Shosho wa Murang’a: Ruto alinipa Sh1.5 milioni ila asipositisha kudhulumiwa kwa Gachagua, nitamtema
KISA cha Mama Margaret Njambi almaarufu Shosho wa Ruto kinahusishwa na mwanamke wa kimuujiza katika kitabu cha Mathayo Sura ya 9: 20-22 ambaye alikuwa akivuja damu kwa miaka 12 na jinsi, huku akiomba usaidizi, alimkabili Yesu aliyekuwa akipita amponye.
Andiko hilo linasema hivi: “Mwanamke mmoja ambaye amekuwa akivuja damu kwa miaka kumi na miwili alikaribia nyuma ya Yesu na kugusa vazi lake. Akajiambia kwamba nikigusa vazi lake tu, nitapona. Yesu aligeuka na kumwona. ‘Jipe moyo, binti wa mtu’ Yesu akasema, ‘imani yako imekuponya.’”
Na mwanamke huyo alipona wakati huo.
Kwa miaka mingi, Mama Njambi, 67, amekuwa amekuwa akivuja “damu” kutokana na umasikini hadi pale aliposikiwa kuwa Mbunge wake Ndindi Nyoro aliandaa mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Gikandu mnamo Januari 12, 2021.
Yeye ni kundi la akina mama wenzake anaowaongoza, waliamua kuhudhuria mkutano huo.
Kwa kudura za mwenyezi Mungu, Mjambi aliratibiwa kuhutubia umati huo.
Mama huyo aliyekatiza masomo yake katika darasa la saba, lakini anayezungumza Kizungu anasema alielezea hisia za wenzake wanachama wa “chama” ambao wakati huo walipinga mchakato wa mageuzi ya katiba chini ya Mpango wa Maridhiano (BBI).
“Tulikuwa wafuasi sugu wa Mbunge wetu Ndindi Nyoro na pia wafuasi wa Naibu Rais wakati huo William Ruto ambaye alikuwa akiendesha kampeni ya urais,” anasema.
Hotuba yake ya dakika 12 ilionekana kuchangamsha umati kwani ililakiwa kwa makofi, shangwe na hoi hoi.
“BBI ni nini?. Hatujui ina maana gani!. Sisi ni wafuasi wa Dkt Ruto na atakuwa rais….Nitamfanyia kampeni na nikikutana naye ana kwa ana, nitamrejelea kama rais,” Mama Njambi, almaaruf “Shosho wa Ruto” akasema.
Huku akishangiliwa zaidi hata na Bw Nyoro, nyaya huyo ambaye alianza kuwa mjane mnamo 2008, mumewe alipoanza dunia akasema hivi: “Kila mtu aliye hapa aseme hivi, tunayemjua ni Dkt Ruto na hatutaki BBI.
Alipokuwa akirejea kuketi, kila mtu aliachwa akipiga makofi. Na video ya hotuba yake ilianza kuzungushwa katika mitandao ya kijamii na kuvutia watu wengi.
Habari kuhusu Mama Njambi aliyejaaliwa watoto tisa (wanaume saba na mabinti wawili, wenye umri kati ya miaka 30 na 46), zilipomfikia Dkt Ruto, kupitia Bw Njoro, alimwalika katika makazi rasmi ya Naibu Rais, Karen, Nairobi mnamo Februari 24, 2021.
Kupitia ujumbe katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii X (zamani twitter), Dkt Ruto aliwaambia wafuasi wake hivi.
“Leo nilitangamana na mfanyakazi wa zamani wa timbo la mawe na mkulima mdogo Margaret Njambi, baada ya video yake iliyonaswa wakati wa mkutano wa maendeleo Kiharu kusambaa. Alielezea nia ya kukutana na Naibu Rais ‘Macho kwa Macho’. Nilikubali kupiga jeki shughuli zake za kilimo.”
Wale wanaomfahamu Mama Njambi mjini Murang’a ambako ameishi kwa miaka mingi wanamtaja kama “mwanamke mwenye bidii na talanta katika kusukuma malengo yake.”
Anasema kuwa amewahi kuuza chang’aa ili kujikimu kimaisha na amewahi kufungwa jela kwa miaka mitano. Lakini nyakati zingine amekuwa akiwezesha kuachiliwa kwake kwa “njia zingine”.
