Sugar beet inachukua muda mfupi kukomaa
HUKU kiwango cha ukumbatiaji kilimo cha sugar beet kikiwa kingali chini, James Kariuki, ambaye ni mtafiti anaamini zao hilo ni bora zaidi kuangazia gapu ya upungufu wa sukari nchini.
Kariuki ndiye mwanzilishi wa International Research and Development Ltd, shirika la kibinafsi linalohamasisha ukuzaji wa sugari beet.
Anataja mmea huo kama njia mbadala ya miwa, kuzalisha sukari.
“Miwa inakomaa miezi 24 baada ya upanzi, huku sugar beet ikichukua miezi sita pekee hivyo basi kuwa bora zaidi katika uzalishaji wa sukari,” anafafanua.
Isitoshe, mmea huo una mazao mengi ukilinganishwa na miwa.
Chini ya matunzo faafu na ya kitaalamu, Kariuki anasema ekari moja ina uwezo kutoa tani 120 hadi 160.
“Miwa inazalisha karibu tani 18.69 kwa kila ekari, mazao hayo yakiwa chini mno, na kinyume na kiwango wastani cha uzalishaji kilichowekwa 2014 na Bodi ya Sukari Kenya cha tani 24,” anaelezea.
Mtaalamu Kariuki anamiminia sifa sugar beet, akisema kando na kuzalisha sukari na mafuta ya stovu, mmea huo pia unatumika kuunda chakula cha mifugo, malighafi ya kutengeneza bidhaa za plastiki kama simu, na ethanol.
Aidha, anaipa serikali changamoto kulainisha mikakati yake ya uidhinishaji mimea yenye tija, akipendekeza taratibu ndefu na zinazochukua miaka na mikaka kupitishwa zinapaswa kutathminiwa.
Hali kadhalika, anaisihi serikali kupiga jeki huduma za utafiti hususan katika sekta ya kilimo ili kuangazia pengo la uhaba wa chakula nchini.