SUZZAN ANDANJE: Nimechoshwa na mabosi kunitaka kimapenzi
Na JOHN KIMWERE
NI ndoto ya kila msanii kuona anaimarika katika kazi zake na kutambulika kote duniani.
Suzzan Andanje Makabira haachwi nyuma ameibuka miongoni mwa wanadada wanaolenga kujizolea umaarufu hapa nchini na kufikia viwango vya wasanii mahiri kimataifa.
Anasema anatamani kufikia hadhi yake mzawa wa Nigeria, Omotola Jalade Ekeinde mwigizaji wa filamu za Nollywood bila kusahau Lupita Nyong’o Mkenya anayetamba katika filamu za Hollywood.
”Nilianza kujituma katika uigizaji mwaka 2012 ambapo ninapania kukwea milima na mabonde angalau nifikie kiwango cha Hollywood hivi karibuni,” anasema na kuongeza kuwa anaamini ana kipaji tosha kufanya kweli katika tasnia ya maigizo. Kipindi hicho alianza kushiriki uigizaji chini ya kundi liitwalo Pasha Media Production.
Ndani ya miaka mitatu sasa anaodhoreshwa kati ya waigizaji wengi wa kike wanaojivunia kuchota wafuasi wengi tu kupitia filamu iitwayo ‘Pima Weight’ inayoendelea kupeperushwa kwenye runinga ya K24.
Kwenye filamu hiyo anafahamika kama Jemima ingawa kisanaa anajulikana kama Lady S. Binti huyu anasema anataka kujituma mithili ya mchwa ili kufikia viwango vya kimataifa miaka ijao ingawa tangia akiwa mdogo alidhamiria kuhitimu kuwa mtangazaji kwenye runinga.
Bila shaka wahenga hawakupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa walivyolonga kuwa ‘Vitu vya biashara havigombani.’ ‘
‘Dah! Umbo langu la kuvutia limeibuka tatizo ambapo limesababisha nipoteze nafasi ya ajira mara tatu baada ya kupigia chini ombi la wahusika la kunitaka kimapenzi,” alisema na kuwaponda maprodusa ambao hupenda kuwashusha wanawake hadhi ili kuwapa ajira.
Anajivunia kushiriki ‘Real Househelps of Kawangware,’ ‘ Baba yao’ (KTN), ‘Pima Weight,’ ‘Mambo Mambo,’ ‘Bila Capital’ (K24), ‘Auntie Boss’ (NTV), ‘Tahidi High’ (Citizen TV), ‘Njoro wa Uber,’ ‘Hulaballoo,’ na ‘Varshita’ (Maisha Magic East). Pia ameshiriki filamu iitwayo ‘Majuto’ (Netflix).
Anasema hapa nchini anatamani kufanya kazi na waigizaji kama Catherine Kamau pia Naomi Ng’ang’a ambao wameshiriki filamu kama ‘ Sue and Johny’ na ”Sumu la penzi’ mtawalia.
”Kusema kweli waigizaji hao ni miongoni mwa wasanii ambao hunitia moyo zaidi katika ulingo wa maigizo,” anasema.
Kimataifa angependa kushirikiana na waigizaji wengi tu akiwamo Omotola Jalade na Mercy Johnson wote (Nigeria) pia Jacqueline Wolper (Tanzania).
Katika mpango mzima anasema filamu iitwayo ‘Blood Sisters’ kazi yake Omotola Jalade ndiyo iliyompa motisha zaidi kuzamia sekta ya maigizo.
Binti huyu mwenye umri wa miaka 27 anamiliki brandi iitwayo Badilisha Productions akishiriana na mwenzake Valary Akinyi. Anasema kando na kusaka mkwanja wanapania kukuza waigizaji chipukizi wanaume na wanawake.
Anashauri wenzake wajiheshimu pia watambue malengo yao katika uigizaji wala wasikubali wanaume wawashushe hadhi.
Anawachana waigizaji wepesi ambao hupenda kukubali matakwa ya maprodyuza mafisi ambao huwalazimisha kuingia katika mahusiano ya kimapenzi ili kupata ajira.