TAHARIRI: Ahadi kuhusu kansa itekelezwe
Na MHARIRI
HATIMAYE wendazao Gavana wa Bomet Joyce Laboso na Mbunge wa Kibra Ken Okoth wamemaliza rasmi safari yao duniani leo kwa taratibu za mazishi huku taifa zima likiendelea kujizatiti kukabiliana na mshtuko wa kupoteza viongozi hao.
Ikiwa hotuba za wengi wa waliozungumza katika ibada zao za wafu ni jambo la kutiliwa maanani, basi hamna shaka kwamba viongozi hao walikuwa watu wa vitendo na wala sio maneno matupu.
Mumewe Dkt Laboso, Bw Edwin Abonyo alimtaja mwendazake kuwa mwanamke mkakamavu, shupavu na aliyekwepa ufisadi huku akitoa mfano kwamba yeye mwenyewe akiwa mwanakandarasi – wengine watasema mkandarasi – hata hakupata zabuni kutoka kwa kaunti ya Bomet licha ya kuwa mume wa Gavana.
Na kwa upande wa marehemu Ken Okoth, licha ya mgogoro mdogo uliozuka Alhamisi kuhusu kuwepo kwa mtoto anayedaiwa kupata na mke wa pembeni, kwa jumla wengi walikuwa na mengi mazuri ya kusema kumhusu huku miradi yake haswa katika nyanja za kielimu ikionekana wazi kwa kila mtu.
Ibada ya Ijumaa ya Dkt Laboso mjini Bomet ambayo ilihudhuriwa na viongozi mashuhuri wakiwemo Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga pia ilikuwa fursa nzuri kwa taifa kusikiliza kuona kile utawala wa nchi unafikiria kuhusu janga ambalo linatukodolea macho la saratani.
Ingawa Dkt Ruto na Bw Odinga walitumia muda waliopewa kusema masuala kadhaa kuhusu uhusiano wa karibu na mwendazake pamoja na siasa za vyama hapa na pale, ilikuwa ishara nzuri wakati Kiongozi wa Taifa alipotumia fursa yake kuzungumza kwa kutangaza kwamba serikali yake itabuni vituo vya kutoa matibabu na huduma kwa wagonjwa wa saratani katika sehemu mbali mbali kote nchini.
Hiyo ni habari njema na iliyosubiriwa kwa hamu na wengi kwa sababu kama Rais mwenyewe alivyosema kwenye hotuba yake, matibabu na matunzo kwa mgonjwa wa saratani ni ghali mno na familia nyingi haziwezi kumudu.
Kile tunachosema hapa ni kwamba, ahadi hii isigeuke kuwa hewa.
Serikali ianze mara moja kuitekeleza na kuweka imani miongoni mwa umma kwamba inajali maslahi ya wengi wasiokuwa na uwezo.
Kupoteza viongozi wa haiba ya juu kama tuliopoteza kutokana na ugonjwa huo ni idhibati kwamba twahitaji juhudi za dharura kukabiliana na adui huyu.