• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
SHINA LA UHAI: Uraibu hatari kwa afya na mazingira pia

SHINA LA UHAI: Uraibu hatari kwa afya na mazingira pia

Na BENSON MATHEKA

JE, unafahamu kuwa sigara ina kemikali zaidi ya 4,000 zinazodhuru mwili na kwamba katika kila muda wa sekunde nne mtu mmoja hufariki kutokana na matumizi ya tumbako?

Tafiti zinaonyesha kuwa saba kati ya wavutaji sigara kumi huanza uraibu huu wakiwa wangali watoto na wanaoendelea kuvuta kwa muda mrefu hufupisha maisha yao kwa miaka 20 hadi 25.

Sababu ni kuwa sigara ina kemikali hatari ambazo zina uwezo wa kudhuru afya ya binadamu. Madhara yanayosababishwa na uvutaji sigara ni mengi na yamesambaa mwilini kote.

Na kufuatia kuongezeka kwa watu wanaokufa kutokana na uvutaji wa sigara na madhara yake, mapema Agosti 2019 Ibrahim Mohamud Ibrahim, mkazi wa Nairobi aliwasilisha ombi katika Mahakama Kuu akitaka uraibu huo upigwe marafuku nchini.

Katika ombi lake, Ibrahim analaumu serikali kwa kuruhusu ukuzaji, utengenezaji, usambazaji na matumizi ya tumbako nchini licha ya kubainika wazi ina madhara tele kwa afya. Anadai kwamba sheria ya kudhibiti matumizi ya tumbako haifai kwa sababu ni bidhaa hatari kwa afya ya umma.

Malalamishi ya Ibrahim yana uzito kwani kulingana na ripoti ya 2018 ya wizara ya Afya, Wakenya 15,000 waliaga dunia mwaka huo kutokana na maradhi yanayosababishwa na matumizi wa tumbako. Watu 5,000 miongoni mwao ni wanaoishi karibu na wavutaji sigara.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa watu zaidi ya 5.4 milioni huaga dunia kutokana na uvutaji sigara kila mwaka.

Shirika hilo linakadiria kuwa ifikapo 2040, idadi hii itapanda hadi 8.3 milioni.

Vipande vya sigara iliyokwisha kuvutwa. Picha/ Maktaba

Waziri wa Afya Sicily Kariuki anasema Kenya hutumia Sh2.9 bilioni kila mwaka kukabiliana na maradhi yanayotokana na matumizi ya tumbako.

“Nusu ya wanaotumia bidhaa za tumbako hufariki. Tafiti zinaonyesha kuwa tumbako huua watu wasiopungua milioni saba kila mwaka na milioni moja hufariki kutokana na athari za uvutaji sigara. Madhara ya uvutaji sigara ni mengi,” akasema waziri Kariuki alipozindua bodi ya kudhibiti matumizi ya tumbako.

Aliongeza: “Imegunduliwa kuwa uvutaji wa sigara huchangia ongezeko la saratani ya mapafu, koo na matatizo ya moyo.”

Takwimu za wizara hiyo zinaonyesha kuwa Wakenya zaidi ya 2.2 millioni hutumia bidhaa za tumbako kama vile sigara, kuber na shisha ambayo imepigwa marufuku nchini.

Ripoti ya WHO ya 2013 ilibaini kuwa zaidi ya sigara bilioni 6.4 zilivutwa nchini Kenya.

Mnamo 2015 idadi ya sigara zilizovutwa ilipanda hadi bilioni 8. Hiyo inamaanisha kwamba Wakenya wanavuta sigara milioni 22 kwa siku.

Watu 31,000 hufariki kila mwaka humu nchini kutokana na maradhi yanayotokana na uvutaji wa sigara. Takwimu za WHO pia zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya watu wanaovuta sigara wamejaribu kuacha lakini kati yao ni asilimia saba pekee ambao wamefanikiwa kuachana na uraibu huo.

David Ndambuki, mchuuzi mjini Machakos anakiri kwamba amekuwa akivuta sigara kwa miaka 40 na japo imeathiri afya yake, ameshindwa kuacha. “Imenisababishia matatizo ya kifua lakini nimeshindwa kabisa kuachana na uraibu huu,” asema.

