Makala

SHINA LA UHAI: Kupiga mpira kwa kichwa hatari kwa ubongo wa wanawake

December 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 5

Na LEONARD ONYANGO

JE, upigaji mpira kwa kutumia kichwa mara kwa mara miongoni mwa akina dada wanaosakata kabumbu huathiri ubongo?

Baadhi ya watafiti sasa wanahusisha wanawake kupiga mpira kwa kichwa na maradhi ya kusahau (dementia).

Watafiti wanasema wanawake wako katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa Chronic Traumatic Encephalopathy (CTE) ambao husababishwa na kugongwa gongwa kwa kichwa.

Dalili za maradhi hayo ni kubadilika kwa tabia, kukasirika kiholela bila sababu na kushindwa kufikiri. Wanasema madhara ya ugonjwa huo hujitokeza miaka mingi baadaye.

Chuo Kikuu cha Boston kimeanzisha uchunguzi kubaini jinsi wanasoka wa kike wanavyoathirika wanapopiga mpira kwa kichwa.

Utafiti huo unahusisha wanawake 20 wa umri wa miaka 40 na zaidi ambao wamestaafu kutoka kwenye soka ambao wamewahi kuchezea timu ya taifa ya Amerika na kushiriki mashindano ya Olimpiki nchini humo.

Washiriki watafanyiwa vipimo mbalimbali katika idara ya maradhi ya CTE ya Chuo Kikuu cha Boston.

Matokeo ya utafiti huo yanatarajiwa kutolewa mwaka 2020.

Utafiti uliofanywa na Chama cha Madaktari wa Ubongo cha Amerika Kaskazini ulionyesha kuwa kupiga mpira kwa kichwa kuna madhara kwa wanasoka wa kike ikilinganishwa na wenzao wa kiume.

Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Radiology, ulionyesha kuwa mwanamke anapopiga mpira kwa kichwa mara kwa mara huathiri sehemu nane za ubongo huku wenzao wa kiume wakiathiri sehemu tatu tu.

Jarida la Afya na Jamii lilikutana na mchezaji Diana Kosgei (pichani), mchezaji wa kiungo cha kati kutoka timu ya wanawake ya Nakuru West Queens, inayoshiriki ligi ya akina dada nchini, Kenya Women Premier League (KWPL).

Diana anasema alianza kusakata kabumbu akiwa shule ya msingi, uwezo wake kuzolea timu kadhaa mataji umemtengenezea jina ndani na nje ya nchi ya Kenya.

Kulingana naye, raha ya kusakata kabumbu ni kufurahisha mashabiki kwa kufunga magoli mengi, ambapo ufundi wa aina yake unahitajika wakati wa kutafuta mabao.

“Kichwa, kifua na miguu ni viungo muhimu wakati wa kutuliza na kuelekeza mpira wavuni, ujuzi ambao kila mchezaji ni lazima ajihami nao, andapo analenga kufika mbali,” akasema.

Alieleza kuwa mchezaji anaweza akausimamisha mpira kwa kutumia kipaji cha uso (mbele ya kichwa),kisha akautuliza kwenye kifua na kuufyatua kwa miguu.

Hata hivyo anaungama kuwa sio jambo la kawaida kwa wanawake kupiga mpira kupitia kichwa, isipokuwa wachache tu wenye ujasiri wasiojali maumivu makali.

“Ni sehemu ya juu katikati ya kichwa ambayo hupata maumivu makali pindi mpira unapotua juu yake, na kocha wetu amekuwa akitueleza kuepukana na mipira inayotua sehemu hii,” akasema.

Ni kwa sababu hiyo wachezaji wengi wa kike wamekuwa wakikwepa mpira kuangukia katika sehemu hii ya kichwa, ambapo fuvu hukutana na kipaji cha uso.

Anasema mara ya kwanza kupiga mpira kwa kichwa, nusra azirai kwa sababu hakuwa amezoea kufanya hivyo. Hatimaye alijifundisha kuvumilia maumivu hadi alipokuja kuzoea na siku hizi ni desturi yake kufunga magoli kupitia kichwa.

Mpira unaokuja kwa kasi unaweza kumfanya mchezaji akapata kisunzi na kuathiri macho kwa muda, kabla ya kurejelea hali ya kawaida. Jambo hili ni la kawaida kwa wachezaji ambao bado ni chipukizi.

Inasadikika kuwa kemikali za neva juu ya kichwa hupitiza ishara kwa haraka hadi kwenye ubongo pindi kitu chochote kinapotua juu ya kichwa.

Diana aliongezea kuwa upigaji mpira kupitia kichwa ni ujuzi ambao umekopwa kutoka kwa timu za wanaume, akiamini kuwa wavulana wengi waweza kustahimili dhoruba kali kwa sababu ya ukakamavu.

Lakini anawashauri wachezaji wenzake wasizoee kupiga mpira kwa kichwa na badala yake wacheze kwa kifua na miguu yao.

Anawapongeza kinadada wanaotumia vichwa kupiga mpira kwa sababu ni njia mojawapo ya kuonyesha kuwa si waoga na wako tayari kutafutia timu zao ushindi kwa njia yoyote.

Wazo ambalo mkufunzi wake Peterson Esitoko aliunga mkono akisema kuwa yeye amekuwa akiwafundisha wachezaji kutumia sehemu zote za mwili wakati wa kusakata kabumbu.

Kichwa, Kifua na miguu ni mambo ya kimsingi ambayo yanahitajika ili kunogesha ladha ya kucheza mpira.