“Mara kadhaa ningepatikana nikivunja sheria……… kosa langu lilikuwa kwamba mimi ni mwanamke masikini ambaye anajikaza kulisha watoto wake. Kufungwa jela kuliniongezea shida na umasikini hata zaidi. Watoto wangu walikosa nafasi ya kupata elimu na wengine wakageuka chokoraa. Nyakati zingine jela sio taasisi ya kurekebisha tabia bali kuongeza umasikini,” anasema.
Mama Njambi anasema uhusiano kati yake na mumewe ulianza kuwa mbaya tangu 1995 na wakatengana.
“Niliondoka nyumbani kwangu Gikandu kusaka amani mjini Murang’a. Lakini mume wangu alipoaga dunia mnamo 2018, nisitisha biashara ya kuuza chang’aa na kurejea nyumbani kusimamia shamba la familia la ukubwa wa ekari 2.5,” akasema.
Baada ya video yake kuibua msisimko mitandaoni baada ya hotuba yake katika mkutano wa Kiharu, umaarufu wake uliongezeka hata zaidi picha za mkutano wake na Naibu Rais ziliposambazwa katika majukwaa hayo.
“Nilijichuna mara mbili kujihakikishea kuwa sikuwa nimekufa na kwamba kweli nilikuwa katika makazi rasmi ya Naibu Rais nikiwe nimeketi katikati mwa watu mashuhuri. Nikusikia vizuri yale ambayo Dkt Ruto alikuwa akinong’oneza mara kadha sikioni mwangu, nikiwa nimeketi kando yake. Lakini nilimnong’onezea kwamba sina meno, nyumba nzuri na haja yangu kuwekeza katika ufugaji ng’ombe wa maziwa,” anasema.
Baada ya chakula na manong’onezo kukamilika, ulitimu wakati wake kuondoka Karen.
“Sikuamini masikio yangu pale Naibu Rais alipoamuru kwamba nijengewe nyumba ya thamani ya Sh600,000, nipewe ng’ombe wawili wa maziwa na mmoja sharti awe mja mzito na mwingine awe ni wa kukamuliwa maziwa, kwamba niwekewe meno bandia na niwepe Sh300,000 kama pesa za matumizi,” Mama Njambi anafichua kwenye mahojioni ya kipekee na Taifa Dijitali.
Kwa ujumla, anasema, zawadi aliyopewa na Dkt Ruto ilikuwa ya thamani ya Sh1.5 milioni
“Shosho wa Ruto” anaongeza kuwa “maishani mwangu pesa nyingi ambazo nimewahi kupewa ni Sh200…… lakini kule Karen Naibu Rais alinipa noti mpya za jumla ya Sh300,000. Nilimwomba Mbunge wangu kunibebea noti hizo kwani sikujua jinsi ya kuzibeba ndani ya mavazi yangu.”
Mama Njambi alisema awali, amekuwa akipewa pesa kidogo kidogo, “na sikuwahi kuwa na zaidi ya Sh2,000 mfukoni mwangu mara moja.”
Tulipomtembelea nyumbani kwake Agosti 5, 2024 tulipata akifanyakazi shambani mwake.
Nyumba yake ya vyumba vitatu, ambayo Dkt Ruto aligharamia ujenzi wake ungali katika hali nzuri. Imepakwa rangi cha Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Rais.
“Nenda ukamwambia Dkt Ruto kwamba yeye ni mtu mzuri. Lakini hajanishawishi kwamba yeye ni rais mzuri. Anapaswa kuamuru marafiki zake kukoma kumhujumu Naibu Rais Rigathi Gachagua,” akasema.
Anasema anakanganywa na Dkt Ruto aliyemfaa na Ruto kama Rais, akisema “yale anayotendewa Gachagua hayanifurahishi na yanaweza kunifanya kuhamia chama kingine kuelekea 2027”.
Mama Njambi anasema alijisajili kwa kozi ya uendeshaji magari, akaanda kuhudhuria vituo vya mazoezi ya viungo (gym) na kuanza kujifunza kuogelea.
Hata hivyo, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imedinda kumpa cheti cha mienendo kwa misingi kuwa nilisukumwa gerezani.
TAFSIRI: CHARLES WASONGA