Naye Duncan Mwakideu* (sio jina lake halisi), 52, ambaye amekuwa akivuta sigara kwa miaka 39, anasema kuacha uraibu huu sio vigumu ila shida ni ushawishi wa marafiki wavutaji sigara.

“Nilianza kuvuta sigara mwaka 1980 na sijapata madhara yoyote kiafya. Ninajua sigara inaathiri afya lakini ninahakikisha ninapata lishe bora. Huwa ninavuta sigara nikiwa na marafiki zangu tukiburudika lakini nikiwa peke yangu sio lazima nivute,” asema.

Anasema akiwa na marafiki, anaweza kuvuta hadi pakiti nzima na kuna siku havuti kabisa. “Uvutaji sigara kama uraibu wowote ule, unahitaji nidhamu kwa sababu unaweza kuathiri waliokaribu nawe,” asema.

Watafiti wanasema uraibu wa tumbako umekuwepo tangu mwaka 3500B.C kabla ya Yesu kuja hapa duniani.

Madhara

• Kung’oka nywele

Wanaoitumia hung’oka nywele mapema kufuatia kudhoofika kwa kingamwili na kudhuru mizizi ya nywele.

• Maradhi ya macho

Wavutaji sigara hupata magonjwa ya macho mara nyingi kuliko wasiovuta. Sehemu ya macho inayopitisha mwangaza inaweza kufunikwa kama vile wingu hufunika jua na kusababisha upofu. Wavutaji wako katika hatari ya kupofuka ghafla mara 16 ikilinganishwa na wenzao wasiovuta. Hii ni kwa sababu kemikali zilizomo kwenye moshi huzuia damu kusambaa kwenye jicho hivyo kulisababisha kushindwa kuona.

Kulingana na Aishah Fazlanie mmoja wa wataalamu waliofanya utafiti huo nchini Uingereza, idadi kubwa ya watu duniani wanafahamu kuwa sigara inasababisha maradhi ya kansa ya mapafu lakini asilimia zaidi ya 80 hawafahamu kuwa sigara inadhuru macho pia.

Ugonjwa huu husababishwa kwa njia mbili. Kwanza moshi wa sigara huwasha macho na pili kemikali zilizo ndani ya sigara hupita kwenye mishipa, damu na hatimaye kudhuru macho.

Sigara pia husababisha kudhoofika kwa sehemu ya kati ya macho (retina) na hivyo kupunguza uwezo wa macho kuona vizuri na hata kutofautisha rangi.

• Kuathiri ngozi

Kemikali zinazopatikana ndani ya sigara hupunguza uwezo wa ngozi kujijenga na kulainika. Mvutaji sigara huonekana mzee zaidi kuliko umri wake hasa.

• Kusababisha uziwi

Matumizi ya tumbako husababisha magonjwa mengi ya masikio. Sababu ni kwamba uvutaji wa sigara husababisha uchafu kuganda kwenye mishipa ya damu na hivyo kupunguza mwendo wa damu hadi kwenye sehemu za ndani za masikio.

Moshi na kemikali za tumbako pia hujeruhi sehemu za ndani za masikio na majeraha hayo yanaweza kuambukiza hata ubongo. Yote haya yanaweza kusababisha uziwi.

• Saratani ya ngozi

Kemikali za sigara husababisha vidonda kwenye ngozi ambavyo haviponi kwa urahisi. Baada ya muda hugeuka kuwa saratani. Sigara huleta magonjwa mengi ya ngozi kama vile uvimbe, kuwashwawashwa na hudhoofisha hali ya ngozi.

Zaidi ya kemikali 40 zinazopatikana kwenye tumbako zimethibitishwa kusababisha saratani.

• Magonjwa ya meno

Sigara hutatiza mdomo na kuongeza uchafu unaoganda kwenye meno hivyo kusababisha kuoza kwa meno, harufu mbaya mdomoni na uchafu wa meno.

Sigara pia hutatiza kupona kwa vidonda hasa baada ya kung’olewa kwa jino. Saratani ya mdomo na ulimi inapatikana zaidi kwa wavutaji sigara na watumiaji wa tumbako za aina nyingine.

