muda mrefu na kujiweka kwenye hatari ya kupofuka macho.
Kulingana na waziri Kagwe, sasa kuna takribani Wakenya 250,000 waliopofukia ukubwani baada ya kukosa huduma za mapema za macho.
Wakenya wengine milioni 7.5 wanahitaji matibabu ya haraka ya macho, kwa mujibu wa takwimu za wizara ya Afya.
Hiyo inamaanisha kuwa watu 15 kati ya 100 wana matatizo ya macho humu nchini.
Ripoti ya Hali ya Uchumi ya 2020 iliyotolewa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS), inaonyesha kuwa Wakenya 1,013,862 walienda katika hospitali za umma kutafuta huduma za macho mwaka 2019.
Idadi yaongezeka
Takwimu hizo za KNBS zinaonyesha kuwa idadi ya watu wanaofika katika hospitali za umma kutafuta huduma za matibabu inaongezeka kila mwaka.
Jumla ya watu 656,451 na 939,572 walienda kutafuta huduma za matibabu ya macho mnamo 2017 na 2018 mtawalia.
Bw Kagwe anasema kuwa hivi karibuni serikali itazindua mpango wake unaolenga kuboresha huduma za macho kati ya 2020 na 2025.
Mpango huo unapendekeza kuwa serikali inahitaji kuwekeza Sh22 bilioni ili kuboresha afya ya macho ndani ya miaka mitano ijayo.
Tatizo la kuharibika kwa lenzi ya jicho, maarufu ‘mtoto wa jicho’ au cataract, ndilo huchangia kiasi kikubwa cha visa vya watu kupofuka nchini Kenya.
Kulingana na Dkt Paul Nyalo, daktari wa macho, ‘mtoto wa jicho’ (cataract) hutokea jicho linaposhindwa kupitisha mwangaza wa kutosha.”
“Ugonjwa wa cataract husababishwa na kujazana kwa aina fulani ya protini ndani ya jicho. Mara nyingi tatizo hilo huwakumba zaidi wazee,” anasema Dkt Nyalo.
“Tatizo hilo pia linaweza kutokea baada ya jicho kupata majeraha ya aina fulani kama vile kufanyiwa upasuaji. Baadhi ya watoto huzaliwa na ‘mtoto wa jicho’ na wanaweza kupofuka macho iwapo hawatapata matibabu ya haraka,” anaeleza.
Dalili zake ni ugumu wa kuona vitu kwenye maeneo yaliyo na mwangaza hafifu au gizani na macho hutatizika yanapotazama vitu vyenye rangi.
Matatizo mengine ya macho yanayosababisha upofu humu nchini ni trachoma, glaucoma, kushindwa kuona vitu vilivyo mbali au karibu na maradhi ya macho utotoni.
Ugonjwa wa trachoma husababishwa na bakteria ambao hufanya macho kuwa na maumivu wakati wa kupepesa.
Ugonjwa huu umeshika kasi katika mazingira machafu na yaliyo na uhaba wa maji.
Watu wanaweza kuambukizwa maradhi hayo kwa kushikana mikono au kutumia shuka, nguo na malazi pamoja na mwathiriwa.
Glaucoma au ugonjwa wa presha ya macho husababishwa na kuharibika kwa mishipa inayowezesha jicho kuona vizuri.
Mishipa hiyo huharibika kutokana na kuongezeka kwa presha ndani ya jicho na mara nyingi tatizo hili huathiri wazee wa zaidi ya umri wa miaka 60.
Kulingana na wizara ya Afya, wazee, haswa katika maeneo ya vijijini humu nchini ndio hupatwa na maradhi ya macho kwa sababu ya kukosa huduma za matibabu.
“Kati ya Wakenya milioni 7.5 wanaohitaji huduma za matibabu ni asilimia 20 pekee wamekuwa wakipata huduma hizo. Ubora wa matibabu wa macho pia uko mashakani,” anasema waziri Kagwe.
Dkt Ken Tanui, tabibu wa macho wa Hi-Tech Opticians iliyoko mjini Nakuru anasema, maradhi ya kisukari yanaweza kusababisha matatizo ya macho endapo mtu hatachunguzwa mapema.
“Kiwango cha juu cha sukari huharibu sehemu ya nyuma ya jicho ambayo huwezesha watu kuona vitu, maarufu retina.
Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watu wanaougua maradhi ya kisukari humu nchini inaongezeka kila uchao. Mtu mmoja kati ya 17 anaugua maradhi ya kisukari humu nchini.
Waziri Kagwe ameonya kuwa upofu unaosababishwa na ugonjwa wa kisukari huenda ukaathiri idadi kubwa zaidi ya Wakenya endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kukabiliana na maradhi hayo.
Dkt Tanui anawashauri watu kupata uchunguzi wa kimatibabu mara kwa mara kwani wakati mwingine, huwa sio matatizo ya macho ila ni shinikizo la damu au maradhi ya kisukari.
Anasema matatizo ya macho miongoni mwa wazee yanaweza kusababishwa na mambo mengi kama vile uzee, shinikizo la damu katika retina, ajali kati ya mambo mengineyo.
Alisema kuwa idadi kubwa ya watu wanaokuja kutafuta huduma za matibabu katika Kaunti ya Nakuru ni wale walio na matatizo ya kutoona mbali.
Dkt Tanui anasema kuwa moshi pia unaweza kusababisha matatizo ya macho.
“Mgonjwa anapokuja akiwa na matatizo ya macho, huwa pia tunampima kubaini ikiwa ana kisukari au shinikizo la damu. Iwapo anapatikana na matatizo hayo, huwa tunamshauri atibiwe kwanza ndipo aendelee na matibabu ya macho,” akasema.
Anasema mgonjwa wa kisukari na shinikizo la damu wanahitaji kupimwa macho angalau mara moja kwa mwaka ili kuthibitisha kwamba macho yao hayajaathiriwa.
Watu walio na matatizo ya kutoona mbali pia wanafaa kupimwa angalau mara moja kwa mwaka.
Watoto wanaozaliwa chini ya wiki 32 wakiwa na uzani wa chini ya kilo 1.5 wanafaa kufanyiwa vipimo vya macho ndani ya wiki nne baada ya kuzaliwa.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), watu zaidi ya 2.2 bilioni wana matatizo ya macho kote duniani.