SHINA LA UHAI: Visa vya mimba kuharibika vyaongezeka nchini
Na LEONARD ONYANGO
WALIPOKUWA wakichumbiana miaka sita iliyopita Naomi Makini na Philip Mwangi waliafikiana kupata watoto watatu tu na kisha kufunga uzazi.
Ilipofika Juni 2013, wawili hao waliooana na kuishi pamoja mtaani Kayole, jijini Nairobi. Miezi sita baadaye, Naomi alikuwa mjamzito.
“Nilipoenda kliniki kwa mara ya kwanza, ujauzito ukiwa na miezi miwili, niliambiwa kuwa ningezaa mtoto mnene hivyo nilihitaji uangalizi wa karibu wa daktari,” anaelezea Naomi.
Aliporudi kliniki miezi miwili baadaye daktari alimwambia kwamba alikuwa na watoto wawili.
“Niliporudi nyumbani nilipasua mbarika kwa mume wangu kuwa tulikuwa tukitarajia watoto pacha. Nilidhani kwamba angeshtuka lakini alifurahi. Alisema azma yetu ya kutaka kuzaa watoto watatu ingetimia mapema kuliko tulivyotarajia,” anasema.
Wasichana hao pacha sasa wanasoma Gredi 1. Lakini juhudi za Mwangi, 34, na mkewe kupata mtoto wa tatu zingali hazijazaa matunda. Naomi, 30, amepoteza mimba tatu.
Mnamo 2017, Naomi alipata ujauzito lakini furaha yao ya kupata mtoto wa tatu ilifikia kikomo miezi mitano baadaye.
“Nilipata matone ya damu na nikachukulia kuwa jambo la kawaida. Siku mbili baadaye tulienda katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki na nikaambiwa kuwa mimba ilikuwa imeharibika.
“Tulizama kwenye maombi na kusoma neno la Mungu ili kujiliwaza,” anaelezea.
Mara baada ya Naomi kugundua kwamba alikuwa mjamzito Julai 2018, alianza mapema kutafuta ushauri wa daktari kuhakikisha kuwa mtoto anakua vyema bila matatizo.
Lakini baada ya miezi saba, walipigwa na butwaa walipoambiwa na madaktari kwamba mapigo ya moyo ya mtoto yalikuwa chini.
Mwezi mmoja baadaye, daktari aliwaeleza kuwa mtoto alikuwa ameacha kukua – ishara kwamba kijusi kilikuwa kimekufa.
Madaktari waliondoa kijusi na kisha kuwashauri kungojea kwa miezi sita kabla ya kujaribu tena kupata mtoto.
Naomi anasema kuwa kilichowavunja moyo ni kwamba hakuna daktari aliyeweza kuwaelezea sababu za mimba kuharibika ilhali.
Mnamo Mei, mwaka huu, wakati Rais Uhuru Kenyatta aliweka marufuku ya kutoingia na kutoka jijini Nairobi, Naomi alipoteza ujauzito wa tatu.
“Watoto pacha nilijifungua vizuri bila tatizo lolote. Lakini sasa sijui kinachosababisha mimba kuharibika. Tumemwachia Mungu afanye mapenzi yake,” anasema huku akionekana kukata tamaa.
Naomi ni miongoni mwa maelfu ya akina mama ambao hupoteza mimba kila mwaka.
Kulingana na Dkt James Gitonga wa Idara ya Afya ya Uzazi katika wizara ya Afya, Nairobi inaongoza kwa visa vya kuharibika kwa mimba na vifo vya akina mama wajawazito.
Takwimu
Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa mimba 1,045 ziliharibika jijini Nairobi huku akina mama 134 wakifariki wakati wa kujifungua 2018.
Dkt Gitonga anasema kuwa Nairobi inaongoza kwa kuwa na visa vingi kwa sababu ina idadi kubwa ya watu ikilinganishwa na kaunti nyingine.
Mwaka wa 2018, wanawake 539 walipoteza mimba katika Kaunti ya Kiambu, Nakuru (461), Mombasa (449), Kisumu (339), Kakamega (447), Kilifi (530), Kisii (284), Nyandarua (276), Bungoma (311), Kitui (315), Mandera (301), Narok (442) na Siaya (319).
Ripoti ya wizara ya Afya iliyotolewa 2017 inaonyesha kuwa kufariki kwa mtoto akiwa tumboni kunaweza kuhatarisha maisha ya mama.
