Makala

SHINA LA UHAI: Pombe sumu ya wanawake

January 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na LEONARD ONYANGO

“MABAYA yanaponikumba, ninakunywa pombe ili nisahau. Ninapopata mazuri ninalewa ili kusherekea. Ikiwa hakutatokea lolote, nabugia pombe ili kitu kitokee.”

Hiyo ni nukuu kutoka katika kitabu Women chake Charles Bukowski akijaribu kuelezea kwa nini idadi ya watu wanaobugia mvinyo inaongezeka kila uchao.

Pombe inachukuliwa kuwa kama burudani hivyo imekuwa kivutio kwa wengi. Zamani, idadi kubwa ya wabugiaji wa pombe walikuwa wanaume. Lakini sasa ukizuru eneo moja la burudani hadi jingine mijini, utapata karibu idadi sawa ya wanaume na wanawake.

Utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (Nacada) mnamo 2011 ulionyesha kuwa idadi ya wanawake wanaobugia mvinyo inaongezeka kwa kasi.

Ripoti hiyo ilionyesha kuwa idadi kubwa ya wanawake wanaokunywa pombe wako chini ya umri wa miaka 35.

Kati ya vijana wa kati ya umri wa miaka 25 na 34 wanaobugia pombe, asilimia 15 ni wanawake na asilimia 79 ni wanaume, kulingana na ripoti hiyo ya Nacada.

Ripoti ya Wizara ya Afya iliyotolewa 2016 ilionyesha kuwa wanawake wa kati ya umri wa miaka 45 na 49 ndio wanaolewa chakari ikilinganishwa na wenzao walio chini ya umri wa miaka 40.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwanamke mmoja kati ya 10 anakunywa pombe jijini Nairobi.

Kuna uwezekano maradufu kwa wasichana na wanawake wanaoishi mijini kunywa pombe ikilinganishwa na wenzao wa vijijini.

Ripoti iliyotolewa na Nacada mnamo 2018 ilionyesha kuwa jumla ya Wakenya milioni 2.8 wanakabiliwa na matatizo ya kiafya yanayohusiana na uraibu wa pombe.

Jiji la Nairobi linaongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu wanaosumbuliwa na matatizo ya kiafya yanayohusiana na unywaji wa pombe kwa asilimia 18.4. Eneo la Magharibi linafuatia kwa asilimia 13 huku ukanda wa Mashariki ukifunga jedwali la maeneo matatu yaliyoathiriwa zaidi na pombe kwa asilimia 10.

Wataalamu wa afya wanasema, pombe huathiri afya ya wanawake zaidi ikilinganishwa na wanaume.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kudhibiti Unywaji wa Pombe nchini Amerika (NIAAA) unaonyesha kuwa pombe inadhuru zaidi afya ya wanawake ikilinganishwa na wanaume.

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo yaliyotolewa wiki iliyopita, pombe pia inasababisha vifo vingi zaidi miongoni mwa wanawake ikilinganishwa na wanaume.

Watafiti ambao wamechapisha kazi yao katika jarida la Alcoholism: Clinical and Experimental Research, walichunguza vyeti vya kifo vya watu wa kuanzia umri wa miaka 16 waliofariki dunia kati ya 1999 na 2017 nchini Amerika.

Watafiti waligundua kwamba watu milioni moja walifariki kutokana na maradhi yanayosababishwa na pombe.

Taasisi hiyo ilibaini kwamba idadi ya wanawake wanaofariki kutokana na maradhi yanayosababishwa na pombe ilikuwa ya juu zaidi na iliongezeka kila mwaka.

Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa utafiti huo ulionyesha kuwa idadi ya wanawake wanaolewa chakari iliongezeka kwa kasi.

Watafiti wanasema kuwa kuongezeka kwa idadi ya wanawake wanaokunywa pombe kulichangiwa na matangazo yanayopeperushwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

“Miaka ya zamani, ni wanawake wachache waliokunywa pombe. Lakini kampuni za kutengeneza pombe ziliamua kulenga wanawake katika matangazo yao, zilifanikiwa kuwashawishi na sasa kuna idadi kubwa zaidi ya wanawake wanaobugia pombe na wengi wao wamehatarisha afya zao,” Dkt Keith Humphreys wa Chuo Kikuu cha Stanford, alinukuliwa na Yahoo Lifestyle akisema.

