SHINA LA UHAI: Kidonda cha dhuluma za kimapenzi huacha makovu sugu
Na PAULINE ONGAJI
UNAPOMTAZAMA ni rahisi kutambua uchungu unaomkumba, hali ambayo inajitokeza kupitia hofu machoni mwake anapojaribu kuzungumzia yaliyomkumba miezi kadhaa iliyopita, huku machozi yakimlengalenga.
Ni hali ambayo Zuhura, 15, (sio jina lake halisi) amekuwa akikumbana nayo tangu anajisiwe mwezi Mei.
Masaibu yake yalianza Mei 4, 2020, baada ya jirani yao ambaye alikuwa akimfahamu vyema kusemekana kumshawishi kuingia chumbani kwake kisha kumtendea kitendo hicho cha unyama.
Baadaye alipopelekwa hospitalini, alifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na kupewa dawa za kuzuia mimba na virusi vya HIV, kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Lakini licha ya kuwa huenda anaonekana buheri wa afya, ni tukio ambalo limemwachia makovu sio tu ya kimwili, bali pia kiakili.
Kwanza kabisa amelazimika kutorokea kwa shangaziye sio tu ili kuepuka hofu ya kumbukumbu mbovu alizonazo kuhusu nyumbani kwao, bali pia usalama wake hasa ikizingatiwa kwamba mshukiwa ameachiliwa kwa dhamana huku kesi ikiendelea mahakamani.
“Amekuwa na hofu sana kiasi kwamba hata mimi mwenyewe nahofia kumtuma dukani, au hata kumruhusu aende nje,” asema Jamila (sio jina lake halisi), shangaziye aliyempa hifadhi eneo la Bombolulu.
Ni masaibu ambayo Miriam Kimemia, mkazi wa eneo la Ziwa la Ng’ombe, Bombolulu, pia anakumbuka kukumbana nayo miaka saba iliyopita baada ya mjukuwe kulawitiwa.
“Sio tu mjukuu wangu, bali familia yangu yote iliathirika kutokana na tukio hilo. Kwanza kabisa tuliingiwa na hofu kubwa kwani kesi ilipokuwa ikiendelea, tayari mshukiwa alikuwa ameachiliwa kwa dhamana,” aeleza.
Anasema kwamba kila mara walikuwa na hofu ya usalama wa mwathiriwa, suala lililowalazimu wabadilishe kabisa ratiba yao ya maisha. “Kwa mfano, tofauti na awali ambapo alikuwa akiandamana na wenzake kwenda shuleni, sasa ilitulazimu mimi na babu yake kumpeleka na kumchukua kila mara, huku tukiagiza walimu kamwe wasimruhusu mtu mwingine kumchukua,” aeleza.
Lakini mbali na athari hizo, Bi Kimemia pia anakumbuka majeraha ambayo mjukuwe aliachiwa baada ya kitendo hicho. “Kabla nigundue na kumpeleka hospitalini, alikuwa akitoa harufu mbaya katika tupu ya nyuma bali na kushindwa kuketi chini. Baada ya kumpeleka hospitalini, uchunguzi wa kimatibabu ulionyesha kwamba alikuwa na majeraha mabaya katika tupu ya nyuma,” aeleza.
Sasa ni miaka saba tangu tukio hilo ambapo Bi Kimemia anasfurahia mjukuwe kupona majeraha ya kimwili aliyokuwa nayo, huku aliyetekeleza unyama huo akiendelea kuhudumu kifungo cha maisha gerezani.
Lakini licha ya hayo, bibi huyu anasisitiza kwamba bado mtoto huyu anaendelea kukabiliwa na athari zinazotokana na dhuluma za aina hii. “Anaogopa watu na sio rahisi kwake kumuamini yeyote. Aidha, ni rahisi kwake kushtuliwa na jambo dogo,” aeleza.
Kulingana na ripoti ya Kenya Demographic and Health Survey-KDHIS, kati ya Januari na Julai mwaka huu, visa 421 vya dhuluma za kimapenzi vimeripotiwa katika Kaunti ya Kilifi, huku Kaunti ndogo ya Malindi ikinakili idadi kubwa zaidi ya visa 184.
Kulingana na Kenneth Miriti, mratibu wa afya ya uzazi ya vijana katika Kaunti ya Kilifi, ripoti hiyo inaonyesha kwamba huenda visa hivi vikawa vingi hata zaidi hasa ikizingatiwa kwamba vituo vya kuwasaidia waathiriwa wa dhuluma za aina hii viko katika hospitali za level 4 na 3.
Na japo takwimu hizi hazionyeshi wazi visa vya dhuluma za kimapenzi dhidi ya watoto, Bw Miriti anasisitiza kwamba ni vingi.
Kaunti hii ni mfano wa jinsi licha ya Kenya kupiga hatua katika vita dhidi ya dhuluma za kijinsia, tatizo hili bado limekita mizizi. Kinachosikitisha hata zaidi ni kwamba visa vingi haviripotiwi, huku waathiriwa wengi wa ubakaji na ulawiti wakiendela kuumia kimyakimya.
