Sugar beet: Mmea mbadala kuunda sukari
KENYA inaendelea kuwa mateka wa uagizaji chakula nje ya nchi licha ya ardhi yake kubwa yenye rutuba, hasa katika maeneo kame ambayo ikitumika vyema itaziba pengo hilo.
Taifa hili huagiza kwa kiasi kikubwa nafaka kama vile mahindi, ngano, na mchele.
Sukari, kiungo kinachotumika sana kwenye vinywaji, pia huagizwa, ingawa wakulima wanasema wakipigwa jeki bidhaa hii itazalishwa kwa wingi nchini.
Uagizaji wa chakula nje ya nchi unagharimu serikali mabilioni ya pesa, mzigo ambao hatimaye hubebeshwa walipa ushuru.
Licha ya sukari kuorodheshwa miongoni mwa bidhaa zinazonunuliwa nje kwa wingi, ulijua upo mmea unaoweza kutumika kuizalisha badala ya miwa?
Kampuni ya Kitaifa ya Utafiti na Maendeleo, ndiyo, International Research and Development Ltd, ina jawabu hili kupitia zao aina ya sugar beet.
“Uhaba wa sukari tunaoshuhudia kama taifa unaweza kuangaziwa kwa kukumbatia ukuzaji wa sugar beet na kuiongeza thamani,” anasema Mwasisi na Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika hilo, James Kariuki.
Sugar beet, ni mmea unaofanana na mboga ambapo mizizi yake inasifiwa kuwa na kiwango cha juu cha sukari.
Ni kati ya bidhaa mbili kuu ulimwenguni zinazofahamika kwa uzalishaji wa sukari.
Aidha, inaorodheshwa kwenye familia ya Amaranthaceae na ina kiwango cha sukari cha kati ya asilimia 15 hadi 20.
Hata ingawa mmea huo unafanya vyema maeneo yenye baridi, ukiwa maarufu Bara Uropa, Amerika Kaskazini na Bara Asia, Kariuki anasema Kenya ina hali bora ya anga na hewa kuukuza.
“Unaweza kukua eneo lolote lile la nchi, ikiwemo maeneo kame,” asema mtafiti huyo.
International Research and Development Ltd, kampuni yenye makao yake makuu Nairobi, ilianza utafiti wa sugar beet kama njia mojawapo kusaka kawi mbadala ya majiko iliyokuwa ikiuza.
“Majiko aina ya Bio-Moto (stovu) tunayohamasisha Wakenya kutumia, yalikuwa yakitumia mafuta yanayotokana na malighafi kuunda sukari lakini kiwanda cha Mumias kilipofungwa miaka kadha iliyopita (japo sasa kimefufuliwa), tulihangaika kupata kawi,” Kairuki anaelezea, akikumbuka jinsi nusra afunge biashara yake.
Ni kupitia utafiti aliofanya kati ya 2017 na 2019, alibaini kuwa sugar beet pia inazalisha mafuta ya stovu.
Kwenye utafiti huo, alishirikiana na Wanasayansi kutoka Bara Uropa na wazalishaji wa mbegu kuibuka na bridi bora kati ya humu nchini na ile ya Uropa.
“Mwaka uliopita, 2023, taasisi ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis) iliidhinisha ukuzaji wa sugar beet kwa minajili ya kibiashara,” Kariuki akafichua wakati wa mahojiano ya kipekee na Akilimali Dijitali.
Mtafiti huyu amefanya jaribio la ukuzaji sugar beet na zaidi ya wakulima 300 katika kaunti ya Kiambu, Kisumu, Kakamega, Narok, na Kajiado.
Mbali na Kenya, mataifa yanayolima mmea huu Afrika ni pamoja na Afrika Kusini, Somalia, Uganda, Tanzania, Ghana, Nigeria, na Ethiopia.
Kwa mujibu wa data za 2022 za Knoema, kiwango cha uzalishaji wa sugar beet Afrika kilipanda kutoka tani milioni 1.71 mwaka 1971 hadi tani milioni 16.8 mwaka 2020, hilo likiashiria ukuaji wa asilimia 5.77 kila mwaka.
Knoema, ni kampuni ya kiteknolojia ya kibinafsi inayoshughulika na masuala ya utoaji data za mimea, iliyoko New York.