Makala

TAHARIRI: Heko Wanyama kuanzisha wakfu

November 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MHARIRI

VYOMBO vya habari vimeripoti jana Ijumaa kwamba mwanasoka stadi wa Kenya, Victor Wanyama ambaye huchezea klabu ya Tottenham Hotspur ameamua kufanya hisani kwa kuanzisha wakfu wake.

Wakfu huo unalenga kuwafaa watoto kukuza talanta zao za michezo pamoja na kuwapa elimu.

Kwa mfano, wapo wajasiriamali au wawekezaji waliofanikiwa zaidi maishani lakini ni nadra sana kuwaona wakitumia pesa zao kuwaauni raia wenzao wanaonyanyasika na maisha.

Japo Wanyama ameanzisha mradi huu kwa kuchelewa, wahenga walisema, heri nusu shari kuliko shari kamili.

Yamkini kiungo huyo maarufu amejifunza somo kutokana na shutuma zilizotolewa dhidi ya ndugu yake, McDonald Mariga aliyewania kiti cha ubunge wa Kibra mapema mwezi huu.

Mwanasoka huyo wa zamani wa klabu za Inter Milan, Parma (Italia), Real Oviedo na Real Sociedad (Uhispania) ambaye anakisiwa kuvuna hela nzuri akichezea klabu hizo za hadhi, alikumbushwa kuwa hakuna alichofanya kuwasaidia raia wa Kenya hasa vijana wasiojiweza licha ya kuvuna mamilioni ya pesa akiwa mwanasoka.

Alilinganishwa na wanasoka wenzake maarufu barani kama vile wastaafu Didier Drogba, Samuel Eto’o, Yayah Toure na mkali wa Liverpool, Sadio Mane ambao wametendea nchi wanazotoka makuu kimaendeleo.

Naam, shutuma hizo zinaonekana kumzindua Victor Wanyama aliyeamua kufanya hisani hii ya kujenga wakfu wake kwenye ardhi ya ekari 21 katika Kaunti ya Busia.

Ni matumaini yetu kuwa kiungo huyo maarufu ataweza kuvutia wahisani wengine wengi kumsaidia katika kukuza wakfu huo wake ili vijana wengi waweze kunufaika.

Nao wanasoka wengine na hata wanariadha wetu ambao huvuna hela nzuri kimataifa, wanafaa waige mfano huo wa Wanyama ili waweze kuwasaidia vijana wengi wenye hamu ya kufaulisha maisha yao lakini hawana msaidizi.

Serikali yafaa ihakikishe kuwa watu wenye roho safi ya kuinua maisha ya vijana kama anavyofanya Wanyama wamesaidiwa kwa njia zote ili kufanikisha juhudi zao hizo.