Hapa nchini, dhuluma za kimapenzi ni mojawapo ya hatari kuu ambazo zimeendelea kuongeza mzigo wa magonjwa, huku takwimu za kitaifa zikionyesha kwamba watoto wanaathirika pakubwa.
Aidha, takwimu hizi zinaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 90 ya waathiriwa hawa hawatafuti matibabu, ilhali zaidi ya nusu ya wanaosaka matibabu, hawakamilishi tiba kuambatana na ushauri wa daktari. Pia baadhi ya waathiriwa huenda hospitalini lakini hawaanzishiwi matibabu.
Kulingana na Dkt Ademola Oladije, Mwakilishi wa Hazina ya idadi ya watu ya Umoja wa Mataifa- UNFPA hapa nchini, licha ya visa hivi kuendelea kuongezeka, waathiriwa wengi wamehofia kabisa kujitokeza na kuzungumzia yaliyowakumba, suala ambalo limetatiza juhudi za kukabiliana na zimwi hili.
Upungufu
Dkt Patricia Owira kutoka shirika la International Center for Reproductive Health-Kenya, anasema kwamba upungufu wa rasilimali za kuhimili huduma za kimatibabu kwa waathiriwa huenda umechangia pakubwa.
“Kwa mfano, kuna baadhi ya mashirika yaliyojitolea kuwashughulikia waathiriwa wa dhuluma za kimapenzi, lakini mara nyingi yanakabiliwa na changamoto za kifedha,” aeleza.
Aidha, anasema kwamba umaskini umechangia pakubwa kimya cha jamii. “Kwa mfano, kuna baadhi ya watu wanoadhani kwamba ni gharama kwa mwathiriwa kupata matibabu baada ya kudhulumiwa. Kwa hivyo, badala ya kwenda hospitalini, wako tayari kupokea senti kidogo kutoka kwa waliotekeleza unyama huu kama hongo ya kuwanyamazisha,” asema.
Ni suala ambalo anaongeza kwamba limetatiza jitihada za kupata haki.
“Kumbuka kwamba, bila uchunguzi wa kimatibabu, ni vigumu kupata ushahidi wa kumfunga mshukiwa,” anaeleza.
Lakini mbali na masuala ya kisheria, kimya hiki kimeendelea kuwa hatari kwa waathiriwa. Kwa mfano, John Musau, Afisa wa Afya katika kituo cha afya cha Mtwapa, Kaunti ya Kilifi, anasema waathiriwa wengi wa dhuluma hizi wanaoletwa kituoni humo huwa na majeraha mabaya ya sehemu za siri, huku baadhi yao wakihitaji kufanyiwa upasuaji.
Pia kuna ambao huenda wakaonyesha ishara za maambukizi ya magonjwa hya zinaa kama vile kisonono, kaswende, chlamydia, au virusi vya HIV. “Kuripoti visa hivi kutamsaidia mwathiriwa kupokea huduma za kuzuia maradhi na hata mimba, ambapo endapo hatopokea matibabu, afya yake imo hatarini,” asema.
Aidha, licha ya majeraha ya kimwili, kulingana na Jarida la Journal of Pediatric Psychology, kuna hatari ya kukumbwa na majeraha mabaya ya kiakili.
Wataalamu wa kiafya wanahoji kwamba dhuluma ya kimapenzi hasa dhidi ya watoto imehusishwa na matatizo ya kiafya baadaye katika umri wa ukomavu. Kwa mujibu wa jarida hili, watu ambao wamewahi kukumbana na unyama huu utotoni, wamo katika hatari kubwa ya kupatwa na matatizo ya kiakili.
Kulingana na jarida hili, baadhi ya hatari zinazowakodolea macho waathiriwa watoto baadaye maishani ni pamoja na tatizo la Post-Traumatic Stress Disorder (PTSD), mfadhaiko na kuishiwa matumaini.
“Aidha, kuna mabadiliko ya kitabia kama vile kukumbwa na hasira, kutoamini watu wengine na hofu, ambapo mambo yakiwa mabaya hata zaidi, kuna hatari ya hisia za kutaka kujitoa uhai.
“Ndiposa tunasisitiza umuhimu wa ushauri nasaha kabla ya mwathiriwa kufikia kiwango kisichoweza kudhibitiwa,” asema Dkt Owira
Dkt Ademola anasema kwamba suala la dhuluma za kimapenzi halipaswi kupuuzwa kwani huenda likasababisha matatizo makubwa katika siku zijazo, hasa ikizingatiwa kwamba waathiriwa watalazimika kuishi na makovu haya daima.
Anasisitiza kwamba waathiriwa wanapaswa kufikia huduma kwa urahisi.
“Mojawapo ya mbinu za kuhakikisha hili ni kwa vituo vinavyotoa huduma hizi kuwa na mazingira salama kwa waathiriwa kutoa taarifa na kupokea matibabu, pasipo kuwa na hofu,” aeleza.
Dkt Ademola anasema kwamba umewadia wakati kwa jamii kuchukulia suala la dhuluma ya kimapenzi dhidi ya watoto kwa umakini. “Watu wanapaswa kutambua kwamba, mbali na majeraha ya kimwili, mwathiriwa pia yumo katika hatari ya kukumbwa na matatizo ya kiakili,” aeleza.