SHINA LA UHAI: Upandikizaji figo bado changamoto kwa wagonjwa wengi nchini
Na PAULINE ONGAJI
ALIZALIWA akiwa na figo zote mbili lakini kulingana na madaktari, ni moja tu iliyokuwa ikifanya kazi.
Kufikia mwaka wa 2014, hali ilikuwa mbaya kwa Christine Wang’ombe, figo iliyokuwa ikifanya kazi iliposita pia.
Ni shida iliyomtatiza kwa mwaka mmoja na kumlazimisha kuanza kufanyiwa utaratibu wa dialisisi.
“Nilifanyiwa dialisisi kwa miezi mitatu kabla ya kubahatika kuwa mmojawapo wa wanufaishwa waliochaguliwa kufanyiwa upasuaji ili kupandikiza figo (Kidney transplant) bila malipo chini ya mradi wa hazina ya Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta,” anasema.
Hii ilikuwa baada ya pamoja na jamaa zake kadhaa kufanyiwa chunguzi mbalimbali kubaini ni yupi kati yao aliyefuzu kumgawia Bi Wang’ombe figo.
“Hatimaye nilibahatika kwani binamu yangu alifuzu kiafya kunipa figo, ambapo baadaye nilipandikizwa. Miezi sita baadaye, nilikuwa nishapona na kurejelea shughuli zangu za kawaida,” aeleza.
Sasa ni miaka sita tangu Bi Wang’ombe ambaye ni tabibu, afanyiwe utaratibu huo ambapo anasema kwamba ulibadilisha mwelekeo wa maisha yake kabisa.
“Bila shaka kama mtu ambaye amewahi kupandikizwa figo, lazima niendelee kutumia dawa. Lazima nihudumiwe kila wakati kwenye kliniki kwani nisipofuatilia matibabu, basi kuna hatari ya mwili kukataa figo hiyo mpya, kumaanisha kwamba haitanisadia,” afafanua.
Lakini licha ya hili, anasema kwamba hali yake kiafya iko sawa ikilinganishwa na wakati ambapo alikuwa akitegemea dialisisi.
“Japo lazima niendelee kwenda hospitalini kwa ukaguzi na matumizi ya dawa, maisha yangu ni ya kawaida sana kwani naweza kufanya shughuli zangu bila tatizo,” aeleza.
Bi Wang’ombe ni mmoja wa wagonjwa wachache wa figo wanaobahatika na utaratibu huu humu nchini kila mwaka.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani WHO, idadi ya watu wanaokumbwa na matatizo ya afya inaendelea kuongezeka huku maradhi yasiyosambazwa yakichangia pakubwa takwimu hizi.
Takwimu kutoka kwa chama cha madaktari wa figo nchini (Kenya Renal Association), zinaonyesha kwamba Wakenya milioni 4 wanaugua maradhi ya figo, na kufikia mwisho wa mwaka 2030, huenda idadi hii ikakaribia milioni tano.
Aidha uhalisia huu unathibitishwa na takwimu zinazoonyesha kwamba, idadi ya wagonjwa waliofanyiwa utaratibu wa dialisisi katika hospitali za umma na kibinafsi iliongezeka kutoka 300 mwaka wa 2006, hadi 2,400 miaka miwili iliyopita.
Isitoshe, ripoti zinaonyesha kwamba maradhi ya figo yanaorodheshwa ya sita kwa kuchangia idadi kubwa ya vifo sio tu humu nchini, bali ulimwenguni kote.
Kulingana na WHO, mbinu mwafaka ya kukabiliana na matatizo ya figo ni kuimarisha mtindo wa maisha.
Hata hivyo kwa kwa waathiriwa, wataalamu wanasema kwamba upandikizaji unawapa fursa ya kuishi maisha yao ya kawaida.
“Bila shaka dialisisi ni muhimu na imekuwa ikisaidia sana wagonjwa wa figo, lakini upandikizaji unamwezesha mgonjwa kurejelea hali yake ya kawaida kiafya,” asema Dkt Benjamin Wambugu, mtaalamu wa figo.
Dkt Wambugu anaongeza kwamba maisha ya mgonjwa anayefanyiwa dialisisi hutatizika kwani mbali na muda anaochukua kufanyiwa utaratibu huu, kuna masharti kuhusu mtindo wa maisha anayoishi hasa kuambatana na vyakula anavyopaswa kula.
Lakini licha ya ushahidi bayana kuhusu manufaa ya kupandikiza figo, utaratibu huu umeonekana kuwa changamoto kwa wagonjwa wengi.
