Siri za mkutano wa Kalonzo, Matiangi, Gachagua na vigogo wa upinzani
MKUTANO mkubwa wa upinzani unaolenga kuunda muungano thabiti dhidi ya Rais William Ruto kuelekea uchaguzi wa 2027 umeanza kwa mvutano, baada ya kambi ya kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kupinga ushiriki wa mshirika wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta katika mazungumzo ya uteuzi wa mgombea urais.
Chama cha Jubilee kiliwakilishwa na mwenyekiti wa kitaifa Torome Saitoti – ambaye ni Katibu wa zamani wa wizara katika utawala wa Uhuru – badala ya Katibu Mkuu Jeremiah Kioni ambaye amekuwa akishiriki katika mikutano ya awali. Hatua hiyo ilionekana kuwa jaribio la kupunguza mvutano baina ya kambi ya Kalonzo na ile ya Kenyatta kuhusu nani anafaa kuwa mgombea urais wa upinzani.
Mkutano huo ulivutia sura nyingi maarufu akiwemo Naibu wa Rais wa zamani Rigathi Gachagua, ambaye alikutana kwa mara ya pili katika muda wa siku nne na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i – tukio linalodokeza uwezekano wa Kenyatta kumkubali Gachagua kama mshirika mpya wa kisiasa.
Ajenda ya mkutano huo ilihusisha mambo sita: kuanzisha muungano, mikakati ya kuratibu uungwaji mkono wa kikanda, maandalizi ya mkataba wa ushirikiano, uundaji wa kamati za utekelezaji, mikakati ya kushawishi vijana, na kuibua “dhoruba ya kisiasa” yenye msisimko wa kitaifa.
Hata hivyo, mkutano huo ulikumbwa na migongano kufuatia madai kuwa Kioni alishawishi Jubilee kumuunga mkono Matiang’i kama mgombea wa urais, hali ambayo haikupokelewa vyema na kambi ya Kalonzo. Kalonzo anahisi kuwa yeye ndiye kiongozi mwenye hadhi zaidi katika mrengo huo na hivyo anastahili kupeperusha bendera ya muungano.
Viongozi wengine waliokuwepo ni Martha Karua (People’s Liberation Party), Eugene Wamalwa (DAP-K), pamoja na mawaziri wa zamani Justin Muturi, Mithika Linturi, na Mukhisa Kituyi.
Wengine walitaka mchakato wa uteuzi uwe wa wajumbe kulingana na nguvu za kila chama, huku Kalonzo akisisitiza maridhiano.
Eugene Wamalwa alisisitiza kuwa hakuna mgombea aliyeteuliwa rasmi: “Huu ni mchakato wa kujenga muungano mpana wa upinzani.”
Wakati huo huo, baadhi ya washirika wa Kalonzo walisema kuwa hatua ya Kenyatta kuunga Matiang’i ni ya kutiliwa mashaka. Seneta Dan Maanzo alihoji: “Kama Uhuru alishindwa kumfanya Raila rais akiwa na mamlaka kamili ya serikali, atawezaje kumfanya Matiang’i rais akiwa mstaafu?”
Seneta wa Kitui, Enoch Wambua, alitaja mkutano huo kuwa na uzito mkubwa tangu uchaguzi wa 2022. Alisema: “Hii ni dalili kuwa Ruto atakuwa Rais wa muhula mmoja. Huu si mpango wa kumtengenezea mtu urais – ni harakati za kuikomboa Kenya.”
Naibu Gavana wa Machakos, Francis Mwangangi, alionya viongozi wa upinzani dhidi ya kugawanyika kutokana na tamaa za urais. “Tumewahi kuona serikali ikitumia vyombo vya dola kugawanya upinzani. Lazima tujifunze kuwa umoja ni silaha,” alisema.
Hata hivyo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa KANU Nick Salat alikejeli harakati hizo akisema ni “nyuso zilezile ambazo zimekuwa serikalini kwa miongo kadhaa bila kutoa mabadiliko yoyote kwa Wakenya.”
Lakini mchanganuzi wa siasa Profesa Gitile Naituli alisema muungano wa upinzani ni ishara ya kizalendo. “Hili linaonyesha kuwa viongozi wako tayari kuweka taifa mbele ya tamaa zao binafsi – hiyo ndiyo roho ya Katiba kupitia Ibara ya 10,” alisema.
Kwa upande wake, mtaalamu wa siasa John Okumu alisema huu ni mwanzo wa “mashambulizi ya muungano wa wapinzani kumlenga Ruto,” akiongeza kuwa iwapo viongozi hao wataweza kuweka kando tofauti zao, basi uchaguzi wa 2027 utakuwa wa kihistoria.
Katika taarifa ya pamoja, viongozi hao walilaani mauaji ya watu watano yaliyotokea Kilgoris, na kuitahadharisha Tume ya IEBC kuhusu mchakato wa uteuzi unaoendelea.
Walisema: “Tuna wasiwasi mkubwa kuwa hadi sasa mchakato huo haujakidhi viwango vya juu vya uwazi na uaminifu wa uchaguzi. Tume hii inapaswa kuweka maslahi ya taifa mbele ya siasa za upendeleo.”
Dkt Matiang’i na Dkt Kituyi hawakutia saini taarifa hiyo, ingawa waliidhinisha yaliyomo kwa mujibu wa Muturi.