Makala

SHINA LA UHAI: Upasuaji wa titi ulivyomzidishia karaha maishani

October 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 5

Na PAULINE ONGAJI

MIAKA minne iliyopita, Rosemary Wangu Mwangi, 55, alikuwa anaishi maisha ya kawaida ambapo alikuwa akiendesha biashara yake eneo la Kirinyaga ya kusafirisha mboga kutoka sehemu za mashambani hadi jijini Nairobi.

Kwa upande mwingine, mumewe Harun Mwangi alikuwa akifanya kazi kama muuzaji bidhaa mjini Thika, ambapo pamoja wangeshughulikia mahitaji yao ya kifedha pasina tatizo.

Lakini kwa sasa taswira ni tofauti kabisa.

Unapokutana nao nyumbani kwao mtaani Mundia, mjini Thika, picha unayokumbana nayo ni ya unyonge; kuashiria mambo hayaendi kawaida. Hali yao imetokana na kuzorota kwa afya ya Bi Wangu ambaye kwa zaidi ya miaka mitatu sasa amelazimika kuishi na maumivu mengi.

Tumbo na miguu yake imefura. Kifua chake kimefungwa kwa bendeji kufunika donda kubwa kutokana na upasuaji sehemu hii.

Hawezi kuzungumza na hata kupumua kwake ni changamoto kwani kunaandamana na maumivu makali katika sehemu iliyoathirika.

Mara nyingi anaketi tu kwenye kiti asiweze kufanya mambo ambayo kwa wengine ni ya kawaida, kama vile kwenda msalani au kutembea. Majukumu haya yameachiwa mumewe, ambaye alilazimika kuacha kazi ili kumshughulikia.

Kwa hivyo mara nyingi anategemea nepi. Hawezi kuvaa rinda na hujifunga leso kiunoni na kuvalia shati kubwa ambalo huwa hafungi vifungo.

Hii ni mbali na kitita kikubwa cha pesa ambacho kimetumika kwa matibabu, hali ambayo imewaacha hoi.

Haya yote yalitokana na upasuaji kwenye titi la kulia; utaratibu ulionuiwa kukabiliana na maradhi ya kansa. Hata hivyo ni hatua wanayosema ilichukuliwa hata kabla ya thibitisho kamili kwamba alikuwa akiugua kansa.

Matatizo yake yalianza Februari 19, 2019 baada ya kwenda kufanyiwa uchunguzi kubaini iwapo alikuwa na maradhi ya kansa, kupitia kampeni ya kutoa huduma bila malipo katika kituo kimoja cha afya alikokuwa anaishi eneo la Kirinyaga.

“Awali nilikuwa nimegundua uvimbe mdogo kwenye titi hilo na nikadhani kwamba ilikuwa kansa, kwa hivyo niliposikia kuhusu kampeni hii, niliona haja ya kuenda kufanyiwa uchunguzi,” aeleza Bi Wangu.

Anaongeza: “Baada ya kukaguliwa na mmojawapo wa madaktari waliokuwa wakishughulika, nilitumwa katika hospitali moja ya kibinafsi kwa uchunguzi zaidi ambapo nilitarajiwa kurejesha matokeo katika hospitali hiyo.”

Hata hivyo baada ya kurejesha matokeo, alifahamishwa hayakuonyesha tatizo ni nini na hivyo akatumwa katika hospitali nyingine ya kibinafsi.

“Nakumbuka nikifanyiwa utaratibu fulani. Daktari aliingiza sindano kwenye titi langu la kulia na kuondoa majimaji hivi. Aliingiza sindano mara nne huku akifyonza majimaji fulani yaliyoonekana kama mafuta ya kupika. Mara ya tano aliondoa mchanganyiko wa majimaji mfano wa mafuta na damu, na mara ya sita akatoa mengine mfano wa maziwa,” aeleza.

Sampuli hizi zilipaswa kurejeshwa katika hospitali hiyo eneo la Karatina ili kuwawezesha madaktari kubaini iwapo alikuwa na kansa au la.

“Kwa hivyo baada ya majuma mawili nilirejea tena hospitalini ambapo walikuwa wameagizwa wanifanyie uchunguzi wa seli na tishu kwenye titi (biopsy). Daktari niliyekutana naye alikuwa mwanafunzi na nashuku kwamba hakuwa anajua alichokuwa anafanya. Badala ya kunifanyia uchunguzi huo, aliniweka kwenye orodha ya kufanyiwa upasuaji mdogo mara moja,” asema.