• Magonjwa ya mapafu

Uvutaji wa sigara ndio sababu kubwa zaidi ya saratani ya mapafu. Pia husababisha kupasuka kwa vibofu vya hewa safi na kutoa harufu mbaya mwilini.

Wavutaji pia hupata saratani ya koromeo na kuziba njia ya hewa na hivyo basi inabidi kutobolewa kwa kishimo kwenye shingo ili kuwezesha mwathiriwa kupumua.

• Mifupa

Tumbako inasababisha mifupa kuwa myepesi na kupunguza nguvu. Sababu ni kuwa kemikali zilizoko ndani ya sigara hupunguza uwezo wa mwili kujenga mifupa iliyo na nguvu.

Mifupa kama hii huvunjika kwa urahisi na kuchukua muda mrefu sana kupona. Mvutaji sigara anakabiliwa na uwezekano wa mara 22 zaidi kupata kansa ya mifupa.

• Ugonjwa wa moyo

Sigara ndio sababu kubwa zaidi ya magonjwa ya moyo. Inasababisha moyo kupiga kwa kasi zaidi na hivyo kuongeza msukumo wa damu mwilini. Mwishowe husababisha mshtuko wa moyo na hata kifo.

Moja kati ya kila vifo vitatu ulimwenguni hutokana na magonjwa ya moyo na kulingana na Shirika la WHO, huua zaidi ya watu milioni moja Afrika.

• Vidonda vya tumboni

Sigara hupunguza uwezo wa mwili kujikinga dhidi ya viini vinavyosababisha vidonda tumboni. Pia hupunguza uwezo wa tumbo kustahimili nguvu ya asidi baada ya kula.

Vidonda vya mvutaji huwa vigumu kutibu, na mara nyingi hutokea tena baada ya kupona.

• Vidole na kucha

Kutu ya sigara hukusanyika na kuganda kwenye kucha na vidole. Kisha hubadilisha rangi ya vidole na kucha kuwa za manjano au maji ya kunde. Ngozi ya vidole pia hukauka na kuwa ngumu sababu ya joto na kemikali za sigara.

• Hutatiza mimba

Sigara huongeza hatari ya kupata saratani ya mfuko wa uzazi. Ni vigumu zaidi kwa mwanamke mvutaji sigara kutunga mimba na ni rahisi sana ujauzito kutoka.

Uvutaji wa sigara pia humfanya mwanamke kumzaa mtoto mfu au aliye na uzito usiotimia wa kawaida-chini ya kilo mbili.

Watoto hawa huwa na afya duni baadaye. Sababu ni kuwa kemikali za sigara huathiri ukuaji wa mtoto akiwa tumboni. Sigara pia inaweza kusababisha utasa.

• Kupunguza nguvu za kiume

Sigara inapunguza mpigo wa damu kwenye sehemu za uume. Sigara pia huharibu mbegu za wanaume na watoto wanaowazalisha huwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kupata magonjwa ya saratani. Sigara pia huwafanya wanaume kuwa gumba.

• Uvimbe mishipani

Husababisha ugonjwa wa uvimbe kwenye mishipa ya damu miguuni na mikononi.

Mishipa hii huzibika na kuzuia mwendo wa damu kwenye sehemu zilizoathirika. Isipotibiwa kwa haraka, mvutaji anaweza kukatwa miguu au mikono.

Mvutaji wa tumbako hukabiliwa na hatari ya kupata saratani ya pua na ulimi maradufu na kupata saratani ya tumbo mara tatu zaidi kuliko asiyevuta.

Wataalamu wanasema kwamba watumiaji wa tumbako wanakabiliwa na hatari ya kupata saratani ya figo mara tano zaidi kuliko wasioitumia.

Tafiti zinaonyesha kuwa matumizi ya tumbako yanaweza kusababisha matatizo ya koo, koromeo na kwamba kuna uhusiano kati ya uvutaji sigara na saratani ya matiti.

You can share this post!

Alipia kitanda alichovunja akimumunya uroda

Selfie kutumika kupima presha

adminleo