• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
SIHA NA LISHE: Mnywaji wa chai yenye tangawizi anapata faida zipi?

SIHA NA LISHE: Mnywaji wa chai yenye tangawizi anapata faida zipi?

Na MARGARET MAINA

[email protected]

TANGAWIZI ni zao ambalo humea katika sehemu mbalimbali duniani na hutumika kama kiungo katika vyakula, kama dawa kwa tiba ya magonjwa na pia kiambato muhimu kwenye vinywaji mbalimbali.

Kilimo cha tangawizi kilianzia katika nchi za Bara Asia, Afrika Magharibi na katika visiwa vya Caribbean.

Ili uweze kuwa na afya bora, unashauriwa kunywa chai ya tangawizi kwa wingi ili uweze kujikinga na kutibu magonjwa mbalimbali.

Zifutazo ndizo faida za kunywa chai ya tangawizi:

Huondoa harufu mbaya ya kinywa

Tofauti na vyakula vingine kama kitunguu saumu, tangawizi husaidia uwe na harufu nzuri unapopumua na kufanya maeneo ya kinywa chako kuwa safi.

Tangawizi husaidia msukumo wa damu

Tangawizi husaidia msukumo wa damu mwilini kwa sababu huupa mwili joto ambalo mara nyingi mwili huhitaji wakati wa usukumwaji wa damu mwilini.

Huondoa mwilini baadhi ya magonjwa au hali mbaya za kiafya

Tangawizi hupunguza na kuondoa kabisa hali mbaya za kiafya kama kikohozi na mafua. Tangawizi pia husaidia kuondosha uchovu hasa asubuhi.

Kwa akina mama wajawazito, tangawizi huwapunguzia homa za asubuhi pindi wanapoamka; na vilevile hutumika kama kichocheo cha utulivu.

Tangawizi husaidia mfumo wa chakula

Husaidia mwili kunyonya virutubisho kwenye chakula. Hii husaidiana sana pale unapoamua kupunguza uzito wa mwili na kupata virutubisho vilivyo muhimu.

Kurekebisha sukari ya mwili

Tangawizi husaidia katika kuweka sawa kiwango cha sukari kwenye damu. Wagonjwa wa Kisukari wanashauriwa kutumia Tangawizi kwa wingi.

Tangawizi huongeza hamu ya kula (appetizer)

Huongeza hamu ya kula chakula. Kwa wale wenye mfumo mbaya wa umeng’enyaji wa chakula, wanashauriwa kutumia tangawizi ili kupata mfumo mzuri wa mmeng’enyo wa chakula.

Kuyeyusha mafuta mwilini

Tangawizi husaidia kupunguza kuganda kwa mafuta mwilini ambayo yana madhara makubwa; hasa magonjwa ya kiharusi na shinikizo la damu.

Husaidia kuondoa sumu mwilini

Tangawizi husaidia kupunguza kichefuchefu na hali ya kuhisi kutapika. Pia huwasadia sana wale watu waliotumia sana dawa ama za tiba au za kulevya na kuwa na sumu nyingi mwilini.

Tangawizi husaidia kutibu vidonda vya tumbo

Kwa asilimia kubwa tangawizi humsaidia mtu mwenye vidonda vya tumbo kwa kupunguza maumivu na hata kuponya vidonda hivyo kama vitakuwa kwenye hatua za mwanzomwanzo.

You can share this post!

MAPISHI: Jinsi ya kupika maini ya ng’ombe

Griezmann aona Ronaldo si lolote si chochote kwa Messi

adminleo