Athari kwa wanawake

Kituo cha Kutafiti na Kuzuia Maradhi (CDC) kinasema kuwa pombe huathiri mwili kwa kutegemea jinsia. Wanawake wako katika hatari kubwa zaidi.

“Kutokana na maumbile yao, pombe huchukua muda mrefu kuisha katika mwili wa mwanamke tofauti na wanaume,” kinasema.

• Ini: Kwa mujibu wa CDC, wanawake wako katika hatari kubwa ya kupatwa na maradhi ya ini (Cirrhosis) yanayosababishwa na pombe kuliko wanaume.

• Ubongo: Pombe huathiri ubongo wa wanawake ndani ya muda mfupi zaidi ikilinganishwa na wanaume, kwa mujibu wa wataalamu wa afya.

“Pombe husababisha ubongo ‘kukonda’ na kumfanya mwathiriwa kuwa na tatizo la kusahau mambo kwa urahisi. Tatizo hili huwa kubwa zaidi miongoni mwa wanawake,” inasema taasisi ya CDC.

Mishipa ya moyo: Taasisi hiyo pia inaelezea kwamba pombe huharibu mishipa ya moyo wa wanawake kwa urahisi ikilinganishwa na wanaume.

Dkt Humphreys anaelezea kwamba pombe huathiri wanawake zaidi kwa sababu wengi wao wana uzani mdogo. “Pombe huwa kwenye sehemu yenye majimaji mwilini. Ukweli ni kwamba wanawake wana kiasi kidogo cha maji mwilini ikilinganishwa na wenzao wa kiume. Hii inamaanisha kwamba mwanamke na mwanaume wa uzani sawa wanapokunywa pombe kiasi sawa, damu ya mwanamke hukolea pombe zaidi kutokana na kiwango kidogo cha maji. Hili humweka katika hatari zaidi ya kupata matatizo ya kiafya,” anaelezea.

Madaktari pia wanasema wanawake wana viini vichache vya ‘alcohol dehydrogenase’ (ADH) ambavyo husaidia mwili ‘kusaga’ pombe na hatimaye kuitoa nje ya mwili.

• Uraibu: “Wanawake pia huwa waraibu wa pombe kwa urahisi kuliko wanaume. Hii ina maana kuwa ni vigumu kwa mwanamke kuachana na pombe baada ya kuitumia kwa muda mfupi,” anasema Profesa Celeste Robb-Nicholson wa Chuo Kikuu cha Harvard.

• Utasa: Pombe kupindukia hutatiza mfumo wa hedhi hivyo kuwafanya wanawake wanaobugia vileo kushindwa kupata watoto.

• Kansa: Kwa mujibu wa CDC, pombe pia husababisha kansa ya koo, mdomo na matiti miongoni mwa wanawake zaidi ikilinganishwa na wenzao wa kiume.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya 2018 inaonyesha kuwa asilimia 40 ya Wakenya hunywa bia, asimilia 21 hubugia whiski na waliosalia hunywa za kienyeji au kila aina ya mvinyo.

• Maradhi ya zinaa: Wanawake wanaobugia pombe kupindukia wako katika hatari ya kushiriki mapenzi bila kutumia kinga hivyo kujiweka katika hatari ya kuambukizwa maradhi ya zinaa kama vile virusi vya HIV, kulingana na WHO.

• Dhuluma za kimapenzi: Wanawake, haswa wanafunzi wa vyuoni, wanapolewa wanakuwa katika hatari ya kudhulumiwa kingono. Tafiti zinaonyesha kuwa mwanafunzi mmoja kati ya 20 wa vyuoni hudhulumiwa kimapenzi kutokana na ulevi.

Kulingana na WHO, watu milioni 3.3 hufariki kila mwaka kutokana na matumizi ya pombe kote duniani. Hiyo kwa kila watu 20 wanaokufa, mmoja huangamia kutokana na pombe.

Watu wazima bilioni 3.1 hawanywi pombe kote duniani.