TAHARIRI: Ahadi ya kumaliza ufisadi itekelezwe
AKIHOJIWA kutwaa nafasi ya Katibu katika Wizara ya Ugatuzi, Bw Nelson Marwa, ameahidi kukabiliana vikali na makundi ya wafisadi na kukomesha utumizi mbaya wa fedha za umma katika serikali za kaunti.
Akipigwa msasa na kamati ya bunge Jumatano, Bw Marwa alijitokeza kuwa mtu mwenye uadilifu na anayejali zaidi maslahi ya Wakenya.
Ingawaje amefanya kazi kwa miaka mingi serikalini, aliwashangaza wanakamati hiyo ya bunge kwa kutangaza kuwa na utajiri wa Sh25 milioni pekee, huku akisema amezingatia zaidi kusaidia jamii kama kudhamini masomo ya wanafunzi, katika maeneo mengi ambayo amehudumu kwa ngazi za utawala.
Hata hivyo, alikiri kuwa kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa pesa za umma hasa katika kipindi cha kwanza cha ugatuzi nchini, hali ambayo alisema lazima idhibitiwe.
Katika taarifa za mkaguzi mkuu wa matumizi ya fedha ambazo zimekuwa zikichunguzwa na Seneti, ni wazi kuwa baadhi ya serikali hizo za ugatuzi hazijaweza kufafanya vilivyo kuhusu pesa zilizoelekezwa kuboresha maeneo hayo ya mashinani. Idadi kubwa ya wasambazaji bidhaa na huduma pia wanalalama kukosa kulipwa na kaunti hizi.
Kwa hivyo, iwapo Bw Marwa atapata kuidhinishwa, ni matarajio ya wengi kuwa akiwa pamoja na Waziri Eugene Wamalwa wataweza kukabiliana na ufisadi na kuhakikisha kuwa Wakenya wanafurahia matunda ya ugatuzi, ambayo dhamira yake kuu, ilikuwa kusongeza huduma karibu nao na kuboresha maisha mashinani.
Tayari kuna suala kama la kaunti ya Nyeri kupendekeza kujenga lango kuu na makao yake makuu litakalogharimu Sh20 milioni, mbali na pendekezo la kujenga nyumba ya gavana itakayogharimu Sh200 milioni.
Baadhi ya masuala haya ndiyo Wakenya wanatarajia yafuatiliwe ili kuhakikisha kuwa pesa za mlipaji kodi zinalindwa na kutumika ipaswavyo.
Vile vile, Bw Marwa alitaja jana suala la mali kuwazungukia wachache tu humu nchini. Ni kweli kuwa ni wachache wanaopata biashara za mabilioni humu nchini, na Wakenya wengi wanatarajia kuwepo kwa usawa ili kuhakikisha kuwa kila pembe ya nchi inafaidika na kujiimarisha kwa njia moja ama nyingine.
Mawaziri wapya walioapishwa pia wameahidi kukabiliana na donda sugu la ufisadi, na kwa sasa Wakenya wanatazama kuhakikisha kuwa wanatimiza ahadi zao kwao.