Kulingana na WHO, katika fani ya kupandikiza ogani mwilini, figo ndio kiungo kinachohitajika zaidi ulimwenguni.
Miaka miwili iliyopita, shirika la Global Observatory on Donation and Transplantation lililonyesha kwamba asilimia 63 ya upandikizaji wa ogani zilikuwa za figo.
Hata hivyo, wagonjwa wa figo wamekuwa wakitatizika kutokana na uhaba wa ogani hii huku wengi wakilazimika kusubiri kwa muda mrefu.
Hapa nchini, sababu kuu ambayo imechangia wagonjwa wa figo kuendelea kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kufanyiwa upasuaji ni upungufu wa ogani hii.
John Gikonyo, mwakilishi wa chama cha wagonjwa wa figo nchini (RPSK) anasema kwamba licha ya kuhitajika mno hapa nchini, kuna vikwazo vingi kabla ya mhusika kupata kiungo hiki.
“Hapa nchini mara nyingi tunategemea mchango wa jamaa za mhusika, huku sheria ikisisitiza kwamba anayekupa ogani lazima awe jamaa ya mwathiriwa,” alalama.
Kulingana na Dkt John Ngigi, mkuu wa kitengo cha tiba ya figo katika Hospitali ya kitaifa ya Kenyatta, tatizo ni kwamba sio rahisi kupata jamaa ambaye yuko hiari kufanya hivyo.
“Na hata wakikubali kugawa figo, mara nyingi unapata kwamba hawafuzu kiafya. Tatizo laweza kuwa aina yao ya damu haiambatani na hata ikiwa inaambatana, mara nyingi matatizo ya figo hurithiwa kifamilia kumaanisha kwamba jamaa huyu hatofuzu kumgawia mwenzake ogani hii,” aeleza Dkt Ngigi.
Mbali na hayo, anasema kwamba katika enzi hizi ambapo magonjwa yasiyo ya kuambukizana yameenea, kinakuwa kibarua kumpata jamaa ya mwathiriwa aliyefuzu kiafya kutoa ogani hii.
Ni tatizo lililoshuhudiwa miongoni mwa waathiriwa waliokuwa wakifanyiwa uchunguzi wa kiafya majuzi, ili kufuzu kupandikizwa figo bila malipo mwaka ujao, chini ya mradi wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta.
Katika shughuli hiyo, kati ya waathiriwa 600 waliojitokeza pamoja na jamaa zao waliojitolea kuwagawia figo, ni 34 pekee waliofuzu kiafya kufanyiwa utaratibu huo.
“Sababu kuu ilikuwa kwamba miongoni mwa wengi waliojitokeza, aina ya damu yao haikuambatana, na kwa wale walioambatanishwa, hawakuwa salama kiafya kiwango cha kuruhusiwa kugawa figo,” aeleza Dkt Ngigi.
Kwa hivyo suluhisho ni nini?
Profesa Seth O. Mcligeyo, mtaalamu wa matibabu ya figo katika Chuo Kikuu cha Nairobi, anasema kwamba suluhisho ni kuongeza fursa za kuwezesha waathiriwa kupata figo wanapohitaji kufanyiwa upasuaji.
Mojawapo ya mbinu zinazopendekezwa na wataalamu ni kwa serikali kuidhinisha mpango wa watu kukubali ogani zao kutwaliwa baada ya kufariki.
Aidha, ikiwa mtu ana majeraha mabaya ya ubongo kiwango cha kutoamka tena na ogani zake ziko kwa hali nzuri, basi kwa idhini ya jamaa zake, zinaweza twaliwa kusaidia watu wengine wanaougua.
Mbali na hayo, wanasema, serikali pia inapaswa kurahisisha uwezekano wa wagonjwa kupokea ogani kutoka kwa watu wengine, mbali na jamaa zao.
Lakini kulegezwa kwa sheria hii kutafungua mwanya kwa ulanguzi wa viungo, tatizo ambalo limekumba ulimwengu mzima, huku takwimu zikionyesha kwamba 10% ya ogani zinazotumika kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji msaada, ni za ulanguzi.
Kumekuwa na ripoti za Wakenya kujaribu kuuza ogani zao mtandaoni ili kutatua matatizo yao ya kifedha.
Dkt Ngigi anasema sio haki kwa wagonjwa halali kunyimwa fursa ya kupona na kuishi maisha yao ya kawaida, kwa sababu ya wahalifu wachache.
“Lazima kuwe na njia ya kudhibiti shughuli hii. Kunahitajika sheria thabiti ya kuzuia uvunaji usio halali wa ogani, vile vile kudhibiti watu wanaoruhusiwa kugawa viungo hivi,” aongeza.