Anasema kuwa endapo mchezaji alikubali kucheza mpira, ni lazima ajumuishe sehemu hizi za mwili ili kuleta matokeo mazuri yanayohitajika. Ndio maana mazoezi ya kila siku za wiki yanalenga kuimarisha kila sehemu ya mwili kabla ya kushiriki ratiba ya michuano kila wikendi.

Mbali na soka, kuna michezo tele inayoaminika kuwa na madhara kwa afya ya ubongo.

Kulingana na tovuti ya Sport Boxing, baadhi ya wanadondi wanaopigana kitaaluma katika kiwango cha juu, wamekuwa wakihusishwa na matatizo mengi ya ubongo yanayotokana na kugongwa masumbwi mara kwa mara.

Wanasema kuwa endapo mpiganaji atapigwa katika kipaji cha uso, sehemu ya nyuma ya ubongo hutikisika pamoja na hata fuvu kupata nyufa.

Wakati mwingine mpiganaji anaweza akapoteza fahamu ama akaanza kutokwa na damu katika pua kutokana na dhoruba kali ya makonde.

Wapiganaji wengi wa ndondi hustaafu wakiwa na matatizo makubwa ya ubongo na wakati mwingine macho, kwa mujibu wa tovuti hiyo.

“Glavu za kupigana husababisha madhara makubwa katika ubongo ikilinganishwa na wapiganaji wanaotumia mikono yao kupigana,” unaelezea.

Matatizo ya ubongo hutokea kulingana na sehemu ambayo mhusika amepigwa.

Kwa mfano mpiganaji anapopigwa katika sehemu ya mbele ya ubongo, madhara huwa sio mabaya ikilinganishwa na utosini au kisogoni.

Mchezo wa raga pia umetajwa kuwa hatari si kwa ubongo tu bali kwa viungo vinginevyo vya mwili.

Baadhi yao wamekuwa wakikingama wenzao kwa kutumia vichwa na hata kufunga magoli kwa kujirusha na kutua juu ya ardhi ngumu.

Kwa kawaida, mchezo wa raga huwa na watu wa miraba minne na unahusisha kusukumana na kugongana mara kwa mara uwanjani.

Mwaka wa 2012, tume ya raga duniani ilianzisha kituo cha kufanyia uchunguzi madhara yanayoweza kusababishwa na mchezo wa raga uliofahamika kama Head Injury Assesment (HIA).

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Glasgow mnamo 2016 ulibaini kuwa ni wachezaji wachache tu wa raga ambao hupata matatizo ya ubongo baada ya kustaafu.

Watafiti hao walichunguza wachezaji wastaafu 52 wa raga wa kiume. Aidha walilenga kufahamu madhara ya mchezo wa raga kwa afya ya ubongo.

Watafiti hao walibaini kuwa wengi wao walikuwa na matatizo ‘madogo’ ya ubongo kuhusiana na kukumbuka mambo.

“Utafiti ulibaini kuwa wachezaji hao walikuwa na ugumu wa kujifunza maneno mapya na kukumbuka mambo,” wakasema watafiti hao.

Lakini tafiti ambazo zimewahi kufanywa nchini Amerika, zinaonyesha kuwa michezo ya masumbwi, raga na mingineyo ina madhara makubwa kwa wachezaji wa kike ikilinganishwa na wenzao wa kiume.

Kulingana na Dkt Douglas Smith wa chuo cha Pennsylvania, seli za ubongo wa wanawake zinazojulikana kama axons ni nyembamba mno ikilinganishwa na seli za wanaume.

Seli hizi za wanaume huwa nzito na ‘zimesukana’ hivyo huwa vigumu kuharibika kichwa kinapogongwa.

“Kwa sababu seli za axons za ubongo wa wawanawake ni nyembamba mno na dhaifu, huharibika kichwa kinapogongwa na kitu kigumu,” Dkt Smith akaambia mtandao wa telegraph.co.uk .

Kulingana na Dkt Smith, ubongo wa mwanaume una uwezekano wa kupona baada ya kugongwa ilhali seli za ubongo wa mwanamke zinaweza kuharibika.

Mchezo wa kuendesha baiskeli pia umelaumiwa kwa kuwasababishia wanawake maumivu tele.

Madhara katika mashindano ya baiskeli miongoni mwa wanawake yalizua mjadala mkali mapema mwaka huu baada ya mshindi mara mbili wa Olimpiki wa Amerika Kelly Catlin kujitoa uhai mnamo Machi.

Catlin alijitoa uhai miezi mitatu baada ya kichwa chake kugonga chini na kupata maumivu ya kichwa Desemba, mwaka jana.

Familia yake iliruhusu watafiti kuchukua ubongo wake kufanya uchunguzi ili kubaini ikiwa mwanamichezo huyo alijitoa uhai kutokana na matatizo ya ubongo.

Chama cha Mchezo wa Vikapu nchini Amerika (NBA) kimeweka kanuni ya kuhakikisha kuwa timu zinajumuisha daktari wa afya ya ubongo miongoni mwa wafanyakazi wake.

Mamlaka ya Mchezo wa Kriketi nchini Australia (CA) huwataka wachezaji angalau kupimwa afya ya ubongo wao mara moja kwa mwezi.Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) linasema kuwa wanamichezo ni sawa na watu wengine katika jamii hivyo wanaweza kupatwa na matatizo ya akili.

 

Habari zaidi na Richard Maosi