• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
Simulizi ya mwanahabari aliyehudumu mochari na kuchuuza kondomu 

Simulizi ya mwanahabari aliyehudumu mochari na kuchuuza kondomu 

NA MWANGI MUIRURI

ILI kutimiza ndoto yake ya kuwa mwanahabari, Mike Githuki, 39, alipitia njia ndefu iliyompitishia biashara ya magendo, huduma katika kibanda cha chakula, uchuuzi wa vitambaa vya hedhi na kondomu, pamoja na ajira mochari.

“Ni njia ambayo imenifundisha mengi na ikanishinikiza kuona maisha kwa uhalisia wa kipekee. Mimi ninajua kuhangaika, najua uchochole na nina ufahamu wa jinsi watu wakisaka riziki huwa na unyonge,” akasema.

Alizaliwa katika kijiji cha Wanjohi kilichoko Kaunti ya Nyadarua akiwa mtoto wa nne katika familia ya watoto saba,

Huku akiachwa yatima akiwa katika shule ya msingi, ilibidi ukoo wao ugawane watoto hao ili wapate malezi na ndipo Bw Githuki alijipata chini ya malezi ya babu yake.

“Nilijipata mikononi mwa babu aliyemzaa marehemu mamangu mzazi. Naye alikuwa mjane na malezi niliyopata yalikuwa hafifu kwa kuwa pia alikuwa akiandamwa na umaskini. Maisha yangu yakageuka kuwa ya bahati tu lakini Maulana akanihifadhi,” anasema.

Alifanya mtihani wake wa kidato cha nne mwaka wa 2006 na akawa ameanguka wakati matokeo yaliachiliwa.

“Ari yangu ilikuwa ya kuwa mwanahabari, kuanguka KCSE hasa katika masomo ya Kizungu na Kiswahili kulinifedhehesha si haba, nikaona kana kwamba nimefika mwisho wa dunia,” anaelezea.

Lakini babu yake alimhimiza arudie masomo yake ya sekondari kwa subira ili afufue ndoto yake na akakubali.

“Nilirejea shuleni na nikajisajili katika kidato cha tatu. Wakati matokeao ya mtihani wa KCSE 2009 yaliachiliwa, nikawa miongoni mwa wanafunzi 81, 048 kati ya wote 330, 000 waliofanya mtihani huo waliofuzu moja kwa moja kuingia chuo kikuu, Nilikuwa nimepata alama ya B-,” anasema.

Lakini mwaliko wake wa kujiunga na chuo kikuu cha Mt Kenya kujipa taaluma ya uandishi wa habari haukufanikiwa kwa kuwa alikosa karo.

“Babu yangu alinituliza kwa kunifadhili na Sh3, 000 ili niende hadi Kaunti ya Busia kuishi na mmoja wa jamii yetu na hapo ndipo nilijipata nikihudumu katika kibanda cha chakula,” asimulia.

Anasema kwamba akiwa katika eneo la Malava aliingia katika genge la kununua kimagendo taulo za hedhi na mawe ya tochi kutoka taifa la Uganda na kisha kuuza upande wa Kenya.

Baada ya kukamatwa mara kadha na kuachiliwa kupitia mlango wa nyuma, akafahamu maisha yake hayakuwa yamepangiwa kuishia jela.

“Nilirejea kwetu nyumbani mwaka wa 2011 na nikasajiliwa katika shule moja ya sekondari kijijini kama kurutu wa kufundisha somo la Hesabu na Fizikia,” asema.

Malipo duni yaliyocheleweshwa yalimpata katika mkondo wa mahangaiko zaidi lakini pesa kidogo alizokuwa amejiwekea akiba alizitumia kujinunulia kamera ndogo na akahamia mjini Naivasha kusaka riziki kupitia upigaji picha.

Mochari ya Naivasha

“Nilikuwa nikipiga picha za watalii Ziwa Naivasha na viunga vyake. Ni katika harakati hizo za kukimbizana na picha nilikutana na rafiki aliyenisaidia kupata kazi katika mochari ya Naivasha,” asema.

