TAHARIRI: Afisi ya Kadhi Mkuu ipewe heshima yake
NA MHARIRI
WAISLAMU kote ulimwenguni wanapojiandaa kwa Sikukuu ya Idd Ul Adha, kama kawaida mjadala umeibuka kuhusu siku halisi ya kufanya maadhimisho hayo hapa Kenya.
Wakati Waziri wa Uslama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i akitangaza na kuweka kwenye gazeti rasmi la serikali kuwa siku hiyo itaadhimishwa kesho, Kadhi Mkuu Sheikh Ahmed Muhdhar amesisitiza sikukuu ni kesho kutwa Jumatano.
Siku hii huadhimishwa na Waislamu ulimwengu mzima kukumbuka tuko la Abrahamu na mwanawe, alipokuwa amepimwa imani yake na Mwenyezi Mungu. Japokuwa alikuwa ameota ndotoni tu kwamba alikuwa akimchinja mwanawe, alifahamu kuwa ndoto ilikuwa mojawapo ya njia za Mwenyezi Mungu kuwasiliana naye.
Kwa kuthibitisha Imani yake, Mwenyezi Mungu alimteremshia Abrahamu kondoo . Tangu wakati huo, Waislamu hukamilisha ibada ya Hajj katika mji wa Makka, Saudi Arabia na kisha huchinja kutoa sadaka kama alivyofanya Abrahamu.
Kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala kuhusu iwapo Idd hiyo iwe siku ya kumi ya mwezi wa Dhul Hijja au baada ya mahujaji kukamilisha kurusha mawe katika eneo la Muzdalifa.
Vyovyote iwavyo, tangu jadi Waislamu wa Kenya wamekuwa wakifuata mwongozo wa Kadhi Mkuu katika masuala mengi yanayohitaji msimamo mmoja.
Inawezekana Kadhi Mkuu hayuko sahihi katika uamuzi wake kuwa Idd iwe Jumatano, lakini hatua ya baadhi ya wanasiasa Waislamu kumkejeli mitandaoni na kuingiza siasa suala hilo haifai.
Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Aden Duale amemkashifu vikali Sheikh Muhdhar n ahata kuapa kuwasilisha malalamishi rasmi kwa Tume ya Huduma za Bunge.
Kwenye akaunti zake za Facebook na Twitter, Bw Duale anasema kuwa mojawapo ya misingi ya malalamishi itakuwa kifungu cha 170 cha Katiba, ambacho kinafafanua ni yapi majukumu ya Kadhi Mkuu.
Huenda makadhi wana udhaifu wao katika baadhi ya maamuzi wanayotoa, lakini si haki wala heshima kwa kiongozi wa ngazi za juu serikalini kuwakejeli kwenye majukwaa.
Kinachohitajika siku za usoni ni viongozi wa Kiislamu kuketi chini na kujadili kwa mapana masuala yanayowahusu. Baadhi ya mambo hayo ni kuonekana kwa mwezi au hata kama tutakubaliana, tuivunje kabisa afisi ya Kadhi Mkuu. Kwa sasa, ni lazima afisi hiyo na anayeishikilia wapewe heshima wanayostahili kutoka kwa kila Mwislamu.