Ni hatua iliyomsababishia Bi Wangu wasiwasi. “Nakumbuka nikijawa na hofu na hasa mhudumu alipomuuliza daktari huyu iwapo angemudu kutekeleza shughuli hiyo bila usaidizi,” aeleza.

Anasema kwamba mambo yalianza kuonekana mabaya tokea mwanzo. “Alipokuwa anajaribu kunidunga sindano ya dawa ya kufa ganzi (anesthesia) nilibaini mara moja kuna tatizo kwani haikupenya na ile dawa ikamwagika. Hii ilifanyika mara tano kabla ya hatimaye kufaulu mara ya sita,” aongeza.

Usingizi ulimjia na akalala huku daktari akianza upasuaji. “Lakini baada ya dakika kadha, niligutushwa na uchungu mwingi sana. Tayari alikuwa amekata sehemu kadha na baadhi ya sehemu za titi langu zilikuwa wazi. Nakumbuka nikipiga nduru na hata kumsihi daktari asiendelee. Ni hapo ndipo alianza kurejesha nyama zilizokuwa wazi na kukimbia kuwaita madaktari wenzake,” aeleza.

Kilichomsababishia wasiwasi hata zaidi ni kwamba madaktari wengine walipokuja, walionekana kustaajabishwa. “Waliniuliza ikiwa nilikuwa nimefanyiwa uchunguzi wa tishu (biopsy) au kupigwa picha kabla ya kufanyiwa utaratibu huo,” asimulia.

Anasema kilichofuatia ni majibizano baina ya madaktari hao. “Ilibidi nifanyiwe upasuaji na daktari huyo huyo pengine kurekebisha kosa alilokuwa amefanya, utaratibu ambao pia haukufanywa vyema,” aeleza.

Baadaye, uchunguzi na matibabu kutoka vituo vingine vya kiafya ulionyesha kwamba upasuaji ulikuwa umefanywa vibaya.

Muda ulivyokuwa unasonga, eneo lililoathirika liligeuka na kuwa jeraha kubwa, likabadili rangi na kuwa jeusi, kisha kuanza kuoza, suala lililosababisha titi hilo kuondolewa baadaye.

Huu ukawa mwanzo wa ziara za kila mara hospitalini na chunguzi zaidi zililionyesha kwamba sehemu hii ilikuwa imeathiri titi lake la kushoto na lilikuwa katika hatari ya kukumbwa na maradhi ya kansa.

Kwa hivyo mwaka 2018 alifanyiwa awamu nane za matibabu ya tibakemia kwenye titi lake la kushoto. Lakini bado hajapata nafuu hasa sehemu ya kulia ambayo imesalia kuwa kidonda kikubwa huku akisubiri matokeo mengine kubaini iwapo ana kansa katika titi lake la kushoto.

Bw Mwangi anajutia hatua ya mkewe kwenda kufanyiwa uchunguzi wa kubaini ikiwa ana kansa. “Hata nashuku ikiwa kwa kweli alikuwa na kansa mara ya kwanza,” asema.

Kulingana na mwongozo wa kitaifa wa kutambua maradhi ya kansa (National Cancer Screening Guidelines) 2018, utaratibu wa mammography ndio mbinu inayopendekezwa kuchunguza iwapo mgonjwa anaugua kansa ya matiti.

Kwa kawaida huhusisha picha ya eksirei kwenye matiti. Picha hii yaweza kutumika kuonyesha uwepo wa kansa ya matiti, hasa kwa wanawake wasioonyesha dalili za maradhi haya. Aidha, uchunguzi huu waweza kutumika ikiwa mgonjwa ana uvimbe kwenye titi au anaonyesha ishara zingine za kansa.

Dkt Miriam Mutebi, daktari wa upasuaji wa kansa ya matiti katika hospitali ya Aga Khan, Nairobi, anasema kwamba utambuzi wa kimakosa wa kansa hutokea kwani mara nyingi maradhi haya hayakabiliwi na kikundi cha wataalamu wa kansa kwa pamoja.

“Hasa kikundi hiki hujumuisha madaktari wa kutibu kansa kupitia mnururisho, tibakemia, wapasuaji, wanapatholojia, wataalamu wa eksirei miongoni mwa wengine. Wataalam hawa wanaweza changanua hali ya mgonjwa na kutambua mbinu mwafaka ya matibabu inayomfaa,” asema.