Anaelezea kwamba kibarua hicho kilikuwa na majukumu ya kupokea miili ya wafu, kuiosha na kuipakia katika majokofu, wengine wakihitajika kunyolewa maeneo yote yanayomea nywele kama maandalizi ya heshima za mwisho.

“Awamu ngumu zaidi katika kibarua hicho ilikuwa ya kupokea maiti kutoka maeneo ya ajali. Pia kupokea miili ya watoto kulinisononesha. Kushuhudia vilio vya waombolezaji ni hali ambayo ilinivuruga akili kwa kiwango kikuu kiasi kwamba mara nyingine hata mimi nilikuwa naangua kilio, lakini nikifahamu shida zangu za kimaisha, nikapiga moyo konde na nikaendelea na huduma,” anasema.

Akichanganya kazi hiyo ya kuhudumia maiti pamoja na kupiga picha katika mazishi, maisha yake yalianza kung’aa kwa kuwa kwa siku angepata hata pato la Sh10, 000.

Pato hilo lilimwezesha kujiunga na chuo kikuu cha Mt Kenya mwaka wa 2014 na ndipo alianza kurejelea ndoto yake ya kuwa mwanahabari.

Akiwa katika chuo hicho kilichoko Mjini Thika Kaunti ya Kiambu, Bw Githuki alianza kufanya kazi katika Mochari ya General Kago iliyoko mjini humo lakini wakati wanafunzi wenzake walipogundua, wakaanza kumtenga na kumbagua.

“Niliachana na kazi hiyo ya kuhudumia wafu na nikaingilia nyingine ya kuchuuza mipira ya kondomu katika mji wa Thika. Lakini pia nilianza kusakwa na maafisa wa kiusalama na nikaachana nayo,” asema.

Ndipo aliamua kama ni mbaya na iwe na akarejea huduma ya mochari pasipo kujali hisia za wanafunzi wenzake.

“Wanitenge wasinitenge, wanibague wasinibague, nilikuja kuelewa kwamba maisha yalikuwa ni yangu nipambane nayo. Nilifanya kazi hiyo ya mochari Mjini Thika hadi nilipohitimu na shahada ya uandishi habari mwaka wa 2017 na nikaingia mtaani sasa kusaka kazi ya taaluma yangu,” anasema.

Alijipata mwaka wa 2018 ndani ya studio za Kenya Broadcasting Corporation (KBC) kama mtangazaji kurutu na bidii aliyodhihirisha ikamwezesha kupewa kazi ya muandalizi vipindi na pia kuandaa habari katika idhaa ya Coro FM inayotangaza kwa lugha ya Gikuyu.

Aidha, huandaa shoo ya Party Time kila Jumamosi.

Kando na hayo ya utangazaji, Bw Githuki ana mtandao wake wa You-Tube ambapo hupakia kipaji chake kingine cha usanii na uchezaji gitaa.

“Huku nikiwa na ngoma kadha za kimuziki, pia huandaa shoo katika maeneo ya burudani. Maisha yangu yamekuwa ni hayo ya kusukumana, kung’ang’ana na chochote ambacho hujipata mikononi mwangu kama pato, huwa nimekitolea jasho,” asema.

Akiwa baba wa watoto watatu wa kiume, Bw Githuki anasema amekuja kutulia ndani ya imani kwamba ipo siku mahangaiko yake ya kimaisha yatatulia na awe na mafanikio ya ajabu maishani mwake na katika familia yake.

Ujumbe wake ni “jitume, huna budi kujituma na hayo mengine umwachie Mungu mwenye haki kwa wote na yote na atakupanga katika mkondo wako wa ufanisi”.

 [email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kaunti tajiri zashindwa sasa kulipa madeni yao

Vijana wanaounda mapambo kwa kutumia mifupa 

T L