Asilimia 30 ya akina mama waliofariki wakati wa kujifungua 2014, kulingana na ripoti hiyo, mtoto alifia tumboni.
Anasema mimba inaweza kuharibika kutokana na mama kupatwa na maradhi kama vile malaria, kisonono na virusi vya HIV wakati wa ujauzito.
“Maradhi kama vile shinikizo la damu, unene kupindukia na kisukari pia yanaweza kusababisha mimba kuharibika,” anasema.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) ya 2020 inaonyesha kuwa mmba 30,000 ziliharibika nchini Kenya mwaka jana
Takwimu hizo za UN zinamaanisha kuwa wanawake watatu nchini Kenya wanapoteza mimba kwa saa.
Ripoti hiyo iliyotolewa kwa ushirikiano wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) na Benki ya Dunia (WB), inaonyesha kuwa Kenya ni miongoni mwa mataifa barani Afrika ambapo visa vya mimba kuharibika vinaongezeka kila mwaka.
Aidha inaonyesha kuwa mimba 19 kati ya 1,000 huharibika humu nchini.
Kenya ingali na kibarua kigumu cha kupunguza kiwango cha mimba zinazoharibika kulingana na mpango wa kunusuru maisha ya watoto wanaozaliwa (ENAP) ambao umeidhinishwa na mataifa yote 194, wanachama wa WHO.
Kulingana na malengo ya ENAP, idadi ya mimba zinazoharibika zinafaa kuwa chini ya 12 kati ya 1,000 kufikia 2030.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kila sekunde 16, dunia hupoteza mtoto mmoja kupitia kuharibika kwa mimba.
Mimba 200 huharibika kila baada ya saa moja kote duniani. Jumla ya mimba milioni 2 huharibika kila mwaka kote duniani, kwa mujibu wa ripoti hiyo yenye jina; Janga Lililotelekezwa: Tatizo la mimba kuharibika duniani 2020.
Nini kinasababisha watoto kufariki wakiwa tumboni kabla ya kuona jua?
Ripoti ya UN inasema kuwa huduma duni ambazo akina mama nchini wanapata hospitalini wakati wa ujauzito zinachangia katika ongezeko la mimba kuharibika.
“Serikali haijawekeza fedha za kutosha katika huduma za kusaidia akina mama wakati wa ujauzito. Vilevile, idadi ya wahudumu wa afya wanaoshughulikia afya ya uzazi ni ndogo,” inasema.
Ripoti hiyo pia inalaumu serikali kwa kukosa mwongozo mwafaka kuhusu jinsi ya kupunguza visa vya kuharibika kwa mimba.
“Visa vingi vya kuharibika kwa mimba huwa haviripotiwi katika vituo vya afya hivyo ni vigumu kwa serikali kujua idadi kamili ya mimba zinazoharibika,” inaongeza.
Kulingana na UN, asilimia 40 ya vifo vya watoto kabla ya kuzaliwa vinaweza kuepukika.
“Asilimia 40 ya vifo vya watoto ambao hawajazaliwa, hutokea wakati wa utungu. Vifo hivyo vingeepukika iwapo mama angepewa huduma bora na uangalizi wa hali ya juu kabla ya kujifungua,” inasema ripoti.
Huduma za afya ya uzazi pia ni ghali hivyo huwafanya baadhi ya akina mama kutafuta huduma za uzazi kutoka kwa wakunga wa kienyeji na kuhatarisha maisha ya watoto wao.
Kumwona mtaalamu wa afya ya uzazi mara moja inagharimu kati ya Sh2, 000 na Sh5,000. Wengi wa akina mama wasiokuwa na bima hawawezi kumudu gharama hiyo.
Takwimu za Sensa ya 2019 zinaonyesha kuwa asilimia nne ya watoto 1,178,260 waliozaliwa kati ya Agosti 8 na Agosti 2019, walizaliwa kwingineko mbali na vituo vya afya.
Ripoti ya Sensa inaonyesha kuwa watoto 173,847 hawakuzaliwa hospitalini katika maeneo ya vijijini. Wengine 15,617 hawakuzaliwa hospitalini licha ya mama zao kuwa katika maeneo ya mijini.
Asilimia 49 ya wakazi wa Kaunti ya Mandera, Marsabit (asilimia 44), Wajir (asilimia 52), Samburu (54), Tana River (43) na Turkana (44) hawakuzalia hospitalini ndani ya kipindi hicho.