Dkt Mutebi anasema hii husaidia madaktari kutambua kiwango cha maradhi husika kabla ya kufanya upasuaji, na hivyo inazuia kuchakura titi kabla ya kujua nini hasa kinachoendelea.

“Hata mimi kama daktari wa upasuaji wa kansa ya matiti, nimekutana na wagonjwa wengi ambao lazima wafanyiwe matibabu ya tibakemia kabla ya kufanyiwa upasuaji,” aeleza.

Kulingana na Dkt Mutebi, tatizo ni kwamba wataalamu wengi hufanya kazi kibinafsi, na hivyo unajipata ukitibiwa na unayekutana naye mara ya kwanza iwe unahitaji matibabu hayo au la.

Japo kukabili maradhi haya kama kikundi cha wataalamu wa kansa kwa pamoja ndio kiwango cha kimataifa, kuna vizingiti hasa katika mataifa yanayostawi, Kenya miongoni mwao.

“Hasa ukosefu wa fedha ndio tatizo kuu. Huduma za wataalamu hawa zinahitaji pesa na wagonjwa wengi hulazimika kulipia matibabu wenyewe,” aeleza.

Pia, kuna changamoto ya utaalamu wa wahudumu wa kiafya.

“Hii imekuwa changamoto ambayo bodi ya kimatibabu imekuwa ikijaribu kukabiliana nayo ili kuhakikisha kwamba wahudumu wanasajiliwa na bodi ya kimatibabu,” anasema.

Tatizo lingine asema Dkt Mutebi ni kwamba wagonjwa wengi hutaka kukabiliana na shida inayowakumba mara moja.

“Unaona uvimbe kwenye titi lako kisha unaingiwa na hofu na kuanza kujiandaa kufanyiwa upasuaji hata kabla ya kubaini tatizo lenyewe. Watu wanapaswa kujua kwamba kati ya vivimbe kumi vinavyopatikana kwenye titi, tisa havisababishi kansa,” aongeza.

Utambuzi wa kimakosa

Kulingana na Dkt Mutebi, woga na kukosa ufahamu kuhusu maradhi haya huwaweka wengi katika hatari ya utambuzi wa kimakosa wa maradhi haya.

“Wagonjwa wengi wa kansa ya matiti hawafahamu kwamba hakuna anayepaswa kuondoa chochote mwilini mwako kabla ya kupigwa picha au kufanyiwa uchunguzi wa tishu au seli (biopsy). Na ni kutokana na sababu hii ndiposa tunaona haja ya kuhamasisha wagonjwa ili kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu afya yao,” aeleza.

Kwa wagonjwa wengi wa kansa ya matiti, hofu hutokana na unyanyapaa vile vile vifo vinavyotokana na maradhi haya. Kulingana na utafiti wa GLOBOCAN 2018, kwa ujumla, kansa ya matiti ndiyo inayoongoza katika visa vipya vya maradhi haya nchini huku kukiwa na visa 5,985 vipya.

Kuhusu ikiwa wanawake wanapaswa kuhofia uchunguzi wa mapema wa kansa, Dkt Mutebi anasisitiza kwamba endapo kansa itatambulika mapema, basi si lazima upasuaji.

Kulingana na takwimu, wagonjwa wengi wa kansa ya matiti hujitokeza wakiwa wamechelewa, suala linaloongeza uwezekano wa vifo.

Utafiti uliofanywa mwaka 2018 katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) ulionyesha kwamba asilimia 7.4 ya wagonjwa waligundulika katika awamu ya kwanza, asilimia 33.7 katika awamu ya pili, asilimia 29.7 katika awamu ya tatu, na asilimia 21 katika awamu ya nne.

Dkt Mutebi anasema kutambulika mapema huimarisha uwezekeno wa matibabu kufaulu na mgonjwa kupona. Anasema kwamba utambuzi wa mapema hasa katika awamu ya kwanza, unamaanisha kwamba mgonjwa hatahitaji matibabu makali.

“Jaribu kufanyiwa uchunguzi wa matiti angalau mara moja kwa mwaka, na ikiwa una umri zaidi ya miaka 40, angalau fanyiwa uchunguzi wa mammogram baada ya mwaka mmoja au miwili,” ashauri.