Siku ambayo Raila aliwaka bungeni
Mnamo Machi 18, 2008, aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga alizungumza Bungeni akipinga siasa za ubaguzi wa kabila na mgawanyiko, mambo ambayo, alisema, yalikuwa yakisambaratisha nchi.
Huku nchi ikiendelea kuomboleza kifo cha Odinga aliyefariki akitibiwa India wiki iliyopita, kiongozi huyo mkongwe wa upinzani aliwaambia wabunge kuwa alikuwa na ndoto ya nchi ambayo hakuna mtu atakayenyimwa fursa kwa sababu ya asili yake, na viongozi watakaohubiri amani na kuweka mbele maslahi ya taifa.
Hiyo ilikuwa ndoto ya Odinga miaka 17 iliyopita, japo haionekani kutimia, kama inavyoonekana kutokana na kauli za Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, aliyefurahia kifo cha Odinga.
Odinga alikuwa akichangia Mswada wa Marekebisho ya Katiba ya Kenya wa mwaka 2008, baada ya kuingia kwake katika serikali ya mseto na Rais mstaafu Mwai Kibaki iliyoundwa kufuatia uchaguzi wa mwaka 2007 uliosababisha ghasia za baada ya uchaguzi.
Sehemu za rekodi za Bunge zilizopatikana na Taifa Leo, Odinga alisema kuwa mazungumzo yaliyoongozwa na Kofi Annan yalipokuwa yakiendelea, baadhi ya viongozi wa upinzani walipokea simu za kuwahimiza wakatae makubaliano na kurudi barabarani kuandama.
“Tulifikia hatua ambapo tulikuwa tunapokea simu kila siku kutoka kwa watu wakituambia: Hakuna maridhiano! Tuko katika upinzani na tusubiri miaka mingine mitano; nimetamka na ningependa kusema tena hapa, tulihisi Kenya ilikuwa kubwa na kuu zaidi ya sisi wote,” alisema Odinga.
“Tunahitaji pia kuleta maridhiano miongoni mwa watu wetu. Kwa hiyo, tunahitaji kukabiliana ana kwa ana na mnyama mchafu anayeitwa ubaguzi wa kikabila. Nchi inayogawanyika kwa misingi ya kikabila ni nchi inayopigana yenyewe na hivyo haiwezi kutarajia kuendelea. Tuungane.” aliongeza.
Rekodi zinaonyesha kuwa Odinga alipendekeza nchi ifanye kongamano la kitaifa la ubaguzi wa kikabila ambapo wawakilishi wa jamii zote nchini wangeweza kuungana kujadiliana jinsi zitakavyoishi kwa amani.
“Inapaswa kuwa kosa mtu kumtukana mtu kwa sababu tu amepasuliwa masikio, ameondoa meno mawili au sita, au hajatahiriwa. Tukifanya hivyo, tutaelekea mbele katika kuunganisha watu wetu,” ilisema rekodi.
Katika mchango wake, Odinga pia alikosoa siasa za kulipiza kisasi akisema zinapingana na mafundisho ya Mungu katika Biblia.
“Tusilipize kisasi kwa sababu, kama Biblia inavyosema: Achia Mungu alipize kisasi.” “Tunahitaji kuhisi kuwa kitu kimoja. Tusijitazame kama Wabunge wa PNU, ODM-K, ODM na kadhalika,” Odinga alisema.